Mazao yatakayosaidia kutokomeza migogoro ya tembo na wakulima
Serikali imewataka wananchi wanaoishi karibu na mbuga za wanyama kutumia njia mbadala kuzuia tembo kuvamia mashamba na makazi yao kwa kuepuka kulima mazao yanayovutia wanyama hao zikiwemo ndizi.
- Wakulima watakiwa kuacha kulima mazao yanayovutia tembo karibu na mbuga za wanyama.
- Njia nyingine za kudhibiti wanyama hao ni kutumia oili chafu, pilipili na kufuga nyuki karibu na hifadhi.
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja amewataka wananchi wanaoishi karibu na mbuga za wanyama kutumia njia mbadala kuzuia tembo kuvamia mashamba na makazi yao kwa kuepuka kulima mazao yanayovutia wanyama hao zikiwemo ndizi.
Kwa muda mrefu sasa, migogoro ya wananchi na wanyamapori wakali katika maeneo ya hifadhi za Taifa imekuwa ikishamiri na kusababisha uharibifu wa mashamba na makazi ya wananchi wanaoishi karibu na hifadhi.
Masanja aliyekuwa akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Aprili 28, 2021 amesema migogoro hiyo inasababishwa na wananchi kuvamia mapitio (ushorobo) ya tembo, hivyo wananchi wanatakiwa kutokulima mazao yanayovutia wanyama hao kupita katika maeneo yao.
“Tuendelee kuhamasisha wananchi waachane na mazao ambayo yanahamasisha tembo kupita katika mashamba yao kama katani. miwa, ndizi na matikiti,” amesema Masanja.
Soma zaidi:
- Mbinu zilizotumika kukomesha ujangili wa tembo Rufiji
- Botswana yapoteza zaidi ya tembo 300 ndani ya miezi mitatu
- Mvutano wa tembo, binadamu unavyoacha maumivu Tanzania – 1
Aidha, Naibu Waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum amesema kama itashindikana kutokulima mazao hayo basi walime pilipili kwenye mipaka ya mashamba na kufuga nyuki karibu na hifadhi za Taifa.
Mbinu nyingine mbadala ni kutumia fensi iliyopakwa oili chafu na pilipili kuzunguka mashamba yao.
Masanja alikuwa alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Cecilia Pareso aliyetaka kufahamu mikakati ya Serikali kuwadhibiti wanayamapori wakali ambao wanavamia mashamba ya wakulima.