October 6, 2024

Mazao matano ya biashara yaliyoiingizia Tanzania fedha nyingi za kigeni 2018

Mazao hayo ni tumbaku, kahawa, chai, korosho na pamba.

  • Mazao hayo ni tumbaku, kahawa, chai, korosho na pamba.
  • Mauzo ya korosho nje ya nchi  katika kipindi hicho yalishuka kwa asilimia 62.9. 

Dar es Salaam. Tanzania imekuwaa ikifanya biashara na nchi mbalimbali duniani hasa katika usafirishaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo mazao ya biashara ambayo yamekuwa yakiingizia Taifa fedha za kigeni. 

Unayafahamu mazao matano ya biashara yaliyoiingizia Tanzania fedha nyingi za kigeni mwaka 2018? 

Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018 kilichotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), tumbaku, kahawa, chai, korosho na pamba ndiyo mazao yaliyoingiza fedha nyingi za kigeni.  

1. Tumbaku

Tumbaku inalimwa katika mikoa ya Ruvuma, Tabora, Mbeya, Morogoro na Iringa ambapo kwa Mwaka 2018, thamani ya mauzo ya tumbaku nje ya  nchi iliongezeka kufikia dola za Marekani milioni 270.3 (Sh621.6 bilioni) ikilinganishwa na dola milioni 195.8 (Sh450.3 bilioni)  mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 38.0.

Kitabu hicho kinaeleza kuwa ongezeko hilo limetokana na idadi ya tani zilizouzwa nje kutoka tani 48,300 kwa mwaka 2017 mpaka tani 72.200 kwa mwaka jana.

Kwa mauzo hayo, tumbaku linakuwa zao la biashara lililoongoza kuingiza fedha nyingi za kigeni mwaka jana. 

2. Korosho

Korosho inalozalishwa katika mikoa kama Mtwara, Lindi, Pwani, Tanga na Ruvuma imeshika nafasi ya pili kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni. 

Mwaka jana, thamani ya mauzo ya korosho nje ilikuwa dola za Marekani milioni 196.5 (Sh 451.8 bilioni)  ikilinganishwa na dola milioni 529.6 (Sh1.2 trilioni) mwaka 2017  sawa na upungufu wa asilimia 62.9 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Kitabu hicho kinaeleza kuwa sababu kubwa ya kushuka kwa mauzo ya korosho nje ya nchi ni kupungua kwa korosho zilizouzwa nje kwa asilimia 63.5 kutoka tani 329,400 mwaka 2017 mpaka tani 120,200 kwa mwaka jana.

Pia sakata la bei ya korosho kwa wakulima nalo lilichangia ambapo mwaka jana Serikali iliwazuia wanunuzi binafsi kuchukua korosho ya wakulima kwa sababu ya bei ndogo waliyokua wananunua.


Zinazohusiana:



3. Kahawa

Thamani ya mauzo ya kahawa nje ya nchini kwa mwaka 2018 iliongezeka mpaka kufikia dola za Marekani milioni 147.9 (Sh340.1 bilioni) kutoka dola milioni 126.3 (Sh 290.4 bilioni) kwa mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 17.1. 

Mauzo hayo yalitokana na kuongezeka kwa usafirishaji wa zao hilo nje ya nchi ambapo mwaka jana ziliuzwa tani 56,600 ikilinganishwa na tani 41,800 za 2017.

Kahawa imekuwa ni tegemeo kwa wananchi wa mikoa ya Kagera, Ruvuma, Mbeya, Kilimanjaro, Kigoma, Arusha na Mara ili kujiingizia kipato kwa ajili ya kuendeleza maisha. 

4. Pamba.

NBS inaeleza kuwa  pamba iliyouzwa nje ya nchi kwa mwaka 2018 ilikuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 68.4 (Sh 157.3 bilioni) ikilinganishwa na dola milioni 36.8 (Sh 84.6 bilioni kwa mwaka 2017.

Ongezeko hilo ni sawa asilimia 85.9 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, ambapo lilichangiwa zaidi na kuongezeka kwa uzalishaji na kiasi kilichosafirishwa nje ya nchi.

“Kuongezeka kwa bidhaa hiyo kwa mwaka jana ilitokana na kuongezeka kwa kiasi cha pamba kilichouzwa nje kutoka tani 25,300 mwaka 2017 hadi tani 47,400 kwa mwaka jana mwaka 2018,” inaeleza sehemu ya kitabu hicho kinachotolewa kila mwaka. 

Mauzo hayo yamekuwa yakiwafaidisha wakulima wa mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mwanza na Singida ambako zao hilo linalimwa sana. 

5. Chai

Tofauti na kahawa na pamba, mauzo ya chai nje ya nchi kwa mwaka jana yalishuka kwa asilimia 6.5 na kuifanya nchi ipoteze dola za Marekani milioni 3.2.

Thamani ya mauzo nje ya zao hilo mwaka jana ilikuwa dola za Marekani milioni 45.9 (Sh 105.5 bilioni) ikilinganishwa na dola milioni 49.1 (Sh 112.9 bilioni) mwaka 2017.

“Upungufu huo ulitokana na kushuka kwa bei ya chai katika soko la dunia kwa asilimia 4.5 kutoka dola za marekani 1,783.6 kwa tani mwaka 2017 mpaka dola 1,707.4 kwa tani mwaka jana 2018,” kinaeleza kitabu hicho.

Huenda kushuka kwa mauzo ya chai kuliwaathiri kwa sehemu wakulima wa zao hilo linalolimwa zaidi katika mikoa ya Mbeya, Arusha, Tanga, Iringa na Njombe.