October 6, 2024

Mfuko maalum kukopesha wawekezaji waanzishwa Tanzania

Serikali imeanzisha mfuko maalum wa kukopesha watu wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda vya kati na vikubwa, lengo likiwa ni kuwanufaisha Watanzania waliokosa mitaji na wenye nia ya kuwekeza nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki pamoja na meza kuu wakifuatilia hoja wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki na Wanachama wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Uswidi na Afrika Mashariki kaika Ukumbi wa Mikutano Serena Hotel Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Machi, 2020. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Utatoa mikopo kwa watu wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda vya kati na vikubwa.
  • Utawanufaisha Watanzania waliokosa mitaji na wenye nia ya kuwekeza nchini.
  • Serikali yasema inaendelea kuboresha mazingira ya biashara ili kuvuti wawekezaji.

Dar es Salaam. Wawekezaji wa ndani ambao walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya uanzishaji wa miradi ya kiuchumi, sasa wana kila sababu ya kutabasamu maana wamewekewa njia nzuri ya kupata mikopo hiyo. 

Serikali imeanzisha mfuko maalum wa kukopesha watu wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda vya kati na vikubwa, lengo likiwa ni kuwanufaisha Watanzania waliokosa mitaji na wenye nia ya kuwekeza nchini.

Mfuko huo ulioanzishwa Februari 22 mwaka huu utakuwa ukikopesha Watanzania kuanzia kiwango cha Sh8  milioni hadi Sh50 milioni kwa wenye nia ya kuwekeza viwanda vya kati na Sh50 milioni hadi Sh300 milioni kwa wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda vikubwa.

Mfuko huo unaendeshwa na Mfuko wa Hifadhi za Jamii (NSSF), Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Shirika la Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki alieleza hayo jana (Machi 12, 2020) wakati akizungumza na Waandishi wa Habari  mara baada ya kufungua Kongamano la pili la Biashara na Uwekezaji la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Sweden linaloendelea kwa siku mbili Jijini Dar es Salaam.

Amesema mfuko huo utasaidia wawekezaji kupata mitaji kuwekeza na kuendeleza uzalishaji viwandani, jambo litakalosaidia Serikali kupata mapato na wananchi kuhakikishiwa bidhaa bora.


Soma zaidi: 


Wakati akifungua kongamano hilo Kairuki aliwataka Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza nchini Tanzania kwa kueleza kuwa Sera, Sheria na miundombinu yake imeboreshwa kwa kiwango kikubwa.

“Tunazo fursa nyingi za uwekezaji hapa Tanzania, tuna fursa kwenye Kilimo cha mazao ya chakula na biashara pamoja na mnyororo wake wa thamani kwenye sekta hiyo, tunahitaji uwekezaji wa viwanda mbalimbali vikiwepo vya dawa na  vifaa tiba, mafuta ya kula na vinginevyo vingi,” amesema Kairuki.

Kongamano hilo limehudhuriwa na zaidi ya makampuni makubwa 20 toka Sweden kupitia Chama chao cha Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Afrika Mashariki (SWEACC).

Mwenyekiti wa SWEACC Jan Furuvald amesema uwekezaji kwenye nchi za EAC umekuwa na manufaa kutokana na kuwa na soko kubwa la watumiaji wa bidhaa zao na kuwataka wawekezaji kuja kuwekeza Afrika Mashariki.

“Sisi Wafanyabiashara na wawekezaji mara nyingi tunaangalia mazingira mazuri ya uwekezaji, kuwekeza kwenye nchi za Afrika Mashariki kunatuhakikishia soko kubwa kwani licha ya kuwa kwenye jumuiya hii pia kuna fursa nyingine za SADC”, amesema Furuvald.

Kongamano hilo lenye kauli mbiu ya “Suluhisho la Kijani kwenye Majiji ya Afrika Mashariki” linalenga kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwenye majiji yaliyopo kwenye Jumuiya hiyo.