Matarajio ya wadau bajeti kuu ya Serikali Tanzania 2020-21
Hii ndiyo bajeti ya mwisho ya kipindi cha kwanza cha uongozi wa Rais John Magufuli na inawasilishwa kipindi Tanzania inakabiriwa na athari za corona.
- Wadau washauri kupunguzwa kwa kodi na tozo kwa wafanyabiashara hasa wa wadogo.
- Bajeti ijielekeze kuwainua wakulima na tafiti za Taifa.
Dar es Salaam. Zimesalia siku tatu tu Watanzania kujumuika na wenzao wa Afrika Mashariki kufuatilia bajeti za nchi zao zitakazoweka wazi mapato na matumizi kwa mwaka 2020/2021 na mustakabali wa maendeleo ya mataifa yao.
Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) za Kenya, Uganda, Tanzania na Rwanda zimejiwekea utaratibu wa kusoma bajeti kwa siku moja. Ni Burundi na Sudani Kusini pekee ambazo hazifuati utaratibu huo.
Bajeti hizo zinasubiriwa kwa hamu na wengi kwa sababu zitaweka baya uwepo wa unafuu au ugumu wa maisha ya wananchi wa kawaida, wafanyakazi na biashara kwa mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai mosi.
Bajeti ya Serikali huweka bayana miradi ya maendeleo ya Serikali, mikakati ya kikodi na isiyo ya kikodi ambayo baadhi huwa ni mzigo huku mingine ikipelekea ahueni kwa wananchi.
Tofauti na miaka mingine, bajeti ya mwaka ujao wa fedha itakayowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango, ndiyo bajeti ya mwisho katika kipindi cha kwanza cha uongozi wa Rais John Magufuli.
Pia, bajeti hiyo safari hii itawasilishwa wakati Taifa likikikabiliwa na athari za janga la virusi vya corona ambavyo vimeathiri sekta mbalimbali za uchumi ukiwemo utalii.
Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango akiwasilisha bajeti ya wizara yake Mei 15 mwaka huu. Wengi wanasubiria kuiona mipango ya Dk Mpango katika Bajeti Kuu ya Serikali Juni 11.
Makadirio ya awali ya bajeti hiyo ya 2020/2021 ya Tanzania yaliyowasilishwa na Dk Mpango bungeni yalikuwa Sh34.88 trilioni kutoka Sh33.1 trilioni ya mwaka 2019/20.
Je, wadau wanatarajia nini kutoka kwenye bajeti hiyo ya mwisho ya kipindi cha kwanza cha Serikali ya Rais Magufuli itakayowasilishwa bungeni Dodoma Juni 11?
Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) limesema linatarajia bajeti ya Tanzania na nchi nyingine za EAC zitajumuisha virushi wezeshi vya uchumi kukabiliana na athari za COVID-19 ili kuchochochea ukuaji wa uchumi.
EABC katika taarifa yake iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita imependekeza kulegezwa kwa sera za kodi katika ukanda huo ili kuwapa ahueni wananchi na wazalishaji viwandani ikiwemo kuondoa kabisa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa bidhaa muhimu zinazotumika kipindi hiki cha COVID-19. Bidhaa hizo ni pamoja na barakoa, vitakasa mikono.
Pia Serikali za EAC zimeshauriwa kupunguza VAT kutoka kiwango cha sasa cha kati ya asilimia 16 na asilimia 18 hadi asilimia 1 hadi asilimia 14 ili kuchochea matumizi ya bidhaa na huduma za ndani kwa wananchi wa kawaida.
“Ili kuwapa ahueni wafanyakazi ya athari za janga la COVID-19, EABC inapendekeza nchi wanachama wa EAC kupunguza kiwango cha kodi ya mshahara (Paye) kutoka asilimia 30 hadi asilimia 25,” imeeleza taarifa ya EABC.
Zinazohusiana:
- Dk Mpango: Uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 4 mwaka 2020
- Serikali yaanika bajeti ya mwaka 2019-20
Mwanaharakati na mwanachama wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Jovita Mlay amesema anatarajia bajeti ya mwaka ujao itajikita kuweka mikakati ya kuwatengenezea mazingira rafiki wafanyabiashara wadogo hasa wasio na maeneo yasiyo rasmi ili kuboresha afya na kipato chao.
Amesema baada ya Rais Magufuli kutoa vitambulisho vya mjasiriamali, wananchi wengi wamejitokeza kufanya biashara na kuibua changamoto ya uchafuzi wa mazingira hasa barabarani na kwenye mitaro ya mitaa, jambo linalotishia afya zao ikiwemo kupata maambukizi ya magonjwa mengine nje ya corona.
