November 24, 2024

Mgawanyiko usio sawa vituo vya ubunifu unavyoathiri ukuaji wa teknolojia Tanzania

Mpaka kufikia Septemba 2018 kulikuwa na vituo 43 katika mikoa tisa ya Tanzania bara na vinne tu vipo Zanzibar.

  • Mpaka kufikia Septemba 2018 kulikuwa na vituo 43 katika mikoa tisa ya Tanzania bara na vinne tu vipo Zanzibar.
  • Karibu nusu ya vituo hivyo vya ubunifu viko Jijini Dar es Salaam.
  • Wadau wamesema ukosefu wa ushirikiano na mipango endelevu unachangia vituo hivyo kushindwa kujitanua katika mikoa mingine.

Dar es Salaam. Licha ya umuhimu wake katika maendeleo ya sayansi na teknolojia, mgawanyiko wa vituo vya ubunifu wa teknolojia nchini (innovation hubs) bado haujazingatia usawa wa kimkoa jambo linalosababisha vijana katika baadhi ya mikoa kukosa fursa ya kunoa na kuendeleza ubunifu wao. 

Vituo vya ubunifu ni maeneo ya kijamii, maeneo ya kufanyia kazi au utafiti ambayo yanatoa fursa ya kutumia teknolojia kuendeleza maarifa na ujuzi unaosadia kutafuta suluhisho la matatizo yaliyopo katika jamii. 

Ripoti ya utafiti wa mtawanyiko wa vituo vya ubunifu Tanzania (A mapping of Tanzanian hubs and innovation spaces) iliyotolewa Novemba 2018 na Mfuko wa Ubunifu wa Maendeleo ya Watu (HDIF) unaeleza kuwa Tanzania ina vituo vya ubunifu 43 ambapo  hutofautiana kutokana na utendaji wake, makundi yanayokusudiwa, huduma zinazotolewa na mfumo wa kibiashara lakini vinagawanyika katika makundi matatu;

“Kundi la kwanza linajumuisha kwa sehemu vituo rasmi vyenye bajeti, bodi, teknolojia au kujikita sekta moja na wafanyakazi wachache walioajiriwa. Kundi la pili linajumuisha vituo vya kijamii visivyo rasmi ambavyo vimejikita katika ujuzi, ajira na maendeleo ya nguvu kazi na jamii, Vinaishi kutokana na shughuli za kujitolea.”

“Kundi la tatu linaundwa na vituo visivyohuru ambavyo vinamilikiwa na kuendeshwa na mashirika na vyuo kama COSTECH (Tume ya Sayansi na Teknolojia) ambavyo vilianzisha kama sehemu ya miradi na havijakusudiwa kudumu muda mrefu,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo. 

Ripoti hiyo inaeleza kuwa vituo vingi vimeanzishwa baada ya mwaka 2010 huku idadi ya vituo ikiongezeka kwa kujikongoja licha ya kuwa takriban vituo saba vimefungwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo kukosa mtaji wa kujiendesha.

Hata hivyo, mtawanyiko wa vituo hivyo haujazingatia usawa wa kimkoa na vingi viko katika maeneo ya mjini na kuwanyima fursa vijana wengi waliopo vijijini. 

Vituo hivyo 39 vinapatikana Tanzania Bara katika mikoa tisa tu huku vinne vilivyosalia vikiwa visiwani Zanzibar. Kwa tafsiri rahisi ni kuwa kuna mikoa 19 kati ya 26 ya Tanzania Bara haina vituo hivyo. 

Hiyo ni sawa kusema robo tatu au asilimia 73 ya mikoa ya Tanzania Bara haina vituo vya ubunifu jambo linaloibua maswali juu ya juhudi za kuendeleza sayansi na teknolojia nchini.

Licha ya vituo vilivyopo kufanya kazi kubwa katika kuendeleza ubunifu na ujasiriamali wa teknolojia, navyo havijatawanyika kikamilifu katika wilaya na kata ili kuwafikia watu wengi zaidi  wanaopatikana katika maeneo husika kutokana na kujengwa mjini na vinalenga kuwafikia watu maalum. 

