Matokeo kidato cha nne haya hapa
Ufaulu waongezeka kidogo kwa asilimia 1.38 kutoka matokeo ya mwaka 2018 huku takriban nusu ya watahiniwa wote wakipata daraja la IV.
- Ufaulu waongezeka kidogo kwa asilimia 1.38 kutoka matokeo ya mwaka 2018
- Takriban nusu ama asilimia 48.6 ya watahiniwa wote wa mwaka 2019 wamepata daraja la nne.
- Watahiwa 19 kati ya 100 waliofanya mtihani huo wamepata sifuri.
Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya kidato cha nne mwaka 2019 huku ufaulu ukiongezeka kidogo kwa asilimia 1.4 kutoka ule wa mwaka 2018.
Licha ya ufaulu huo kuongezeka, bado takriban nusu ama asilimia 48.6 ya watahiniwa wote wa mwaka 2019 wamepata daraja la nne.
Necta imeeleza leo kuwa katika mtihani huo wanafunzi 340,914 wamefaulu mtihani kati ya wanafunzi 422,722 waliofanya mtihani huo Oktoba mwaka jana ikiwa ni sawa na asilimia 80.65 ya watahiniwa wote. Hii ni sawa na kusema kuwa wanafunzi 81 kati ya 100 waliofanya mtihani huo wamefaulu.
Ufaulu huo, kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde, ni sawa ongezeko la asilimia 1.38 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2018. Mwaka juzi asilimia 79.27 ya watahiniwa wa shule walifaulu mtihani huo.
Hata hivyo, ni wanafunzi 135,301 au takriban theluthi tu (asilimia 32) ya watahiniwa wote waliofanya mtihani huo wamefanikiwa kupata daraja la I hadi la III.
Kati ya wanafunzi hao waliopata ufaulu mzuri zaidi, wasichana ni 58,542 na wavulana ni 76,759.
“Hivyo ubora wa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.25 ikilinganishwa na mwaka 2018 ambapo watahiniwa waliopata ufaulu wa daraja la I hadi la III walikuwa 113,825 sawa na asilimia 31.76,” amesema Dk Msonde.
Kundi kubwa la wanafunzi hao limepata daraja la nne ambalo huwa ni vigumu kidogo kuchaguliwa moja kwa moja kwenda kidato cha nne. Wanafunzi 205,613 au sawa na asilimia 48.6 ya watahiniwa wote wa kidato cha nne mwaka jana wamepata daraja hilo la nne.
Hata wakati wakati wanafunzi 80 kati ya 100 waliofanya mtihani huo wakifaulu, wenzao 19 kati ya 100 wamefeli kabisa jambo linalowatoa katika nafasi ya kuendelea na masomo ya kidato cha nne. Wanafunzi 81,808 wenye daraja sifuri kwa kawaida huwa hawapati vyeti.