November 24, 2024

Matumizi sahihi ya chanjo za dharura za Corona

Kila chanjo iliyoidhinishwa kwa matumizi ya dharura ina masharti yake hasa katika uhifadhi na utumiaji ili iweze kuwa na ufanisi.

  • Mpaka sasa chanjo sita zimeidhinishwa na WHO kama chanjo za dharura.
  • Usafirishaji, uhifadhi na muda wa utumiaji wa chanjo hizo hutofautiana.
  • Nchi zinazopokea chanjo hizo zatakiwa kuzingatia mwongozo wa matumizi yake. 

Mwanza. Ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa COVID-19, Shirika la Afya Duniani (WHO) mpaka sasa limeidhinisha aina 6 za  chanjo kwa ajili ya matumizi ya dharura.

Chanjo hizo ni Pfizer/BioNTech, AstraZeneca/Oxford, Moderna, Johnson & Johnson, Sinovac na Sinopharm. Chanjo hizo ni miongoni mwa chanjo zaidi ya 200 ambazo ziko kwenye utafiti ili kukabili Corona.

Hata hivyo, kila chanjo iliyoidhinishwa kwa matumizi ya dharura ina masharti yake hasa katika uhifadhi na utumiaji ili iweze kuwa na ufanisi. 

Kwa mujibu wa mwongozo wa WHO wa utoaji wa chanjo, Pfizer/BioNTech inahitaji ubaridi wa nyuzi joto hasi 70 katika kipimo cha selsiyasi (-70℃). Lazima chanjo hiyo iwe imeganda, na iwapo itayeyuka na kuganda tena basi ufanisi wake  unapungua.

Kiwango hicho cha ubaridi cha uhifadhi ni changamoto kwa nchi nyingi za kipato cha chini na kati ambazo hazina miundombinu ya majokofu ya kuhifadhi na kusambaza chanjo.

AstraZeneca inahitaji ubaridi wa kati ya nyuzi joto 2 hadi 8 katika kipimo cha selsiyasi ( +2 °C hadi 8 °C,) kiwango ambacho ni sawa na chanjo za kawaida ambazo hutolewa katika nchi za kipato cha chini na kati. 

Na chanjo hizi hazihitajiki kuwa zimeganda barafu wakati anapatiwa mhusika.

Majokofu yenye baridi kali yanayotumiwa na Rwanda kuhifadhi chanjo ya COVID-19 aina ya Pfizer/BioNTech katika kituo cha serikali cha kuhifadhi chanjo kilichoko mjini Kigali. Rwanda ni miongoni mwa nchi zilizopokea chanjo ya Pfizer/BioNTech kupitia mpango wa Umoja wa Mataifa wa COVAX. Picha| UNICEF/Andy Rugema.

WHO katika mwongozo huo inaeleza kuwa Pfizer na Moderna zinazotumia teknolojia ya kuchochea seli ya mwili kuzalisha protini ili kuongeza kinga ya mwili dhidi ya virusi na hivyo zikipata joto au baridi kupitiliza zinaharibika. 

“Chanjo iliyoharibika lazima itupwe na WHO haitaki hata dozi moja ya chanjo itupwe. Hivyo lazima nchi kuzingatia mifumo na masharti ya uhifadhi wa kila chanjo, imesema taarifa ya redio ya Umoja wa Mataifa kuhusu mwongozo huo.

Chanjo zaidi zinaendelea kutengenezwa na zinafanyiwa utafiti kabla ya kuidhinishwa na WHO. Miongoni mwao ya Sputnik V kutoka Urusi. RDIF/Stas Zalesov-Nakashidze

Chanjo zaidi zinaendelea kutengenezwa na zinafanyiwa utafiti kabla ya kuidhinishwa na WHO. Miongoni mwao ni hii ya Sputnik V kutoka Urusi.

 

Utunzaji na matumizi

Kwa chanjo ya Pfizer, iwapo haijachanganywa na imehifadhiwa katika nyuzi joto hasi 90 hadi hasi 60 (-90 °C hadi -60 °C) inaweza kutunzwa kwa miezi 6 tangu itengenezwe. 

Ikiwa kwenye nyuzi joto 2 hadi 8 inaweza kutumika ndani ya siku 5 tu, na joto likipanda zaidi na kuwa nyuzi joto 30 inapaswa iwe imetumika ndani ya saa 2. Na iwapo itachanganywa na iko katika nyuzi joto 2 hadi 30 basi lazima itumike ndani ya saa 6.

Kwa upande wa AstraZeneca kichupa cha chanjo ambacho hakijafunguliwa na kimehifadhiwa katika nyuzi joto kati ya 2 hadi 8 (2 °C hadi 8 °C ) kinaweza kutumika hadi miezi 6. Kile ambacho kimeshafunguliwa lakini kiko katika ubaridi wa kati ya nyuzi joto 2 hadi 25 katika kipimo cha selsiyasi (2 °C hadi 25 °) kinaweza kutumika ndani ya saa 6 tu.

Chanjo ya AstraZeneca/Oxford dhidi ya COVID-19 inatengenezwa nchini India chini ya leseni maalum. Picha| UNICEF/Dhiraj Singh

Kwa nini chanjo hizo zimeorodheshwa kwa matumizi ya dharura?

WHO inasema ni kwa kuzingatia mazingira ya janga la Corona, chanjo zinaweza zisiwe zimekidhi vigezo vya awali vya kuidhinishwa moja kwa moja.

Jopo la wataalam linazipitia na kuidhinisha ziwe kwenye orodha ya matumizi ya dharura ili kuchagiza mchakato wa upatikanaji wake na matumizi ya dawa ambazo bado hazijapatiwa leseni lakini zinahitajika katika dharura ya kitabibu ili kulinda afya ya umma.

Shirika hilo linasisitiza kuwa nchi lazima ziwe na mkakati wa kitaifa wa utoaji wa chanjo na wakati huo huo mkakati huo ujumuishe uimarishaji wa mnyororo wa kupokea, kuhifadhi na kusambaza chanjo hizo.

Pia usimamizi wake na vifaa vinavyotakiwa kama mabomba ya sindano, majokofu na makasha ya kutupia sindano zilizotumika upangiliwe vizuri. Usambazaji huo ufikie hadi maeneo ya ndani kabisa ya nchi ili kila mtu anayehitaji kupata chanjo apatiwe.