July 5, 2024

Mfumuko wa bei Tanzania wakwama kiwango cha Julai 2020

Ripoti ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Agosti 2020 inaeleza kuwa kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma ilibaki asilimia 3.3 kama ilivyokuwa Julai 2020.

  • Ripoti ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Agosti 2020 inaeleza kuwa kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma ilibaki asilimia 3.3 kama ilivyokuwa Julai 2020.
  • Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Agosti umeongezeka kidogo hadi kufikia asilimia 3.7 kutoka asilimia 3.8 ilivyorekodiwa Agosti 2019.
  • Baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizopungua bei kwa mwezi Agosti 2020 ni pamoja na mahndi, unga wa ngano na mihogo. 

Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Agosti 2020 imeendelea kubaki kama ilivyokuwa mwaka ulioishia Julai, 2020, jambo linaloonyesha mwenendo imara wa mabadiliko ya bei katika kipindi hicho.

Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na zinazotumiwa na kaya binafsi nchini. 

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Agosti 2020 ulikuwa asilimia 3.3 ikiwa ni sawa kabisa na kiwango kilichorekodiwa katika mwaka ulioishia Julai 2020.

Taarifa ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali iliyotolewa  leo (September 8, 2020) imeeleza kuwa hali hiyo imechangiwa na kuongezeka na kupungua kwa bei za baadhi za vyakula na bidhaa zisizo za chakula kwa kipindi kilichoishia Agosti 2020 ikilinganishwa na bei za Agosti 2019. 


Soma zaidi: 


Licha ya mfumuko wa jumla kubaki tambalale, taarifa hiyo inaeleza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Agosti 2020 umepungua hadi kufikia asilimia 3.7 kutoka asilimia 3.8 ilivyokuwa Julai 2020. 

“Baadhi ya bidhaa zilizopungua bei kwa mwezi Agosti, 2020 ikilinganishwa na Agosti 2019 ni pamoja na mahindi kwa asilimia 5.8, unga wa ngano asilimia 1.1, mihogo kwa asilimia 16.3 na viazi vitamu kwa asilimia 11.9.

“Kwa upande mwingine, baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoongezeka bei kwa mwezi Agosti 2020, ikilinganishwa na bei za mwezi Agosti  2019 ni pamoja na mavazi kwa asilimia 2.2, ada za shule za msingi na sekondari za binafsi kwa asilimia 2.4 na huduma za malazi kwenye nyumba za wageni kwa asilimia 2.8,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo. 

 

Hali ya Afrika Mashariki

Mfumuko wa bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki, taarifa inaonyesha kuwa mfumuko wa bei nchini Kenya kwa mwaka unaoishia Agosti 2020 umebaki kiwango kile kile cha asilimia 2.36 kilichorekodiwa mwaka unaoishia Julai 2020.

Taarifa ya mfumuko wa bei katika nchi ya Uganda katika mwaka ulioishia Februari 2020, zinaonyesha kuwa mfumuko wa bei umepungua kidogo hadi asilimia 4.6 mwaka unaoishia Agosti 2020 kutoka asilimia 4.7 mwaka ulioishia Julai 2020.