November 24, 2024

Mfumuko wa bei Tanzania wakwama kiwango cha Septemba 2020

Ripoti ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Oktoba 2020 inaeleza kuwa kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma ilibaki asilimia 3.1 kama ilivyokuwa Septemba 2020.

  • Ripoti ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Oktoba 2020 inaeleza kuwa kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma ilibaki asilimia 3.1 kama ilivyokuwa Septemba 2020.
  • Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Oktoba umebaki kwa asilimia 3.4 kama ilivyokuwa Septemba 2020.
  • Baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizopungua bei kwa mwezi Agosti 2020 ni pamoja na mahndi, unga wa ngano na mihogo.

Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Oktoba 2020 imeendelea kubaki kama ilivyokuwa Septemba mwaka huu jambo linaloonyesha mwenendo imara wa mabadiliko ya bei katika kipindi hicho.

Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na zinazotumiwa na kaya binafsi nchini. 

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Oktoba 2020 ulikuwa asilimia 3.1 ikiwa ni sawa kabisa na kiwango kilichorekodiwa katika mwaka ulioishia Septemba 2020.

Taarifa ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali iliyotolewa  leo (Oktoba 9, 2020) imeeleza kuwa hali hiyo imechangiwa na kuongezeka na kupungua kwa bei za baadhi za vyakula na bidhaa zisizo za chakula kwa kipindi kilichoishia Oktoba 2020 ikilinganishwa na bei za Oktoba 2019.


Soma zaidi: 


Licha ya mfumuko wa jumla kubaki tambalale, taarifa hiyo inaeleza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Oktoba 2020 umebaki kuwa asilimia 3.4 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezI Septemba 2020. 

“Baadhi ya bidhaa zilizopungua bei kwa mwezi Oktoba, 2020 ikilinganishwa na Oktoba 2019 ni pamoja mchele kwa asilimia 4.2, mahindi kwa  asilimia 12.1, unga wa mahindi kwa asilimia 3.2, unga wa ngano kwa asilimia 0.9, unga wa mtama kwa asilimia 0.8 unga wa muhogo kwa asilimia 1.2, mihogo mibichi kwa asilimia 2.5, viazi vitamu kwa asilimia 5.4 na ndizi za kupika kwa asilimia 5.4,” imesema taarifa hiyo.

Kwa upande mwingine, baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoongezeka bei kwa mwezi Oktoba 2020, ikilinganishwa na bei za mwezi Oktoba 2019 ni pamoja na mavazi kwa asilimia 2.2, gesi ya kupikia kwa asilimia 6.5, mkaa kwa asilimia 8.8, ukarabati na vifaa vya usafiri kama magari kwa asilimia 8.3 na samani kwa asilimia 1.4.