July 8, 2024

Mfumuko wa bei wazidi kushuka Tanzania

Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini Tanzania imeshuka hadi kufikia asilimia 3.3 kwa mwaka ulioishia Aprili 2020 kutoka asilimia 3.4 iliyorekodiwa Machi mwaka huu,

  • Umeshuka hadi kufikia asilimia 3.3 kwa mwaka ulioishia Aprili 2020 kutoka asilimia 3.4 iliyorekodiwa Machi mwaka huu.
  • Umechagizwa zaidi na kupungua kwa gharama za bidhaa za chakula na zisizo za chakula.
  • Hiyo ni mara ya pili kushuka kama ilivyokuwa mwezi Machi baada ya kung’ang’ania katika kiwango kimoja Januari na Februari. 

Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini Tanzania imeshuka hadi kufikia asilimia 3.3 kwa mwaka ulioishia Aprili 2020 kutoka asilimia 3.4 iliyorekodiwa Machi mwaka huu, ikichagizwa zaidi na kupungua kwa gharama za bidhaa za chakula na zisizo za chakula.

Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.

Ripoti ya mfumuko wa bei ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyotolewa leo (Mei 8, 2020) imeeleza kuwa kushuka kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei za bidhaa za chakula na zisizokuwa za chakula ikilinganishwa na Machi mwaka huu.

Mfumko wa bei  wa bidhaa zisizo za chakula ambazo umeshuka ni pamoja na mafuta ya taa ambayo yamepungua kwa asilimia 4.6, dizeli kwa asilimia7.2 na petroli kwa asilimia 3.8. 

Kwa upande wa bidhaa za vyakula na vinywaji, mfumuko wa bei umeshuka hadi asilimia 4.6 kutoka asilimia 5.3 iliyorekodiwa Machi 2020.


Soma zaidi:


Sambamba na bidhaa hizo, bidhaa na huduma zingine kama hoteli, migahawa na huduma za elimu hazijabadilika kabisa huku huduma za tamaduni na mapumziko (recreation) zikishuka kwa asilimia 0.4.

Hiyo ni mara ya pili mfululizo kwa mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kushuka baada ya kushuhudiwa pia katika mwaka ulioishia Machi 2020 ambapo ulishuka kutoka asilimia 3.7 ya mwaka ulioishia Februari 2020. 

Kushuka kwa mfumuko wa bei kwa miezi miwili mfululizo kumetokea baada ya kasi yake kung’ang’ania katika kiwango kimoja kwa miezi ya Januari na Februari 

Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Februari 2020 ulikuwa asilimia 3.7 ikiwa ni sawa kabisa na kiwango kilichorekodiwa katika mwaka ulioishia Januari 2020.