October 6, 2024

Membe amwelezea Mengi alivyoipaisha diplomasia ya Tanzania kimataifa

Amesema alikuwa kiungo muhimu kwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao, Serikali na sekta binafsi.

Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika Serikali ya awamu wa nne, Bernard Membe amesema kutokana mchango wake katika diplomasia ya Tanzania angependa Watzania na dunia imfahamu Mengi kuwa alikuwa mshauri wa mabalozi Tanzania. Picha|Mtandao.


  • Amesema alikuwa kiungo muhimu kwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao, Serikali na sekta binafsi.
  • Alijitoa kuzisaidia nchi jirani zilizokuwa zinakabiliwa na tatizo la njaa.

Dar es Salaam. Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika Serikali ya awamu wa nne, Bernard Membe amesema marehemu Dk Reginald Mengi alichangia kwa sehemu kubwa kuipaisha diplomasia ya Tanzania kimataifa ikiwemo kuwaunganisha mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao na Serikali katika shughuli za maendeleo ya sekta binafsi. 

Membe aliyekuwa akizungumza leo (Mei 9, 2019) kando ya ibada ya mazishi ya marehemu Mengi iliyofanyika katika kanisa la KKKT usharika wa Moshi mjini, amesema alimfahamu Mengi mwaka 1999 na tangu wakati huo amekuwa naye karibu katika shughuli mbalimbali zikiwemo za kiserikali. 

Amemuelezea Mengi katika muktadha wa kuwa mshauri wa mabalozi na mtu aliyejitoa kuwasaidia wananchi wa nchi jirani ambao walikuwa wanakabiliwa na majanga ya njaa katika maeneo yao. 

“Ni vema Watanzania wajue tu nimesema na narudia kwamba Mhe. Mengi alikuwa kama mshauri wa mabalozi na alifanya kazi vizuri na wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa,” amesema Membe ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Mtama mkoani Lindi. 

Amesema siyo tu alikuwa anashauri mabolozi kuhusu sekta binafsi na masuala mbalimbali ya biashara lakini alikuwa kiungo cha Serikali na sekta binafsi; kiungo cha Serikali na mabolozi hasa kuhusiana na sekta binafsi kama gurudumu halisi la maendeleo.

Ameweka wazi kuwa alitimiza shughuli za diplomasia kivitendo ambapo kila mwezi alikuwa anawaalika mabalozi wawili, watatu nyumbani kwake kula nao chakula.

“Mabolozi kwa upande wao kila mwaka wanapokuwa wanaadhimisha uhuru wa Taifa lao, mzee Mengi hukosi kumuona pale,” amesema Membe na kuongeza kuwa “mara nyingi Waziri wa Mambo ya Nje mimi na mzee Mengi tulikuwa bega kwa bega. Mimi nachapa siasa, yeye anachapa uchumi katika sekta binafsi.” 


Soma zaidi:


Awasaidia wananchi wa Somalia kupata chakula

Mengi hakuishia kuianganisha Tanzania na mataifa makubwa duniani bali alitumia turufu yake ya uongozi kuimarisha uhusiano mzuri kati ya Tanzania na nchi jirani ikiwemo Somalia. 

Somalia ilipopata matatizo ya njaa ambayo yaliwakabili watu 10 milioni mwaka 2009 na 2010, Rais Jakaya Kikwete alimteua Dk Mengi kuwa Mwenyekiti wa wafanyabiashara wote ambao walitakiwa kuichangia chakula Somalia ambayo ilikuwa katika hali mbaya ya kiuchumi. 

“Dk Mengi alifanya kazi kubwa akishirikiana na wizara ya mambo ya nje kupata michango kutoka kwa wafanyabiashara, chakula, sabuni, sukari, mafuta na nguo. Alifanya kazi nzuri tukapata malori kadhaa ambayo yalipeleka moja kwa moja chakula Somalia kwa waathirika wa njaa kupitia Kenya,” ameeleza Membe. 

Membe amesema kutokana mchango wake katika diplomasia ya Tanzania angependa Watzania na dunia imfahamu Mengi kuwa alikuwa mshauri wa mabalozi Tanzania.