Mgonjwa mwingine wa Corona agundulika Tanzania
Mgonjwa mwingine mmoja wa virusi vya Corona (Covid-19) amegundulika leo jijini Dar es Salaam na kuongeza idadi ya walioambukizwa ugonjwa huo Tanzania hadi 25 tangu ulipoingia nchini katikati ya Machi 2020.
- Mgonjwa huyo mwanaume (51) raia Tanzania amethibitishwa leo
- Anaongeza idadi ya wagonjwa wa Covid-19 kufikia 25 huku zaidi ya nusu wakitokea Dar.
Dar es Salaam. Mgonjwa mwingine mmoja wa virusi vya Corona (Covid-19) amegundulika leo jijini Dar es Salaam na kuongeza idadi ya walioambukizwa ugonjwa huo Tanzania hadi 25 tangu ulipoingia nchini katikati ya Machi 2020.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameeleza katika taarifa yake leo (Aprili 7, 2020) kuwa mgonjwa huyo mpya ni mwanaume (51) raia wa Tanzania.
“Mgonjwa yuko chini ya uangalizi wa watoa huduma za afya katika kituo maalum cha tiba Dar es Salaam,” amesema Ummy katika taarifa hiyo.
Mgonjwa huyo mpya wa Covid-19 anaifanya Dar es Salaam kuwa na wagonjwa 14 ambao ni zaidi ya nusu ya wagonjwa wote walioripotiwa nchini.
Amesema wizara yake inaendelea kufuatilia watu wa katibu waliowahi kukutana na mgonjwa huyo na wengine 789 waliokutana na wagonjwa wa Corona.
Zinazohusiana:
Aidha, kuanzia 24 Machi 2020 hadi hadi sasa jumla ya wasafiri 1,181 wamewekwa karantini nchini na kati ya hawa wasafiri 324 wamemaliza siku 14 za uangalizi,” amesema Ummy.
Hata hivyo, wananchi wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari ya kunawa mikono mara kwa mara, kutokugusa pua, mdomo au macho, kutumia tishu wakati wa kukohoa au kupiga chafya na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.