October 6, 2024

Mifumo inayoweza kukusaidia kutumia pesa ukiwa safarini

Mifumo hiyo ni pamoja na matumizi ya kadi za malipo, kadi za benki na hundi.

  • Mifumo hiyo ni pamoja na matumizi ya kadi za malipo, kadi za benki na hundi.
  • Lakini utashi wa kutumia pesa utakavyo kinabaki katik uwezo wako.

Dunia ina tamaduni, makabila, lugha, pesa na  vyakula vya aina mbalimbali. Yote hayo hutumika kuwatofautisha na kuwaunganisha watu kwa shughuli mbalimbali. 

Wakati ukisafiri katika maeneo mbalimbali duniani hutaepuka kutumia pesa. Zinaweza kuwa pesa taslimu, kadi za malipo (Credit cards) au kwa njia ya simu za mkononi. 

Lakini safari yako itakua na maana kama pesa zitatumika vizuri kulingana na mahitaji yako. Unawezaje kudhibiti matumizi ya pesa wakati wa safari? Jaribu mbinu hizi:

Fanya malipo kwa fedha za kigeni

Kama umesafiri nje ya nchi, ni vema kutumia pesa zinazotambulika kirahisi kimataifa ikiwemo dola ya Marekani, Paundi ya Uingereza. Malipo hayo yanaweza kukusaidia kuepuka makato makubwa kwa kutumia pesa ya nchi yako. 

Kabla ya kufanya malipo ya huduma au bidhaa katika nchi ya kigeni tathmini ni aina gani pesa inayokufaa kwa malipo.

Iambie benki yako kuwa unasafiri

Kama unatumia kadi ya malipo (credit card) ni vema uitaarifu benki yako kama unatoka nje ya nchi ili kuiwezesha kadi yako kutumika mahali popote uendapo. 

Hii itakurahisishia na kukuepushia usumbufu wa kukosa huduma ikiwa kadi yako haijaunganishwa na mifumo ya kimataifa ya malipo. 


Zinazohusiana:


Beba kadi ya kutolea pesa kwenye mashine (ATM Card)

Hakikisha kadi yako ya ATM imeunganishwa na mifumo ya kimataifa ili kukuwezesha kutoa pesa kwenye mashine ya ATM popote duniani. Hii ni njia nzuri kwa sababu inakuhakikishia usalama wa pesa zako na kukuepusha na usumbufu wa kubeba pesa nyingi mfukoni. 

Mashine za ATM zinakubali kadi kutoka benki za nchi mbalimbali duniani lakini ni vema kujiridhisha utendaji wake katika eneo unalokwenda na kiasi cha fedha utakachokatwa ili kupata huduma hiyo ya kutoa pesa.

Badili pesa kabla ya kusafiri

Kama utaona inafaa kubeba pesa, ongea na benki yako wakupatie fedha za nchi husika kabla ya kuanza safari.

Lakini utalazimika kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuwa una safiri na kiasi fulani cha pesa nje ya nchi ili kuepuka usumbufu wakati unakaguliwa uwanja wa ndege. 

Pia fuatilia ni kiasi gani cha pesa taslimu unachoruhusiwa kuingia nacho katika nchi unayoenda. 

Pesa inaweza kuharibu au kufanikisha safari yako. Angalia jinsi unavyoitumia. Picha|Mtandao. 

Unaweza kutumia hundi ya benki

Zipo benki ambazo zinakubali hundi kutoka nchi mbalimbali. Kama utaona inafaa na hutaki kutumia kadi ya malipo au ATM. Unaweza kubeba hundi na ukifika unakokwenda ukaenda katika benki husika na utapewa pesa taslimu kwa ajili ya matumizi yako. 

Huenda njia hii haitumiki sana kutokana na usalama wake ambapo inaweza kutumia na watu wasio waaminifu. 

Hata hivyo, hizo ni njia wezeshi za kupata pesa lakini utashi wa kutumia pesa unabaki katika uwezo na maamuzi yako.