October 6, 2024

Matumizi sahihi ya choo cha kukaa kukulinda dhidi ya UTI

Hakikisha unaflashi choo, funika kwa karatasi na kusafisha eneo la kukaa kwa dawa ya kuua bakteria.

  • Hakikisha unaflashi choo, funika kwa karatasi na kusafisha eneo la kukaa kwa dawa ya kuua bakteria.
  • Kwa wanawake wanashauriwa kutumia kifaa maalum cha kukojolea ili kuzuia maji maji kuingia sehemu za siri.
  • Nawa vizuri mikono yako kwa sabani baada ya kumaliza haja.

Ni dhahiri kuwa uwepo wa huduma ya choo katika maeneo yenye mkusanyiko wa watu ni jambo lisilo na mjadala kwa sababu hutumika kujisitiri na kulinda afya za watu wa eneo husika. 

Kwa wanaotembelea katika majengo mbalimbali hasa maeneo ya mjini, lazima utakutana na vyoo vya kisasa vya kukaa vilivyotengenezwa kwa ubunifu tofauti wa teknolojia na malighafi mbalimbali ili kumpa mtumiaji starehe na uhuru wakati ukimaliza haja zake. 

Lakini upande wa pili vyoo hivyo hivyo vimekuwa ni sehemu ya maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo kibofu cha mkojo maarufu kama UTI (Urinary Tract  Infection).

Huenda wewe ni umekuwa ukipatwa na UTI mara kwa mara licha ya kutibiwa lakini hujui kiini chake nini? Basi vyoo vya kukaa vinachangia kwa sehemu kubwa kusambaza ugonjwa huo kutoka mtu mmoja hadi mwingine. 

Nukta inakuletea suluhisho au hatua muhimu unazopaswa kuchukua wakati ukitumia vyoo vya kukaa ili kuepuka maambukizi ya UTI:

Funua mfuniko wa choo kwa kutumia karatasi laini

Kutokana na vyoo hivyo kutumika na watu wengi, ni vema kufunua mfuniko wa choo kwa kutumia karatasi laini (Tissue) ili kuzuia bakteria waliopo sehemu ya kukalia kupenya kwenye mikono yako. Hii ni hatua muhimu kukinga na UTI.

Matumizi sahihi ya choo cha kukaa yanaweza kukusaidia kujikinga dhidi ya maambuki ya njia ya mkojo. Picha|Daniel Samson.

Safisha eneo la kukaa

Kabla hujaanza kutumia choo, ni vema usafishe eneo la kukaa kwa karatasi laini iliyolowekwa kwa dawa au sabuni ya maji ya kuua wadudu (Toilet seat sanitizer). Hii itakusaidia kuua bakteria walioachwa na watu wengine wakati wakitumia choo. 

Flashi kwa maji

Bakteria hawapatikani tu kwenye eneo la kukalia tu, hata kwenye maji maji yanayobaki baada ya kutumia choo. Ni kuflashi choo kabla hujatumia ili hata maji maji yakigusana na sehemu za siri hutapunguza  maambukizi mwilini. 

Katika maeneo mengi, maji ya kuflashi yanakuwa yamewekewa dawa ya kuua wadudu.


Soma zaidi: Watafiti watofautiana matumizi vifaa vya kukaushia mikono


Funika eneo la kukaa kwa kitambaa au karatasi laini

Karatasi hizo zinajulikana kama ‘Toilet seat cover’. Hii ni njia nyingine ya kuzuia bakteria kuingia mwilini kupitia njia ya mkojo. Hutumika kama huna dawa ya kusafisha eneo la kukaa au vyote kwa pamoja ili kujihakikishia ulinzi zaidi. 

Baada ya kukamilisha hatua hizo, sasa kaa na maliza haja yako vizuri huku ukijiamini. Ukikamilisha mchakato wote basi nawa mikono yako kwa maji safi na sabuni ili kuondoa harufu na bakteria. 

Muonekano wa vitambaa vinavyotumika kufunika eneo la kukaa ili kukupa starehehe lakini kukinga na maambukizi. Picha|Mtandao.

Hata hivyo, ipo njia nyingine ya kuvaa kifaa maalum cha kutolea haja ndogo (waterproof funnel-urinary device) ambapo kinawafaa zaidi wanawake kwa kuwawezesha kukojoa wakiwa wamesimama. 

Kimetengenezwa maalum kuwakinga na maji maji ambayo yanaweza kuwa na vimelea vya magonjwa yasiwafikie sehemu za siri. 

Kumbuka hizi ni hatua za awali unazoweza kuzitumia kujikinga na UTI lakini kinachotakiwa zaidi ni kuhakikisha vyoo vinakuwa visafi wakati wote. 

Wataalam wa afya wanashauri kunywa maji mengi, hakikisha unakojoa kila unapojisikia kukojoa, hakikisha sehemu za siri zipo kavu na pendelea kuvaa nguo za ndani zilizotengenezwa kwa pamba, pia zenye kuacha unafasi (loose-fitting). 

Hatari iliyopo ya kukaa na UTI kwa muda mrefu inaweza kukuletea matatizo ya kibofu cha mkojo na hata matatizo ya figo.