Matukio yaliyotikisa sekta ya utalii Tanzania 2019
Baadhi ya matukio hayo ni kuanzishwa kwa hifadhi mpya mbili za Taifa na zinazotozwa katika hifadhi za Taifa na sanamu ya hayati Mwalimu Julius Nyerere iliyozua mjadala mtandaoni.
- Baadhi ya matukio hayo ni kuanzishwa kwa hifadhi mpya mbili za Taifa na zinazotozwa katika hifadhi za Taifa.
- Sanamu ya hayati Mwalimu Julius Nyerere iliyozua mjadala mtandaoni.
Dar es Salaam. Sekta ya utalii ni miongoni mwa nguzo muhimu katika uchumi wa Tanzania kutokana na mchango wake mkubwa katika ukuaji wa pato la Taifa kila mwaka.
Watalii wa ndani na kutoka maeneo mbalimbali duniani wamekuwa wakitembelea vivutio vya utalii nchini na kulala katika hoteli za watalii ambazo pia ni miongoni mwa vyanzo vya mapato na ajira kwa Watanzania.
Wakati tunakaribia kumaliza mwaka 2019, tujikumbushe baadhi ya mambo ambayo yalitikisa sekta hiyo, kiasi cha kuibua gumzo na hata kuwa sehemu ya kuikuza sekta hiyo.
Baadhi ya mambo hayo ni kuanzishwa kwa hifadhi mpya mbili za Taifa na tozo zinazotozwa katika hifadhi za Taifa:
Hifadhi mbili za Taifa zaanzishwa
Tangu mwaka 2014 Tanzania imekuwa na hifadhi za Taifa 16 zenye ukubwa wa kilomita za mraba 57,024 zinazosimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa). Lakini, sasa ziko 18 baada ya hifadhi mbili kuanzishwa kwa nyakati tofauti mwaka huu.
Julai 4, 2019, Rais John Magufuli alizindua hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato iliyopo katika mikoa ya Geita na Kagera, iliyotangazwa rasmi kwenye gazeti la Serikali (GN # 508 la mwaka 2019). Hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilomita za mraba 4,707 ikiwa ni ya tatu kwa ukubwa nchini baada ya Ruaha (kilomita za mraba 20,300) na Serengeti (kilomita za mraba14,763).
Awali hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato ilikua Pori la Akiba lililojulikana kwa jina la Burigi kabla ya kupandishwa hadhi.
Uwepo wa hifadhi hiyo ni muendelezo wa jitihada za Serikali kufungua fursa za utalii katika mikoa ya kanda ya ziwa yenye miundombinu kama reli ya kati na uwanja wa ndege wa Chato ambao utasaidia kuongeza idadi ya watalii.
Magufuli alikabidhiwa sanamu ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla yenye ujumbe maalum kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira ya wanyama pori.Lakini ilizua maswali mengi kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii. Picha|Mtandao.
Baada ya Burigi-Chato, Novemba 19, Wizara ya Maliasili na Utalii, ilitangaza kuanzishwa rasmi kwa hifadhi ya Taifa ya Nyerere yenye ukubwa wa kilomita za mraba 30,893 na kuifanya kuwa miongoni mwa hifadhi kubwa zaidi duniani na yenye vivutio vingi vya utalii wakiwemo wanyamapori.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Rais Magufuli kuagiza Pori la Akiba la Selous lililopo karibu na mto Rufiji utakatokelezwa mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa maji wa megawati 2,115, likatwe ili sehemu moja ya pori hilo iwe hifadhi.
Novemba 9, Bunge la Tanzania lilipitisha azimio la Bunge la kuanzisha Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ambapo Novemba 19, Rais akaweka sahihi kwenye tangazo la kuanzisha hifadhi hiyo.
Hata hivyo, Serikali imekamilisha mchakato wa kuanzisha hifadhi zingine mbili za Kigosi na Mto Ugalla.
Sanamu ya Mwalimu Nyerere yawa gumzo
Wakati wa uzinduzi wa hifadhi hiyo ya Burigi-Chato, Rais Magufuli alikabidhiwa sanamu ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla yenye ujumbe maalum kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira ya wanyama pori.
Hata hivyo, muonekano wa sanamu hiyo ulizua mijadala tofauti tofauti kwenye mitandao ya kijamii,l huku wengi wakionekana kushangazwa na muonekano wake wakidai kuwa hauendani hata kidogo na sura ya Mwalimu Nyerere.
Siku chache baadaye, Dk Kigwangalla alijitokeza na kuomba apewe muda ili kurekebesha mfano wa sanamu ambalo lilichongwa kuashiria kuwa ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Waziri Kigwangalla alisema kuwa “Baba wa Taifa alitoa tamko la kwanza la Uhifadhi nchini, ambalo ndiyo dira yetu, tuache dhihaka kwa sababu hakuna aliyefanya kazi ile kwa kusudi hilo, tumesema linashughulikiwa tunaomba mtuamini, mtupe muda turekebishe.”
