July 5, 2024

Maumivu waliowekeza Vodacom soko la hisa Dar

Thamani ya hisa za kampuni hiyo zimeshuka kwa asilimia 4.71 kutoka kiwango cha Ijumaa Septemba 18, 2020.

  • Thamani ya hisa za kampuni hiyo zimeshuka kwa asilimia 4.71 kutoka kiwango cha Ijumaa Septemba 18, 2020.
  • Wawekezaji wake wamepoteza Sh40 kwa kila hisa moja.
  • Hata hivyo, Vodacom yaongoza kwa mauzo ya hisa katika soko hilo. 

Dar es Salaam. Wawekezaji wa kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) leo watalala na maumivu baada ya thamani ya hisa za kampuni hiyo kushuka na kuwafanya wapoteze Sh40 kwa kila hisa moja kutoka kiwango cha Ijumaa Septemba 18, 2020.

Ripoti ya soko ya siku ya DSE ya Septemba 21 inaonyesha kuwa hadi soko linafungwa leo jioni, thamani ya hisa moja ya Vodacom ilikuwa ni Sh810 kutoka Sh850 iliyorekodiwa Ijumaa.

Hiyo ni sawa kusema thamani ya hisa za Vodacom zimeshuka kwa asilimia 4.71 na kuwafanya wawekezaji wa kampuni hiyo kupoteza Sh40 kwa kila hisa moja iliyouzwa leo sokoni. 

Wakati wawekezaji wa Vodacom wakiugulia maumivu, wenzao wa benki ya KCB watalala na kicheko baada ya thamani ya hisa za benki hiyo kupanda kwa asilimia 1.25 kutoka Sh800 iliyorekodiwa Ijumaa hadi Sh810  iliyotumika leo.  


Zinazohusiana: 


Kampuni nyingine ambazo thamani ya hisa zake imeongezeka ni kampuni ya Habari ya NMG (National Media Group) ambayo imepanda kwa asilimia 13.85 na Jubilee Holding Limited kwa asilimia 1.30.

Vodacom ndiyo kampuni iliyofanya vibaya zaidi leo sokoni huku nyingi zikibaki katika viwango vilivyokuwepo Ijumaa zikiwemo Acacia, benki ya CRDB, DCB na NMB.

Licha ya thamani ya hisa za Vodacom kushuka, ndiyo kampuni iliyoongozwa kwa kuuza hisa nyingi sokoni leo. Vodacom imeuza hisa 380,730 sawa na asilimia 40.9 ya hisa zote zilizouzwa.