November 24, 2024

Mavazi ya wanawake yachangia kupaisha mfumuko wa bei Tanzania

Umepanda hadi kufikia asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2021 kutoka asilimia 3.3 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2021.

  • Umepanda hadi kufikia asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2021 kutoka asilimia 3.3 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2021.
  • Umechangiwa na kuongezeka kwa bei ya baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula vikiwemo vitambaa vya nguo na mavazi ya wanawake.

Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini imepanda hadi kufikia asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2021 kutoka asilimia 3.3 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2021.

Kasi hiyo imechangiwa na kuongezeka kwa bei ya baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula vikiwemo vitambaa vya nguo na mavazi ya wanawake.

Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyotolewa Julai 8, 2021, bei ya vitambaa vya nguo imepanda kwa asilimia 8.5, nguo za wanawake (asilimia 6.3), viatu vya wanaume kwa asilimia 6.2. 

Kodi ya pango kwa asilimia 4.9, vyakula kwenye migahawa (asilimia 5.6) na gharama za malazi kwenye nyumba za kulala wageni zimepanda kwa asilimia 5.7..

Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2021 umepungua hadi asilimia 4.7 kutoka kwa asilimia 4.9 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2021.

Hali ya mfumuko wa bei Afrika Mashariki

Nchini Kenya, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2021 umeongezeka hadi asilimia 6.4 kutoka asilimia 5.8 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2021. 

Kwa upande wa Uganda, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2021 umeongezeka pia hadi asilimia 2 kutoka asilimia 1.9 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2021.