October 7, 2024

Mfumo wa mawasiliano ya wakulima wazinduliwa Dar

Unawaunganisha wakulima ili kutatua changamoto za kilimo bila kuhitaji maafisa ugani.

  • Unawaunganisha wakulima ili kutatua changamoto za kilimo bila kuhitaji maafisa ugani. 
  • Unatumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS).

Dar es Salaam. Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao katika Wizara ya Kilimo, Beatus Malema amezindua mfumo wa mawasiliano wa kidijitali wa ‘WeFarm’ leo utakaowasaidia wakulima kuwasiliana na kutatua changamoto za kilimo kwa haraka na urahisi.

Malema aliyekuwa akizungumza leo (Juni28, 2019) Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mfumo huo, amesema ukitumika vizuri utawasaidia wakulima kupata suluhu ya changamoto wakati wakitekeleza shughuli za uzalishaji katika sekta ya kilimo. 

“Lengo la mfumo huu ni kuimarisha mawasiliano. Matumizi ya mfumo huu yatamuwezesha mkulima kuweza kutuma ujumbe na kuuliza chochote kinacho mkabili shambani kwake ama katika eneo lake la kazi na mfumo huo utamjibu yeye na watu wengine wanao fuatilia,” amesema Malema.

Sekta ya kilimo ina mchango wa asilimia 28.7 kwenye pato la taifa na hivyo kuifanya sekta hiyo kuwa miongoni mwa sekta zilizoajiri Watanzania wengi zaidi hapa nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Wefarmtz Limited  inayoendesha mfumo huo, Nicholaus John amesema mfumo huo unatumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kwa kuunganishwa na simu za wakulima. 

Amesema, kama mkulima yuko shambani na akipata tatizo anaandika ujumbe mfupi wa maneno ambao utawafikia wakulima wenye uzoefu na ujuzi katika kilimo ili kumpatia majibu. 

“Tunafanya kazi kwa karibu na serikali na hata wataalamu mbalimbali kutoka taasisi binafsi.  Tunaamini tutasaidia wakulima kutatua changamoto wanazopitia kwa kutumia viganja vyao,” amesema Nicholaus.

Katika kipindi kifupi tangu mfumo huo uanze kufanya kazi katika mikoa ya Iringa na Mbeya umeweza kuwafikia wakulima takriban 50,000 huku maswali mengi yanayoulizwa yako upande wa masoko, magonjwa ya mazao na mabadiliko ya hali ya hewa. 


Soma zaidi: 


Ubunifu wa teknolojia katika sekta ya kilimo umekuwa ukihamasishwa zaidi ulimwenguni kwa sasa ili kuhakikisha wakulima wanaongeza ufanisi katika uzalishaji wao. 

Mkulima kutoka Mbeya, Khalfan Athuman ambaye ni mnufaika wa mfumo wa WeFarm amesema mfumo huo umemsaidia kujibu maswali mbalimbali ya kilimo cha matunda na mbogamboga.

Kutokana na ufanisi wa mfumo huo, uzalishaji wa kilimo anachokiendesha umeongezeka hasa baada kuzingatia majibu aliyoyapata kutokana na maswali aliyouliza.

Hata hivyo, Malema amesihi mtandao huo kutekeleza kile ambacho inaahidi wakulima wa Tanzania na pia kuzingatia kuwaelimisha wakulima juu ya kilimo endelevu.

“Tunahitaji kilimo kitakachoenda sambamba na mabadiliko ya tabia nchi. Mtu akilima leo aweze kulima na kesho,” amesema.