Wakati Mlay akiwakumbuka wafanyabiashara wadogo, wengine wamesema pia wakulima hasa wanawake wa vijijini wanatakiwa kuangaliwa kwa jicho la tatu katika bajeti hiyo ili kuwaongezea tija katika shughuli zao.
Mjasiriamali na Mwanzilishi wa Shirika la wanawake katika jitihada za kimaendeleo (WAJIKI) Janeth Mawinza amesema kutokana mafuriko yaliyotokea mwaka huu, mazao ya wakulima yameharibiwa sana na hivyo wanahitaji kuwekewa mkakati wa fidia au ruzuku itakayowainua kulima hata mazao yanayokomaa muda mfupi.
“Iwe ni bajeti ambayo itakayopeleka fidia kwa wakulima hasa wanawake ambao tegemeo lao ni kilimo,” amesema Mawinza.
Amesema bajeti iangalie namna ya kuwapa ahueni wakulima hasa wale ambao wamechukua mikopo benki na hawana pembejeo za kilimo ili kuwapunguzia mzigo wakati wa mavuno.
Tangazo:
Ahueni ya kodi na tozo
Moja ya jambo linaloibua mjadala kila mwaka ni utitiri wa kodi za Serikali kwa watu, biashara na kampuni.
Macho na masikio yapo kwa Dk Mpango kujua ni kodi gani zitafutwa, kupunguzwa au zitaongezwa ili wananchi wajipange watakavyoweza kuendana nazo. Je, itakuwa ni bajeti ya kuzikamua bia na sigara?
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Prof Honest Ngowi amesema ni vema bajeti ikatathmini mazingira wezeshi ya walipa kodi ili kuhakikisha viwango vitakavyopangwa vinalipika.
Amesema ni kweli Serikali inahitaji kodi kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za jamii na miundombinu lakini kodi hizo zisiwe mzigo utakaozifanya biashara au kampuni kushindwa kujiendesha kwa faida.
“Katika muitikio wa kisera ambao tumekuwa tukizungumza ni sera pana za kikodi kwa maana ya kuwepo kwa kodi chache zaidi lakini viwango vidogo vya kodi.
“Pia haitakuwa rahisi sana kwa sababu Serikali inahitaji hizi fedha lakini tukifanya hivyo hata kama tutakusanya kodi kidogo tutakuwa tumeacha ahueni kwa walaji na kampuni kusudi zisife kabisa,” amesema Prof Ngowi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi ya Dar es Salaam.
Amebainisha kuwa kwa hali ya sasa ambapo dunia inakabiliwa athari za janga la VOVID-19, ni vema Serikali ikaangalia vyanzo vingine vya mapato ili kukamilisha miradi ya maendeleo.
Majanga ya asili, Corona yasiachwe nyuma
Wadau wa maendeleo wamesema kutokana na janga la Corona, bajeti ni lazima iangalie namna ya kuweka mikakati ya kisera ya muda mfupi na mrefu ya kukabiliana na athari hasa za kiuchumi ili wananchi warejee katika shughuli za kawaida.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Equity for Growth (EfG) Jane Magigita amesema Corona imeathiri zaidi makundi yasiyojiweza na yaliyo pembezoni na hivyo bajeti ioneshe ni jinsi gani itawakwamua kiuchumi.
“Bajeti hii lazima iangalie athari ya janga la COVID-19 na kuanza kushughulikia makundi ya jamii yaliyoathiriwa zaidi hasa waliopoteza ajira au waliopoteza uwezo wa kuzalisha, la sivyo itashindwa kuakisi uhalisia na kushughulikia changamoto halisi za jamii,” amesema Magigita.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) katika uchambuzi wake wa bajeti za wizara mbalimbali kwa mwaka 2020/21 kimeeleza kuwa nchi ina wajibu wa kuendelea na juhudi za kupambana na kuweka mikakati itakayowezesha Taifa kuendelea kipindi ambacho shughuli mbalimbali zimepungua kutokana na tishio la COVID-19.
Naye Mtafiti wa kutoka taasisi ya afya ya Ifakara (IHI) Dk Grace Mhalu amesema bejeti iangalie uwezekano wa kutunisha mfuko wa kushughulikia athari za majanga na kuongeza fedha kwa ajili ya tafiti za kitaifa.
“Jambo la kwanza ambalo ningeshauri ambalo lionekane kwenye bajeti ni kuongeza nguvu kwenye tafiti. Ili tuweze kuendesha sekta ya afya na zingine tunahitaji tafiti ziweze kutupa majibu ya kile tunachotakiwa kufanya kwa wanawake na wadau wa maendeleo,” amesema Dk Mhalu.
Tukutane Juni 11 katika bajeti kuu ya Serikali. Nukta tutakuletea yatakayojiri bungeni.
Habari hii imeandikwa na Daniel Samson na Rodgers George.