November 24, 2024

Maxence Melo wa JamiiForums atoka baada ya kulipa faini ya Sh3 milioni

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imemhukumu mwanzilishi wa mtandao wa JamiiForums Maxence Melo kulipa faini ya Sh3 milioni au kwenda jela mwaka mmoja baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kuzuia polisi kufanya upelelezi wao.

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imemhukumu mwanzilishi wa mtandao wa JamiiForums Maxence Melo kulipa faini ya Sh3 milioni au kwenda jela mwaka mmoja.
  • Imemtia hatiani kwa kosa la kuzuia polisi kufanya upelelezi wao.
  • Amelipa faini ya Sh3 milioni na anakusudia kukata rufaa kupinga uamuzi huo. 

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imemhukumu mwanzilishi wa mtandao wa JamiiForums Maxence Melo kulipa faini ya Sh3 milioni au kwenda jela mwaka mmoja baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kuzuia polisi kufanya upelelezi wao.

Mahakama hiyo pia, imemuachia huru Micke Mushi baada ya ushahidi kushindwa kuthibitisha kuwa alikuwa ni mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi wa Jamii Media inayoendesha Jamii Forums.

“Upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka bila kuacha shaka. Mahakama inamtia hatiani mshtakiwa wa kwanza (Maxence Melo),” Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema mahakamani hapo.

Baada ya kuzingatia hoja zote za mawakili wa utetezi na Serikali zikiwemo kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, Simba amemhukumu Melo kulipa faini ya Sh3 milioni au kifungo cha mwaka mmoja iwapo atashindwa kulipa faini hiyo.


Soma zaidi: 


Baada ya kulipa faini hiyo na kuachiwa, Melo amewaambia wanahabari kuwa hukumu kama hiyo zinatilia shaka hatma ya wanahabari nchini na zaidi uhuru wa wananchi kujieleza.

“Hii ni kwa sababu posts (chapisho) zilihusu masuala ya kifisadi yanayohusu kampuni binafsi lakini dola imeonekana kutumia nguvu kupata taarifa kitendo kinachozidi kuwaminya na kuwaogopesha watoa taarifa. Ila niwatie moyo waandishi wa habari courageous (wanaojitoa) na watoa taarifa wasikate tamaa ya kufanya kazi yao,” amesema Melo.

Amesema hawajaridhishwa na uamuzi wa mahakama hiyo na kwamba wataenda kukata rufaa.

Melo alishtakiwa Desemba 2016 kwa kuzuia polisi kufanya uchunguzi wao kwa kutotoa ushirikiano wa kutoa taarifa za moja ya watumiaji wa mtandao  wa Jamii Forums ambaye alikuwa amechapisha tuhuma za rushwa dhidi ya kampuni binafsi ya mafuta. 

Mmoja wa Wakuregenzi na Mwanzilishi wa JamiiForums William Mushi aliongezwa katika kesi hiyo mapema mwaka 2017.