July 3, 2024

MCT yalaani unyanyasaji waandishi wa habari Tanzania

Baraza la Habari Tanzania (MCT) limelaani kuendelea kwa matukio ya unyanyasaji wa waandishi wa habari unaofanywa na vyombo vya dola na baadhi ya viongozi wa Serikali pamoja na wananchi.

  • Yasema vitendo hivyo vinafanywa na vyombo vya dola na baadhi ya viongozi wa Serikali pamoja na wananchi.
  • Yasema uandishi wa habari ni kazi halali na inatakia iheshimiwe. 
  • Maagizo ya Rais Samia kuhusu uhuru wa vyombo vya habari yaheshimiwe. 

Dar es Salaam. Baraza la Habari Tanzania (MCT) limelaani kuendelea kwa matukio ya unyanyasaji wa waandishi wa habari unaofanywa na vyombo vya dola na baadhi ya viongozi wa Serikali pamoja na wananchi. 

Tamko hilo la MCT limekuja siku moja baada ya mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi, Jesse Mikofu kushambuliwa na askari wa SMZ wakati akifanya kazi yake ya uandishi wa habari visiwani Zanzibar.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, imesema itawachukulia hatua askari wote waliomshambulia mwandishi huyo.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Awadh Juma amesema taarifa za kushambuliwa mwanahabari huyo na hivyo hawezi kuzungumzia suala hilo.

“Ameripoti kwenye kituo gani cha polisi?, mimi sina taarifa,” Kamanda Juma ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz). 

Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Kajubi Mukajanga katika taarifa ya leo Aprili 22, 2021 amesema bado hali ya uminywaji wa vyombo vya habari na wanahabari unaendelea. 

“MCT inapenda kuvikumbusha vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa Serikali na wananchi kwa ujumla kuwa uandishi wa habari sio tu ni kazi halali, bali pia ni ya muhimu sana kwa jamii yetu hatuna budi kuiheshimu na kuipa ushirikiano wakati utakapohitajika,” amesema Mukajanga.

Amesema Aprili 6, 2021 Rais Samia aliiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo  kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa na kuagiza wahusika kutotumia ubabe kuvidhibiti.

“Maagizo ya Rais ni kwamba hapendezwi na hali hii ya unyanyaswaji wa vyombo vya habari na wanataaluma wake, baraza linashangazwa na hali inavyokwenda hivi sasa maana mara baada ya maagizo vitendo vya ukiukwaji wa haki za waandishi vimeshamiri kinyume na matarajio ya Watanzania,” amesema Mukajanga.


Soma zaidi: 


Mukajanga ametaja matukio matano ya unyanyasaji wanahabari ambayo yametokea hivi karibuni likiwemo la Aprili 12, 2021 ambapo waandishi wa habari Christopher James wa ITV na Dickson Bilikwija wa Island TV waliwekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa maagizo ya Mkurugenzi wa Halmashauari ya Temeke, Lusabilo Mwakabibi.

Tukio jingine lilitokea Mwanza Aprili 9, 2021 ambapo Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,  Philis Nyimbi alimtishia mwandishi kuwa atamfanya kitu ambacho kitamsababisha aachishwe kazi, kutokana na mwandishi huyo Mabere Makubi  kuandika habari ambazo alidai zinahatarisha maisha yake.

 “Aprili 12, 2021 mwandishi wa kujitegemea wa gazeti la The Guardian kutokea mjini Moshi, James Lanka alikamatwa na polisi na kuwekwa mahabusu kwa siku tatu mfululizo bila kufunguliwa mashtaka wala kuchukuliwa maelezo, baada ya kuhoji sababu za wafanyabiashara kukamatwa bila utaratibu,” amesema Mukajanga.

Kwa mujibu wa Mukajanga, tukio jingine lilitokea Katavi ambapo mwandishi wa Channeli 10, Pascal Katona alihudhuria shughuli za uchaguzi wa Imamu  wa msikiti wa Makanyagio ulioko Manispaa ya Mpanda kwa ajili ya kupata taarifa ya matokeo lakini  alivamiwa na wananchi kumshambulia na kumuharibia vifaa vyake.

“Bado kuna tukio la Aprili 21, 2021  huko Zanzibar mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi, Jesse Mikofu alishambuliwa na askari wa JKU wakati akifanya kazi yake ya uandishi wa habari,” amesema. 

Amesema kuendelea kuminya uhuru wa vyombo vya habari na kunyanyasa waandishi wa habari ni kwenda kinyume na maagizo ya Rais na haileti picha nzuri kwa Taifa na nje ya nchi. 

Aprili 17 mwaka huu, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema atahakikisha waandishi wa habari wanalinda na kuwataka kufuata sheria za nchi zilizopo ili wasiingie kwenye matatizo.