November 24, 2024

Matarajio ya Watanzania kuelekea bajeti ya kwanza Serikali ya Rais Samia Tanzania

Wengi wanatarajia bajeti kuu ya Serikali mwaka 2021/22 itawasaidia kujikwamua katika lindi la umaskini kwa kutoa fursa zaidi za ajira, kupunguza mzigo wa kodi.

  • Wafanyabiashara wanatarajia serikali kuboresha miundombinu ya kufanyia kazi wajasiriamali wadogo na kupunguza mzigo wa kodi.
  • Vijana wanaishubiri bajeti hiyo kuona kama itafungua fursa za ajira.
  • Wengine wanategemea Serikali kujikita katika kukuza soko la bidhaa na huduma zinazozalishwa na Watanzania.

Dar es Salaam/Mwanza. Saa chache kabla ya kusomwa kwa bajeti kuu ya Serikali, Watanzania mbalimbali wametoa matarajio yao huku wengi wakisisitiza bajeti hiyo ya kwanza kwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ijikite katika kukuza uchumi wa nchi na uchumi wa mtu binafsi.

Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba leo Juni 10, 2021 anatarajiwa kuwasilisha bajeti kuu ya Serikali majira ya Saa 10 jioni kabla ya kuanza kujadiliwa na wabunge na kupitishwa.

Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam wanatarajia kuwa bajeti itakayosomwa leo itajikita katika kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuwaondoa katika lindi la umaskini na kukuza uchumi wa taifa.

Mfanyabiashara wa mihogo eneo la Victoria, Mwanahamisi Mbaruku ameiambia Nukta Habari kuwa anatarajia Serikali itawakumbuka wajasiriamali wadogo wadogo kwa kuwapatia maeneo mazuri ya kufanyia kazi bila usumbufu..

“Kila siku ubebe majiko, masufuria na kuni. Kama ningekuwa na eneo maalumu, ningeviacha tu,” amesema Mbaruku huku akibainisha maeneo maalum ya wafanyabiashara wadogo kama Machinga Complex yangejengwa kila wilaya, kata hadi mitaa.

Wengine wanatarajia bajeti ya kwanza ya Serikali ya Rais Samia itajikita katika kutengeneza fursa za ajira kwa ajili ya vijana ili kuliwezesha kundi hilo kujikwamua na hali ngumu ya maisha kwa kukosa ajira na fursa nyingine za kiuchumi.

Mkazi wa Morogoro, Kennedy Luhende amesema anatarajia kuona bajeti ikisaidia kuanzishwa kwa miradi ambayo itatoa fursa za ajira kwa vijana wengi hasa ambao hawajafikia kiwango cha juu cha elimu.

Baadhi ya wafanyabiashara wadogo wadogo katika soko la Lushoto mkoani Tanga. Wafanyabiashara wadogowadogo wanatarajia bajeti itawaangalia kwa kuandaa maeneo maalum ya kufanyia biashara. Picha|K15. 

Luhende amesema Serikali  imefanya mengi kwa ajili ya kuwawezesha vijana kujiajiri kwa kurahisisha kodi za wajasiriamali na kuboresha huduma za ulipaji kodi lakini bado wapo vijana ambao hawana elimu na mitaji lakini wana nguvu za kufanya kazi.

“Kuna miradi mingi inaendelea. Kuna treni, madaraja na kadhalika. Natarajia kwa bajeti ya mwaka huu Serikali ianzishe miradi mingine ambayo itatoa ajira kwa vijana kujipatia fedha za mitaji na kuendesha maisha yao. Hilo litapunguza waathirika wa madawa ya kulevya mitaani,” amesema Luhende.

Ikuze masoko ya bidhaa za Watanzania

Mbali na matarajio ya jumla ya kuondoa umaskini, wengine wanatarajia bajeti hiyo itawasaidia Watanzania kupata masoko ya bidhaa na huduma zao na kupunguza gharama za kufanya biashara.

Kwa mjasiriamali wa kuzalisha pilipili, Stella Ngambeki anatarajia Serikali itapunguza uingizwaji wa bidhaa ambazo zinashindana moja kwa moja na bidhaa zenye ubora sawa na hata zaidi ambazo zinazalishwa na Watanzania.

