Miaka 55 ya Muungano wa Tanzania inaadhimishwa kwa aina yake
Watanzania wanaitumia siku ya leo kwa kukaa majumbani na kumpuzika na familia zao, hakuna shamrashara za halaiki ya vijana, gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama wala hutuba za viongozi.
- Watanzania na viongozi wanaitumia siku ya leo kwa kukaa majumbani na kumpuzika na familia zao.
- Mwaka huu hakuna shamrashara za halaiki ya vijana, gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama wala hutuba za viongozi.
- Fedha zilizotengwa kwa ajili ya sherehe hiyo kutumika kwa matumizi mengine.
Tofauti ilivyozoeleka kwa sherehe za Muungano wa Zanzibar na Tanzania bara kuadhimishwa kwa shamrashamra mbalimbali, mwaka huu watanzania wanatumia maadhimisho hayo kwa mapumziko wakiwa nyumbani na familia zao.
Sherehe hizo hufanyika Aprili 26 ya kila mwaka ambapo mwaka huu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoundwa na nchi mbili inasherekea miaka 55 tangu kuundwa kwake.
Muungano huo uliasisiwa na marais wawili; Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Sheikh Aman Abeid Karume (Zanzibar) mwaka 1964.
Utaratibu wa kusheherekea Muungano mwaka huu ulitangazwa jana (Aprili 25, 2019) jijini Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambapo amesema leo ni siku ya mapumziko na hakutakuwa na shamrashamra za sherehe zilizoeleka miaka iliyopita.
Wakati watanzania wakipumzika nyumbani, Rais John Magufuli ametoa msamaha kwa baadhi ya wafungwa na anaendelea na ziara yake ya siku nane katika mkoa wa Mbeya ambapo Mei Mosi atakuwa mgeni rasmi katika siku ya wafanyakazi ambayo kitaifa itafanyika mkoani humo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Jacob Kingu, Rais John Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa 3,530 ambapo wafungwa 722 wataachiliwa huru leo April 26, 2019 na waliobaki watamalizia sehemu ya kifungo kilichobaki baada ya kupewa msamaha huu.
Soma zaidi:
Utofauti uko wapi?
Ilizoeleka kuona sherehe hizo zikifana kwa kufanyika katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kupambwa na halaiki ya vijana, mabango na gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama.
Pia Ilikuwa ni fursa ya kusikiliza hotuba za rais kuhusu hatua zilizopigwa kutatua kero za muungano na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi husika.
Muungano huo uliasisiwa na marais wawili; Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Sheikh Aman Abeid Karume (Zanzibar) mwaka 1964. Picha|Mtandao.
Lakini tangu aingie madarakani mwaka 2015, Rais John Magufuli amekuja na utaratibu mpya wa kusheherekea Sherehe za kitaifa ikiwemo kutumia viwanja mbalimbali vilivyopo nchini badala ya kutegemea uwanja wa Uhuru.
Mathalani, mwaka jana maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano wa Tanzania bara na Zanzibar yalifanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.
Mwaka huu, watanzania wamejulishwa kutulia majumbani na kupumzika na familia zao huku fedha zilizopangwa kugharamia sherehe hizo zitatumika kwa matumizi mengine.
“Amesema jumla ya Sh988.9 milioni ambazo zilikuwa zimepangwa kwa ajili ya sherehe hizo, zimeokolewa na zitapangiwa shughuli nyingine,” inasomeka taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu kuahirishwa kwa sherehe za muungano mwaka huu.
Hiyo nayo ni tofauti nyingine ambapo Serikali ikiahirisha sherehe za kitaifa imekuwa ikiweka wazi matumizi ya fedha husika ikiwemo kujenga miundombinu ya barabara na hospitali lakini mwaka huu haijaweka wazi.
Kwa mfano, Rais John Magufuli alipoahirisha sherehe za uhuru Disemba 9, 2018, aliagiza kiasi cha Sh995.18 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe hizo zitumike katika ujenzi wa hospitali itakayoitwa Uhuru mkoani Dodoma.
Licha ya kuahirisha sherehe hizo, viongozi, watendaji wakishirikiana na wananchi katika maeneo yao walikuwa wakishiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kufanya usafi, kutoa misaada katika vituo vya afya na watoto yatima.
Katika sherehe za Uhuru za mwaka 2015, Rais John Magufuli aliahirisha sherehe hizo badala yake aliwaongoza watanzania kote nchini kutumia siku ya maadhimisho ya sherehe za Uhuru wa Tanganyika kufanya usafi katika maeneo ya soko la Feri jijini Dar es Salaam.
Lakini mwaka huu umekuwa wa tofauti. Maadhimisho ya miaka 56 ya Muungano ya mwaka 2020 wakati nchi inajiandaa katika uchaguzi mkuu yatakuja na mtindo upi?