October 6, 2024

MCT wajitosa kuongeza idadi ya wanawake kuripoti habari za kilimo

Hatua huyo imelenga kuhakikisha wanahabari wanatoa elimu kwa mkulima namna ya kufanya kilimo cha kisasa na chenye tija kitakachoongeza kipato.

Meneja wa miradi wa Baraza la Habari Tanzania ,Pili Mtambalike katikati akitambulisha rasmi vipengele vitakavyoshindaniwa katika tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari kwa mwaka 2018. Kulia ni Paul Malimbo, Afisa Mwandamizi wa Miradi wa MCT na kushoto ni Humphrey Mtuli ambaye pia ni Afisa Mwandamizi wa Miradi wa baraza hilo. Picha|Tulinagwe Malopa.


  • Hatua huyo imelenga kuhakikisha wanahabari wanatoa elimu kwa mkulima namna ya kufanya kilimo cha kisasa na chenye tija kitakachoongeza kipato. 
  • Waandishi wasisitizwa kuandika habari za kilimo ili mchango wa mwanamke katika kilimo uweze kutambulika.

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha wanawake wengi wanashiriki katika tasnia ya habari, Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeanzisha tuzo maalum kwa wanawake wanaoripoti habari za kilimo na kilimobiashara ili kuchochea ukuaji wa sekta hiiyo nchini.

Licha ya kilimo kuwa uti wa mgongo wa uchumi kwa kuajiri idadi kubwa ya wanawake bado habari zake zimekuwa haziripotiwi kwa wingi kama inavyohitajika na sehemu kubwa ya ambao huziripoti kwa sasa huwa ni wanaume.

Ripoti ya Utafiti ya Nguvu Kazi ya mwaka 2014  iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha sekta ya kilimo imeajiri wanawake zaidi kuliko wanaume. Katika ripoti hiyo, asilimia 52 ya wanaojishughulisha na kilimo ni wanawake.. 

Kutokana na umuhimu wa sekta hiyo, MCT katika Tuzo za 10 za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) wametoa nafasi ya upekee kwa  wanawake  wanaoripoti habari za kilimo na kilimobiashara ili kuwapa motisha ya kuripoti zaidi habari hizo. EJAT ni tuzo za juu na za heshima zaidi kwa tasnia ya habari Tanzania na hufanywa kila mwaka. 

Meneja Miradi wa MCT,  Pili Mtambalike  amewaambia wanahabari leo (Septemba 19, 2018) kuwa  tuzo hizo za kilimo kwa wanawake wanaoripoti habari za kilimo na kilimobiashara zitafadhiliwa na Jukwaa la kilimo la asasi za kiraia  Agriculture Non-State Actors Forum (ANSAF).

“Wanawake waandishi wa habari wajitokeze kwa wingi kuleta habari zao za kilimo ili ziweze kushindanishwa,” amesema Mtambalike.

Hatua hiyo imelenga kuhakikisha wanahabari wanatoa elimu kwa mkulima namna ya kufanya kilimo cha kisasa na chenye tija kitakachoongeza kipato. 

Baadhi ya wanahabari wameeleza kuwa hiyo ni fursa nyingine ya kumkomboa mwanamke katika sekta ya kilimo na biashara za kilimo kupitia habari. 

“Waandishi tujitahidi kutuma kazi zaidi hasa za kilimo ili mchango wa mwanamke uweze kutambulika katika jamii,” ameeleza Zuhura Mikidadi, Mtangazaji wa kituo cha redio Magic FM.


Zinazohusiana: Wajasiriamali 5 kuiwakilisha Tanzania jukwaa la uwekezaji Afrika

                          Wanahabari wahimizwa kuandika habari za kilimo, sayansi kukuza uchumi wa viwanda


Mtambalike ameeleza kuwa ushiriki wa wanahabari wanawake katika tuzo hizo kwa mwaka 2017 ulikuwa mdogo ukilinganisha na mwaka 2016. Mwaka jana kazi 545 ziliwasilishwa kwa ajili ya kuwania tuzo hizo huku 206 zikiwa ni za wanawake sawa na asilimia 37.8 ya mawasilisho yote.

Ili kuwa na idadi kubwa ya washiriki, MCT imewaomba wanahabari kujitokeza kwa wingi kuwasilisha kazi katika kinyang’anyiro hicho na kwamba mwisho wa kupokea kazi za waandishi ni Januari 31, 2019.