November 24, 2024

Mbinu zitakazowasaidia watahiniwa darasa la saba kufaulu vizuri

Wanafunzi watakiwa kujiamini na kuondoa hofu na mashaka kuelekea siku ya mtihani.
• Wadau wa elimu watoa maoni yao mbalimbali kuhusu mtihani huo wa kuhitimu shule ya msingi.

  • Wanafunzi watakiwa kujiamini na kuondoa hofu na mashaka kuelekea siku ya mtihani.
  • Walimu, wadau wa elimu wawatakia heri wanafunzi wote waliobahatika kumaliza elimu ya msingi.
  • Serikali imekamilisha maandalizi yote na kuwataka wasimamizi, walimu kuzingatia kanuni za mitihani.

Dar es Salaam. Kwa Tanzania msingi wa elimu ya mwanafunzi hujengwa tangu akiwa darasa la awali. Hatimaye anaingia shule ya msingi na kusoma kwa miaka saba na kutakiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ili apate fursa ya kujiunga na masomo ya sekondari.  

Mafanikio ya elimu katika ngazi zote yanategemea zaidi maandalizi ya mwanafunzi kukamilisha safari yake ya kuelimika kwa kujipatia maarifa na ujuzi utakamjenga katika taaluma na kuitumikia jamii.

Kesho ni siku mahususi ambayo wahitimu wa darasa la saba kote nchini wanaanza mitihani kukamilisha safari ya miaka saba ya kuwepo shuleni. Lakini ni mlango mwingine wa kuendelea mbele na masomo ya sekondari.

 Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk Charles Msonda, watahiniwa 960,202 wamejiandikisha kufanya mtihani huo, ambapo wasichana wakiwa ni 456,230 sawa na asilimia 47.51 na wavulana ni 503,972 (52.49%) ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 43,130 ya waliofanya mtihani mwaka 2017.

 Wakati zikiwa zimebaki saa chache wanafunzi hao waanze mtihani, yapo maandalizi wanayopaswa kuyafanya ili kufanikisha mitihani ambayo wataifanya kwa siku mbili mfululizo (Septemaba 5 na 6, 2018). 

 Maandalizi hayo yanahusisha akili na mwili yaani kuwa na afya njema na msawazo wa fikra iliyotulia kumuwezesha mwanafunzi kufanya mitihani yote bila hofu, mashaka au kuishia njiani kabla mitihani haijakamilika.

Mtaalamu wa saikolojia ya binadamu, Ernest Nkandi anayefanya shughuli zake Jijini Dodoma anasema dhana hiyo ni hatua ya kwanza kumuweka sawa mwanafunzi kuelekea siku ya mtihani, “Mwanafunzi kwanza anatakiwa awe tayari kiakili na kimwili.”  

Katika kipindi hiki mzazi anashauriwa kuwa karibu na mtoto wake ili kuhakikisha mahitaji na vifaa vya kufanyia mtihani viko mahali pake. Mwanafunzi anapaswa kulala mapema ili kuipa nafasi akili kupumzika.


 “Wasisome mambo mapya mengi siku za mitihani maana akili ya binadamu husahau mambo mengi ya zamani endapo inalazimishwa kuchukua vitu vipya vinavyoenda kutumika kwa muda mfupi,” – Mtaalamu wa Saikolojia, Hamis Abed.


Nkandi anasema siku inayofuata yaani siku ya mtihani, mwanafunzi aamke mapema na kujiaandaa ikiwemo kupata kifungua kinywa ili kuichangamsha akili tayari kuelekea kwenye kituo cha mtihani. 

Pia mzazi au mlezi ahakikishe mtoto amevaa nguo ambazo hazijambana ili kuufanya mwili kuwa mwepesi na kujiachia  wakati wa kuandika bila bugudha yoyote. 

Anapoondoka nyumbani ni vema akabeba vifaa muhimu vinavyohitajika; kalamu zenye wino wa kutosha zisizopungua mbili, penseli iliyochongwa vizuri na ufutio, rula pamoja na mkebe wenye vifaa vya hisabati.

Mwalimu Maiga Muga kutoka Jijini Mbeya anasema ni vema mwanafunzi afike eneo la katika kituo cha mtihani nusu saa au saa moja kabla ya mtihani kuanza ili kuepuka kuchelewa au usumbufu unaoweza kutokea njiani.

