October 6, 2024

Mauzo soko la hisa Dar yashuka

Yameshuka kwa zaidi ya mara 21 kutoka Sh7.5 bilioni wiki iliyoishia Agosti 16 hadi Sh351.7 milioni Ijumaa ya Agosti 23, 2019.

  • Yameshuka kwa zaidi ya mara 21 kutoka Sh7.5 bilioni wiki iliyoishia Agosti 16 hadi Sh351.7 milioni Ijumaa ya Agosti 23, 2019. 
  • Sababu kubwa ikiwa ni kushuka kwa shughuli za mauzo za soko hilo. 
  • Pia mtaji wa soko hilo nao umeshuka kidogo hadi Sh19.11 trilioni kutoka Sh19.15 trilioni iliyorekodiwa katika wiki iliyoishia Agosti 16. 
  • Benki ya CRDB yaongoza kwa mauzo ya asilimia 85.23. 

Dar es Salaam. Thamani ya mauzo ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE)  yameshuka kwa zaidi ya mara 21 ndani ya kipindi cha wiki moja, huku sababu kubwa ikielezwa na wataalamu kuwa ni kushuka kwa shughuli za mauzo za soko hilo. 

Takwimu za DSE, zilizotolewa na kampuni ya udalali wa dhamana na mitaji na ushauri wa kiuwekezaji ya Zan Securities, zinaonyesha kuwa wiki inayoishia Ijumaa ya Agosti 23, 2019  thamani ya mauzo ilikuwa Sh351.7 milioni ambapo yameshuka kutoka Sh7.5 bilioni katika wiki iliyoishia Agosti 16 mwaka huu. 

Anguko hilo la thamani ya mauzo ni sawa na asilimia 95.3 au zaidi ya mara 21 katika kipindi cha wiki moja. 

Kabla ya kushuka kwa kasi kwa thamani hiyo, soko hilo lilionyesha mwenendo mzuri katika wiki iliyoishia Agosti 16 kwa sababu mauzo yaliongezeka kwa asilimia 884.3 ukilinganishwa na wiki iliyoishia Agosti 9 ambapo yalikuwa Sh761.7 milioni.

Wakati thamani ya mauzo ya DSE yakishuka katika wiki inayoishia Agosti 23, pia mtaji wa soko hilo nao umeporomoka kidogo hadi Sh19.11 trilioni kutoka Sh19.15 trilioni iliyorekodiwa katika wiki iliyoishia Agosti 16. 


Zinazohusiana: 


Kwa mujibu wa kampuni ya Zan Securities yenye makao yake makuu, Upanga jijini Dar es Salaam., kushuka kwa thamani ya mauzo na mtaji wa DSE kunatokana na kupungua shughuli za soko hilo.

“Hata hivyo, tunatarajia kuongezeka kwa shughuli za soko hilo siku zijazo,” amesema Afisa Mtendaji Mkuu wa Zan Securities, Raphael Masumbuko katika uchambuzi wa wiki wa DSE.

Kwa mujibu wa Masumbuko, kurejea kwa shughuli siku zijazo kutaongeza mauzo na mtaji wa DSE.

Licha ya kushuka kwa thamani ya mauzo, benki ya CRDB ndiyo iliyofanya vizuri zaidi katika soko hilo wiki hii ambapo mauzo yake yalikuwa asilimia 85.23 ya mauzo yote ya DSE ikifuatiwa na kampuni ya TPCC (asilimia 12.86).