Ngambeki ameiambia Nukta Habari kuwa kwa sasa ukitembelea maduka makubwa maarufu kama “supermarket”, pilipili nyingi ni zile zinazotoka nje ya nchi.

“Wachache sana ambao wameweza kufikia hilo soko. Wengi wetu tumebaki tunauza kwa njia ya mtandao licha ya bidhaa zetu kuwa nzuri sana. Serikali  ipunguze uingizwaji wa bidhaa ambazo tunazo wajasiriamali wa Tanzania na sisi tupate hata hili soko dogo la ndani,” amesema Ngambeki.

Elimu, elimu, elimu

Hali ya elimu ya Tanzania siyo jambo ambalo linaridhisha Watanzania wote akiwemo Mkazi wa Shinyanga, Monica Meshack ambaye amesema elimu inayofundishwa siyo kwa ajili ya Watanzania bali inawajenga wanafunzi kuwa tegemezi hata wakihitimu.

Mama huyo ameshauri ni muda Serikali kuwekeza katika elimu ya msingi kwa kukuza uwezo wa watoto kuwa wabunifu na kufundishwa kutatua changamoto za masuala ya kilimo, teknolojia, biashara na kuwa wabunifu tangu wakiwa wadogo.

“Wenzetu wa nje mtoto mdogo anatengeneza ‘project’ (mradi) wa maroboti sisi wetu anafundishwa aina za mawe tena akiwa darasani hatoki hata nje kuyaona hayo mawe,” amongeza Meshack akisema uwekezaji mkubwa ufanyike katika elimu ya masuala ya kilimo na teknolojia.

Mkazi mwingine wa Mwanza Maria Swayi amesema wanatamani kusikia kwenye bajeti hii wakiweka  fedha kwa ajili ya kujenga madarasa kwa wanafunzi wanaosoma  masomo ya sayansi ili kuwasaidia wanafunzi kuweza kujisomea vizuri  na kupata ufaulu mkubwa.

Ukiachana na masuala ya elimu, wengine wakiwemo wakazi wa jijini Mwanza wanatamani kuona bajeti ya mwaka 2021/22 inajibu mahitaji yote ya msingi ikiwemo dawa kwenye hospitali na maji.

Bajeti imalize uhaba wa dawa hospitalini

Mkazi wa Kisesa mkoani Mwanza,  Godfrey  Masanzu amesema bajeti hii ijikite kuongeza dawa katika hospital na zahanati kwa sasa kuna uhaba mkubwa wa dawa kwenye hospitali hizo.

“Lakini pia itenge fedha kwa ajili ya kujenga majengo ya huduma ya mama na mtoto ili kuwasaidia wanawake wajawazito kupata huduma bora, ” amesema Masanzu.

Wengine wanatarajia bajeti hiyo itakayosomwa leo Saa 10 jioni itaweka kipaumbele upatikanaji wa maji safi na salama hususani kwenye maeneo ya vijijini ili kumtua mama ndoo kichwani.

“Hatuna maji tunategemea ya visimani ambayo si safi na salama,  hivyo tungependa bajeti ijikite kwenye kupeleka maji kwenye maeneo yasiyokuwa na maji hususani Usagara ili kupunguza adha hiyo, ” amesema Martha Kunju mkazi wa eneo la Usagara mkoani Mwanza.

Baadhi ya wanaharakati wamesema ni vema Serikali ikaendelea kutekeleza miradi iliyokwisha kuanza ili kupeleka maendeleo kwa haraka.

Mwanaharakati wa Jijini Mwanza Frola Magabe ipo miradi mikubwa ya kimkakati  ikiwemo ujenzi wa kituo kikubwa cha kusambaza maji kinachojengwa kata ya Butimba,  ujenzi wa Soko kuu,  stendi za mabasi na ujenzi wa meli pamoja na reli ya kisasa inayopaswa kukamilishwa kwa wakati.

Amesema pia bajeti ijikite katika kumthamini mwanamke kwa kuongeza kiwango cha fedha kilichokuwa kinatolewa katika halmashauri nchini ili kifungue dirisha la kila mmoja kuchukua mkopo wenye riba nafuu.

Imeandikwa na Rodgers George (Dar es Salaam) na Mariam John (Mwanza)