“Aanze mtihani kwa kuomba na amalizie kwa kuomba kulingana na imani yake. Wasipoteze muda kwenye  swali moja au ambalo hawajalielewa na kufanya yale anayoyajua,” anabainisha Muga.


 Zinazohusiana: 


Vilevile mwanafunzi anashauriwa asinywe maji au vimiminika vitakavyomfanya kutoka nje ya chumba cha mtihani mara kwa mara ili kutoa haja ndogo. 

Muga ambaye ana uzoefu wa kusimamia mitihani, anasema mwanafunzi akichelewa na kukuta watahiniwa wengine wameanza kufanya mtihani itamjengea hofu na atalazimika kujibu aswali haraka ili kufidia muda, jambo linoloweza kuathiri matokeo yake.

Katika kipindi ambacho, mhitimu ameingia katika chumba cha mtihani anatakiwa kujiamini na kusikiliz maelekezo yote wanayopewa na wasimamizi. Pia kusoma vizuri maelekezo yaliyopo kwenye karatasi ya majibu.  

Hata hivyo, wanafunzi wanashauriwa kujiepusha na vitendo vyote vya udangajifu ikiwemo kupeana majibu au kuharibu mtihani na kufutiwa matokeo.

 

 Mtihani wa darasa la saba ni kilele cha elimu ya msingi ambayo kila mwanafunzi anatakiwa kufanya kuendelea na elimu ya sekondari. Picha| Mtandao

Walimu wawatakia heri wanafunzi

Walimu ambao wana sehemu kubwa ya kufanikisha ndoto za mwanafunzi, wakati huu wanakuwa wamemaliza kazi yao, kinachobaki ni kusubiri matunda ya kazi yao. Lakini pia wametoa ushauri kwa wanafunzi kwamba wanatakiwa kutulia na kuwa na nidhamu wakati wote wa mitihani.

“Walimu wameshafanya kazi yao, kazi iliyobaki ni ya wanafunzi kuwa na utulivu na nidhamu katika mtihani,” anasema Mashaka John, Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Jitegemee iliyopo kata ya Nzovwe Jijini Mbeya.

 Baadhi ya tafiti zinathibitisha kuwa baadhi ya wanafunzi wanafeli sio kwasababu hawakusoma lakini hupatwa na hofu ya mtihani na hali hiyo huondoka muda mfupi baada ya kumaliza mitihani.

 Kwa upande wake, Mwalimu Flora Chilangi kutoka shule ya msingi Twiga ya Jijini Dar es Salaam amewashauri wanafunzi kushirikiana na wasimamizi na kuomba msaada wanapopata changamoto yoyote, “Wawasikilize wasimamizi vizuri wasiwaogope.”

Serikali yakamilisha maandalizi yote ya mitihani

Serikali kupitia Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) imesema wamekamilisha maandalizi yote ya mitihani ikiwemo kufikisha vifaa katika maeneo husika ili kuwawezesha wanafunzi kuanza mitihani mapema. 

Akizungumza na Wanahabari leo, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk Charles Msonda amesema wanafunzi wasiwe na hofu kwasababu mazingira katika vituo vya kufanyia mitihani yako salama na tulivu. 

 “Vijana watafanya mtihani kwa amani na utulivu, kwa kuzingatia kanuni zote za uendeshaji wa mitihani ya kitaifa,” anasema Dk Msonda.

Amebainisha kuwa ili mitihani ifanyike kwa mafanikio makubwa, wasimamizi, wamiliki wa shule na walimu wanapaswa kuzingatia kanuni za mitihani ili kuepusha usumbufu na udanganyifu unaoweza kuwatia hatiani.

 “Kamati zote za mitihani za mikoa, halmashauri na manispaa nchini kuhakikisha kwamba taratibu zote zinazohusika na uendeshaji wa mitihani ya Taifa zinazingatiwa ipasavyo. Kamati zote zinaagizwa kuhakikisha mazingira yote ya vituo vya mitihani yako salama, tulivu kuwawezesha watoto wetu kufanya mitihani kwa amani kabisa,” anasema Dk Charles Msonde.