October 7, 2024

Masomo yanayowatesa zaidi wanafunzi kidato cha sita

Lipo General Studies ambalo huchukuliwa poa na wanafunzi wa ngazi hiyo ya elimu. Hesabu, Kemia na Fizikia bado mziki mzito.

Hata hivyo, General Studies ambalo huchukuliwa poa na baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita limekuwa ni moja ya masomo matano yanayofanya vibaya huku ufaulu wake ukiwa mbovu zaidi mwaka 2016 na 2017 kabla ya kupaa mwaka jana. Picha|Mtandao.


  • Lipo General Studies ambalo huchukuliwa poa na wanafunzi wa ngazi hiyo ya elimu.
  • Hesabu, Kemia na Fizikia bado mziki mzito.

Dar es Salaam. Achana na hesabu au kemia, somo la General Studies ambalo hufundishwa kidato cha tano na sita ni moja ya masomo manne yanayowatesa zaidi wanafunzi wa ngazi hiyo ya elimu katika mtihani wa Taifa.

Uchambuzi wa takwimu za ufaulu kwa masomo za Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) uliofanywa na nukta.co.tz unaonyesha kuwa kwa kipindi cha miaka minne iliyopita (2015-2018) masomo yaliyokuwa na wastani wa chini wa ufaulu ni ‘Advanced Mathematics’, Kemia, Fizikia, General Studies na ‘Basic Mathematics’.

Wakati masomo hayo yakiwa na ufaulu wa chini kuliko mengine, masomo ya sanaa ya Kiswahili, Kiingereza, Historia, Jiografia na Biashara yamekuwa yakifanya vizuri kwa ufaulu wa wastani wa asilimia 99.

Kwa kawaida imezoeleka kuwa masomo ya hesabu na sayansi huwatoa jasho zaidi wanafunzi katika ngazi zote za elimu lakini siyo kwa yale ya sanaa hususan General Studies ambalo pamoja na mambo mengine hujumuisha mada za mawasiliano, ushirikiano wa kimataifa, mazingira, utamaduni, demokrasia na masuala ya kijamii na kiuchumi nchini.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2018 somo lililowatesa zaidi wanafunzi hao lilikuwa ni Basic Mathematics ambalo ufaulu wake ulikuwa wa chini zaidi wa asilimia 55.3 ikiwa ni ahueni kidogo ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2017. 

Katika mtihani wa mwaka 2017, ufaulu wa somo hilo ulikuwa ni asilimia 49.4 ikiwa ni zaidi ya mara moja na nusu chini ya wastani wa ufaulu kimasomo mwaka huo.


Zinazohusiana:


Somo jingine ambalo wastani wa ufaulu wake umekuwa ni mdogo kuliko mengine kwa kipindi hicho ni Advanced Mathematics ambalo husomwa na wanafunzi wanasoma michepuo yenye hesabu kama PCM, PGM and EGM.

Kwa miaka minne mfululizo ufaulu wa somo hilo haujawahi kuvuka asilimia 85 ikilinganishwa na Kiswahili ambalo huongoza kila mwaka kuwa na wastani wa ufaulu wa asilimia 99.9.

Hata hivyo, General Studies ambalo huchukuliwa poa na baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita limekuwa ni moja ya masomo matano yanayofanya vibaya huku ufaulu wake ukiwa mbovu zaidi mwaka 2016 na 2017 kabla ya kupaa mwaka jana.

Katika mtihani uliofanyika mwaka 2018, wastani wa ufaulu wa General Studies ulikuwa asilimia 94.4 ukiwa umepanda kutoka asilimia 63.7 uliorekodiwa mwaka 2017.

Lakini katika mitihani ya mwaka huu, wanafunzi watalichukulia poa somo la General Studies au watafanya vizuri?