November 24, 2024

Mawasiliano yarejeshwa Hifadhi ya Ziwa Manyara

Maji yasomba Daraja la Merera lililopo kilomita moja kutoka kwenye lango la kuingilia katika hifadhi hiyo.

  • Maji yasomba Daraja la Merera lililopo kilomita moja kutoka kwenye lango la kuingilia katika hifadhi hiyo.
  • Tanapa yawataka watalii waliokuwa wanaelekea hifadhiniwaaihirishe kwa muda safari zao wakati wanatafuta suluhu.
  • Manyara ni miongoni mwa hifadhi za Taifa 11 kubwa nchini kati ya 16 zilizopo.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) imefanikiwa kurudisha mawasilino ya kuingia na kutoka katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara baada ya maji ya mvua zinazoendelea kunyesha kulisomba daraja la Merera.

Meneja Mawasiliano wa Tanapa, Pascal Shelutete ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa shughuli za utalii zinazohusisha kuingia katika hifadhi hiyo zinaweza kuendelea kama kawaida.

Mapema leo asubuhi Aprili 17, 2018 Tanapa iliwatangazia watalii waliokuwa wanaelekea katika hifadhi hiyo kuahirisha kwa muda safari zao hadi tatizo litakapotatuliwa.      

Mvua zinazondelea kunyesha katika maeneo mbalimbali zimesababisha uharibifu wa miundombinu na kusababisha vivutio vya utalii vilivyopo katika eneo hilo kutofikika kwa urahisi.

“Miundombinu ya kuwezesha watalii kufika  hifadhi ya Ziwa Manyara imeharibika kutokana na daraja  la Merera lilipo takribani kilomita moja kutoka lango la kuingilia mbugani hapo kusombwa na  maji,” inasomeka sehemu ya taarifa iliyokuwa imetolewa awali na Meneja Mawasiliano wa Tanapa, Pascal Shelutete. 

Manyara ni hifadhi ya 11 kwa ukubwa Tanzania kati ya hifadhi 16  zilizopo, ikiwa na kilomita za mraba zipatazo  648 ikijumuisha  maeneo ya Babati na Mbulu mkoani Manyara na Karatu na Monduli mkoani Arusha.

             

Shelutete amesema juhudi za kurudisha miundombinu hiyo katika hali ya kawaida  zinaendelea na kubainisha kuwa umma utajulishwa maendeleo ya jitihada husika.

Utalii ni moja ya sekta kubwa mbili nchini pamoja na dhahabu zinazoongoza kwa kuingiza fedha za kigeni ikiwa ni mwenendo chanya wa ukuaji mwaka hadi mwaka. 

Ripoti ya utafiti wa watalii wa kimataifa ya mwaka 2016 (Tanzania Tourism Sector Survey: The International Visitors’ exit Survey Report 2016) iliyotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kuwa mwaka 2016 sekta hiyo ilifikisha watalii milioni 1.28 ikiwa ni ukuaji wa asilimia 12.9 kutoka ule wa mwaka 2015. Mwaka huo mapato yalitokana na utalii yalifikia Dola za Marekani bilioni 2.13 (Sh4.7 trilioni).