Mathalani, Jiji la Dar es Salaam linaongoza kuwa na vituo vingi vinavyofikia 21 sawa na asilimia 48 ya vituo vyote vilivyopo Tanzania au sawa na kusema kwa kila vituo 10 vya ubunifu vilivyopo nchini basi vitano viko jijini hapa. 

Lakini vituo hivyo vinapatikana zaidi kando kando mwa barabara ya Old Bagamoyo na Ali Hassan Mwinyi na maeneo ya jirani hasa Morocco, Victoria na Makumbusho. Baadhi ya vituo hivyo ni Buni Hub ambacho kiko chini ya Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Sahara Ventures,  Atamizi ya Biashara na Teknohama (DTBi), Smart Lab na kituo cha SeedSpace kilichoanzishwa mwishoni mwa mwaka 2018.

Hali kama hiyo huenda ikawatenga watu waliopo nje ya jiji kama walivyo wa vijijini ambao hawafikiwi kabisa na huduma za vituo hivyo, licha ya kuwa na mawazo ya kibunifu ambayo yangeendelezwa yangesaidia kupunguza changamoto mbalimbali za jamii. 

Hata mkoa wa Arusha unaosifika kwa shughuli za utalii na masuala ya kimataifa lina vituo sita tu ukifuatiwa na Iringa na visiwa vya Zanzibar yenye vituo vinne. Mkoa wa Mbeya una vituo viwili ambapo kimoja kinamilikiwa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MIST).

Kwa wakazi wa Lindi na Mtwara wao wanalazimika kutumia vituo vya shirika la kimataifa la VSO linaloendesha miradi ya kijamii kuwawezesha vijana na wanawake kutumia fursa zinazowazunguka kupata kipato. 


Zinazohusiana: 


Kwanini hali hiyo?

Ripoti ya HDIF inaeleza kuwa vituo vingi vya ubunifu vinashindwa kukua na kutawanyika katika maeneo mbalimbali nchini kwa sababu vinaanzishwa kwa juhudi binafsi za watu kuliko taasisi, jambo linaloibua changamoto ya upatikanaji wa mitaji na wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika vituo endelevu.

Meneja Mkuu wa kampuni ya uwekezaji na uendelezaji wa ujasiriamali wa teknolojia ya SeedSpace Tanzania, Innocent Mallya ameiambia nukta.co.tz kuwa kukosekana kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali wa teknolojia kumekuwa kikwazo kwa vituo vya ubunifu kukua kwa haraka.

Hali hiyo pia imekuwa ikiathiri ukuaji wa kampuni za teknolojia zinazochipikua (Startups) ambazo zinategemea vituo hivyo kupata maarifa na ujuzi wa kuendeleza shughuli zao kwenye jamii.

Hata hivyo, Mallya anasema bado fursa ipo ya kujenga mfumo imara wa teknolojia nchini ikiwa tu wadau watakuwa na jicho la kujenga vituo katika mikoa mingine ya Tanzania, kuziandaa kampuni zinazochipykia (startups) kuvutia na kupata mitaji ya uwekezaji kutoka kwa wawekezaji ili kuongeza fursa za ajira. 

Costech kwa kushirikiana na mashirika ya maendeleo kama HDIF na balozi mbalimbali zinazowakilisha nchi zao Tanzania zimekuwa mstari wa mbele kuviwezesha kimtaji, maarifa na ujuzi vituo vya ubunifu ili kuleta matokeo chanya kwenye jamii. 

Kwa pamoja wawekezaji na wafadhili wanaweza kusaidia muunganiko mzuri katika ya vituo vya ubunifu, sekta binafsi, Serikali na mashirika ya kijamii. 

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika  la Foundation for Civil Society, Francis Kiwanga anasema ubunifu ukiwekewa mikakati mizuri ikiwemo kuyafikia maeneo ya vijijini unaweza kusaidia kuleta mabadiliko chanya katika jamii ikiwemo kupunguza umaskini na changamoto za ajira kwa vijana.