“Kilichonifurahisha ni kuwa kizazi cha vijana wa kisasa, bado kinamkumbuka vizuri Baba wa Taifa, kinamuenzi na kumheshimu sana, ndiyo maana wanaikumbuka taswira yake, tutatumia vizuri zaidi wataalamu wetu kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza kabla ya kuitumia,” alisema Waziri Kigwangalla.
Licha ya ahadi hiyo, mpaka sasa Serikali haijazungumza lolote kuhusiana na hatua zilizochukuliwa kuondoa utata wa sanamu hilo.
Zinazohusiana:
- Serikali kuwabana wanaopangisha nyumba kwa watalii bila leseni.
- Tamasha la Urithi Festival kufanyika mikoani kila mwaka.
- Tanzania yaangazi masoko 18 kukuza utalii duniani
Kuanza kwa ukanda wa fukwe
Januari 27, Serikali alitangaza kuanza mchakato wa kuanzisha ukanda maalum wa utalii wa fukwe kutoka Bagamoyo hadi Tanga unakusudia kufungua fursa mbalimbali za shughuli za utalii.
Utalii huo pia utahusisha fukwe ya Ziwa Victoria katika eneo la Chato ambapo inapatikana Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato na eneo la Kilwa mkoani Mtwara.
Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla, fukwe zilizopo maeneo mbalimbali nchini hasa pwani ya bahari ya Hindi hazijatumika ipasavyo kutoa fursa kwa wananchi na Serikali kufaidika na rasilimali hiyo.
Serikali ilisema fukwe hizo zitaboreshwa kwa kutengeneza maeneo ya kupumzika, kuboresha usafiri wa boti na huduma za uongozaji watalii kulingana na jiografia ya nchi.
Sambamba na hilo ni kuwa na gati la boti za kitalii na barabara kubwa zitakazounganishwa na fukwe hizo ili kuondoa changamoto ya usafiri ambayo imekuwa ikiathiri shughuli za utalii hasa wakati wa masika.
Ripoti ya utafiti wa wageni wa nje ya nchi mwaka 2017 (International Visitors’ Exit Survey Report 2017) inaonyesha kuwa hifadhi za Taifa na fukwe ndiyo zinaongoza kutembelewa zaidi na watalii, jambo linalotoa fursa kwa Serikali kufaidika na mapato yake.
Fukwe ni miongoni mwa vivutio vya watalii ambao hupenda kukaa katika mwambao wa bahari na maziwa. Picha|Mtandao.
Serikali yatangaza tozo mpya kuingia mbugani
Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) ilitangaza tozo mbalimbali zinazotozwa kwenye hifadhi inazosimamia nchini kwa wageni wa ndani na nje ya nchi.
Tozo hizo ni za kipindi cha mwaka mmoja na tayari zimeanza kufanya kazi tangu Julai 1, 2019 na mwisho wake utakuwa Juni 30, 2020.
Tozo hizo ambazo zinahusu wageni na wakazi, nyingi zinaonekana kuwa na utofauti wa takribani asilimia 50 kati ya ile ya mgeni na mkazi ambapo tozo ya mgeni ni mara mbili ya ile ya mkazi/ Mtanzania.
Mathalan, kwa mgeni aliye juu ya miaka 15 anayetaka kuingia hifadhi ya Taifa ya Serengeti itabidi agharamie Sh138,198 huku yule aliye na miaka chini ya 15 akitakiwa kugharamia Sh46,066 tu.
Kwa Watanzania, wakazi wa nchi za Afrika Mashariki na wataalamu, pochi zao inabidi zitoe Sh69,099 kwa wote wenye miaka zaidi ya 15 na kwa wale wenye miaka mitano hadi 15 watatakiwa kulipa Sh23,033 kwa kila mtu.
Masharti mapya kwa wanaorusha ndege zisizo na rubani mbugani
Agosti 26, Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) lilitoa mwongozo na taratibu zinazotakiwa kuzingatiwa kwa watu wanaorusha ndege zisizo na rubani (Drones) katika maeneo ya hifadhi za Taifa kwa shughuli mbalimbali katika maeneo hayo.
Katika mwongozo uliotolewa na mamlaka hiyo, unaeleza kuwa mtu yeyote hataruhusiwa kurusha ndege hiyo kwenye hifadhi mpaka apate kibali kutoka kwenye mamlaka zinazotambuliwa kisheria.
Mwombaji anatakiwa apate vibali vinne kutoka Bodi ya Filamu Tanzania, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi, Mamlaka ya usafiri wa anga Tanzania (TCAA) pamoja na kibali cha Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa.
Hata baada ya kupata vibali hivyo, mhusika anatakiwa kwenda mbali zaidi na kufanya maombi rasmi kwa Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa akiwa ameambatanisha nakala za vibali kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi, Bodi ya Filamu Tanzania na TCAA.
Ni mambo gani yataibuka mwaka 2020 katika sekta hii muhimu?