July 8, 2024

Mgogoro wa ardhi unavyosababisha wanafunzi 200 wabanane darasa moja Mbeya

Darasa moja la Shule ya Msingi Inyala mkoani Mbeya linabeba wastani wa wanafunzi 193 mara nne zaidi ya kiwango kinachopendekezwa.

  • Darasa moja la Shule ya Msingi Inyala mkoani Mbeya linabeba wastani wa wanafunzi 193 mara nne zaidi ya kiwango kinachopendekezwa.
  • Baadhi ya madarasa yaliyopo katika shule za msingi za umma za jiji la Mbeya hayapo katika mazingira rafiki kusomea wanafunzi.
  • Ni wakati wa Serikali na wadau kushirikiana kuboresha miundombinu katika shule za umma nchini.

Mbeya. Sarafina Ndonde, mwanafunzi wa darasa la tano shule ya msingi Inyala kata ya Iyunga jijini Mbeya, ana ndoto. Siku atakapomaliza masomo yake na kuwa mkubwa anataka kuwa rais ili kuwakomboa wanyonge. 

Hata hivyo, safari yake siyo rahisi. Ili afikie malengo ya safari hiyo, Sarafina atatakiwa kukabiliana na changamoto lukuki zinazomkabili kwa sasa shuleni kwao ikiwemo wingi wa wanafunzi darasani kutokana na uchache wa madarasa katika shule yao. 

Hadi sasa darasa analosoma Sarafina (10) linasomewa na wanafunzi 162 kwa wakati mmoja ikiwa ni takriban mara nne ya kiwango kinachopendekezwa na Serikali. 

“Darasani tupo wengi sana na madawati nayo hayatoshi. Mimi huwa nakimbilia kukaa mbele ili nimsikie na kumwelewa vyema mwalimu lakini wakati mwingine ukikaa nyuma sana darasani huwezi kumsikia mwalimu na kama haujaelewa basi mpaka umfuate mwalimu tena akuelekeze,” anasema Sarafina.


Sarafina (kulia) akiwa na rafiki yake wakifurahia jambo. Picha|Zahara Tunda.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Inyala, Generosa Samira anasema huwa ni vigumu kwa mwalimu kumfuata mtoto alipo darasani ili aweze kumwangalia anaandika nini kutokana na uwingi wao. 

“Unakuta wanafunzi hawaandiki lakini utamtembeleaje alipokaa wakati  anakaa mwisho na wanakuwa wengi hata hakuna kwa kupita darasani,” anasema Mwalimu Samira.

Idadi ya wanafunzi katika shule hii ni kubwa kiasi cha kufanya uongozi wa shule hiyo uombe vyumba vitano vya madarasa kutoka shule jirani ya Ikuti ili kuhakikisha wanafunzi wote wanapata fursa ya kusoma. 

Inyala iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya ina vyumba vya madarasa saba ikiwa na wanafunzi 1,355 wa darasa la kwanza hadi la saba. Idadi hiyo ya wanafunzi inafanya darasa moja libebe wastani wa wanafunzi 193 ikiwa ni zaidi ya mara nne ya kiwango kinachopendekezwa. Darasa la Chekechea lina wanafunzi 216 wanaosoma kwa wakati mmoja. Serikali inapendekeza darasa moja litumike na wanafunzi wasiozidi 45.

Shida wanazopata wanafunzi na walimu wa shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2003 ni matokeo ya mgogoro wa ardhi ulioibuka kati ya wanakijiji na Serikali. Wakazi wa eneo ilipo shule hiyo wanadai fidia ili waweze kuachia ardhi kwa shule kwa ajili ya kuongeza madarasa.

Shule imezungukwa na mashamba ya mahindi ya watu binafsi kiasi cha kubana nafasi ya kuendeleza ujenzi zaidi. Mashamba hayo yamekaribiana kabisa na darasa la awali ambao hukaa watoto wadogo wanaoanza safari yao ya kielimu.

“Changamoto tunayoipata ni kwamba wanafunzi huwa wanatoroka na kukimbilia vichakani jambo linalowafanya wawe hatarini pia kufanyiwa vitendo vibaya,” anasema Mwalimu Augustino Alpha wa shule hiyo.

Wanafunzi wa darasa la sita wa Shule ya Msingi Inyala  wakiwa darasani hivi karibuni. Picha| Zahara Tunda.

Wamiliki wa mashamba hayo wanasema hawawezi kuachia mashamba hayo mpaka walipwe.

Baadhi wameiambia Nukta kuwa walifanyiwa tathimini ya kulipwa tangu mwaka 2002 lakini mpaka leo hakuna jitihada zozote zilizofanyika kuwalipa madeni yao.

Hata hivyo, wakitaka kujenga wanaambiwa eneo hilo ni la shule licha ya kuwa hawajalipwa jambo lililowafanya waendelee kulima karibu na eneo la shule hadi sasa.

“Kutokana na kutolipa fidia tumewaachia walipojenga shule tu huku tukiendelea kuwadai fidia yetu lakini juu ya shule huku ni mashamba ambayo wananchi tumebaki nayo mpaka pale fidia itakapolipwa,” anasema mmoja wa wamiliki wa mashamba hayo Jafari Hazron.

Mratibu wa Elimu Kata ya Iyunga Cecilia Kakela anasema; “licha ya mimi kuwa mgeni hapa lakini hii kesi hadi mkurugenzi anaifahamu. Jiji ndo linatakiwa lilipe na sisi hatuwezi kufanya chochote pale mpaka walipwe.” 

Jitihada za Nukta kumpata Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya kueleza namna ya kutatua mgogoro huo zimefua dafu baada ya kukosa fursa ya kuonana naye ofisini kwake na hata baada ya kupigiwa simu mara kadhaa hakuweza kupokea.


Zaidi: Njia rahisi kwa wazazi, wanafunzi kujua matokeo ya shule za sekondari. Soma Elimu Yangu


Wakati wanafunzi wa shule za msingi za watu binafsi wakikaa kwenye darasa moja lisilozidi wastani wa wanafunzi 45 hadi 50 hali ni tofauti katika baadhi ya shule za msingi katika jiji hilo ambapo darasa moja wanakaa wanafunzi zaidi ya 120.

Sehemu kubwa ya shule za msingi za umma ambazo Nukta ilizitembelea katikati ya mwezi Mei zilikuwa na wanafunzi wengi kuzidi wastani unaotakiwa na Serikali. 

“Wanafunzi tunao wengi lakini vyumba vya madarasa ni vichache. Uchache huo unafanya hata yale madarasa ambayo hayana madirisha wanafunzi wa  darasa la tatu ambao wapo 135 na wa darasa la nne ambao ni 108 wanayasomea,” anasema Mashaka John, Mwalimu mkuu shule ya Msingi Jitegemee iliyopo katika kata ya Nzovwe jijini hapo.

Mbali ya uhaba wa madarasa bado kuna changamoto ya ukosefu wa sakafu bora, madawati pamoja na nyavu madirishani katika madarasa ya shule ya msingi Jitegemee.

Moja ya darasa linalotumika na wanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Jitegemee. Picha| Zahara Tunda.

Utekelezaji wa sera ya elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne ulioanza rasmi mwaka 2016 baada ya Serikali ya awamu ya nne kuingia madarakani uliwapa hamasa wazazi wengi kuwapeleka watoto wao shule ili wapate fursa ya elimu.

Kasi ya kuongezeka kwa wanafunzi haijaendana na uwekezaji wa miundombinu na kufanya shule nyingi kuwa na mwanya mkubwa wa miundombinu ili kukidhi mahitaji.

Wadau wanaeleza kuwa licha ya kuwa ni jukumu la Serikali katika ujenzi wa miundombinu bado wadau wengine wa elimu hasa wazazi hawana budi kuchangia kwa kiwango kikubwa ili kutengeneza mazingira rafiki ya kujisomea katika shule za msing nchini.

Katika kata ya Iyela, wazazi walijitolea kuchangia na sasa wanaendelea na ujenzi wa madarasa ili kuhakikisha kuwa watoto wao wanasoma vyema ndani ya muda mfupi.

        Moja ya vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Iyela vinavyojengwa kwa michango ya wazazi wa kata ya Iyela jijini Mbeya.

Ukosefu wa vyumba vya madarasa na miundombinu mingine katika shule za msingi katika jiji la Mbeya si wa kupuuza. 

Shule ya Msingi Iyunga iliyopo Kata ya Iwambi licha ya ukongwe bado inakabiliwa na changamoto lukuki zikiwemo madawati, vyoo, na umeme. 

Pia, mazingira ndani ya baadhi ya madarasa yake siyo rafiki kiasi cha kumkosesha mwanafunzi fursa ya kuelewa zaidi akiwa darasani.

      Darasa katika shule ya  msingi  Iyunga ambalo linahitaji matengenezo ili liweze kutumika na wanafunzi. Picha zote|Zahara Tunda

Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1975 ina vyumba vya madarasa 16 lakini ni  vyumba tisa tu hutumika kutokana na baadhi kuwa chakavu jambo linalosababisha wanafunzi wengi kuwepo katika darasa moja. 

Wadau wajitosa kuokoa jahazi

Hata wakati baadhi ya viongozi na wananchi wakisubiri bajeti ya Serikali ili kuwajengea miundombinu wapo baadhi waliojitoa kuchangia fedha na nguvu ngazi ili wanafunzi kama Given wafanikishe ndoto zao za kitaaluma.

Diwani wa kata ya Iwambi Humphrey Ngalawa anasema mbali na kulisukuma suala hilo katika baraza la madiwani ili Serikali itatue aliamua kuchangia ukarabati wa madarasa mawili ya darasa la kwanza na darasa la saba. 

“Hata umeme nimetafuta wadau binafsi na tumeanza kusuka nyaya za umeme na tumetenga fedha ili tuweke umeme katika shule ya msingi  Iyunga,” anasema. 

Hata hivyo, uchangiaji wa ujenzi wa miundombinu katika shule hiyo siyo rahisi kutokana na uelewa hafifu kwa wazazi hasa baada ya Serikali kutangaza kutoa elimu bure. Wazazi wa eneo hilo wanaeleza kuwa hawawajibiki na uchangiaji kwa kuwa Serikali imekataza michango.

Diwani Ngalawa anaeleza licha ya kuwepo vikwazo hivyo bado wanajitahidi kushawishi watu na anatoa wito kwa wadau wengine wachangie ili waweze kusaidia shule kuwa na miundombinu inayotakiwa.

Serikali inasemaje?

Licha ya changamoto hizi za madarasa bado Serikali ina nafasi kubwa ya kuweka wazi na kutoa elimu kuhusu elimu bure ili iweze kuwapa rai wananchi waweze kuchangia katika sekta ya elimu.

“Halmashauri inatenga bajeti, kulingana na uwezo ambao uliopo kwa mwaka huo wa fedha, fedha hizo zikiletwa zinaelekezwa katika kujenga vyumba hivyo vya madarasa, vyoo na miundombinu mengine shuleni,” anasema Paulina Ndigeza Afisa elimu mkoa wa Mbeya.

Ndigeza anasema Serikali ina sehemu yake ya kufanya lakini  jamii pia ina sehemu yake kwa kuwa waraka wa elimu namba 3 wa mwaka 2016 umeweka wazi jamii kutumia nguvu zake kuboresha miundombinu na mahitaji mengine ya shule.