October 6, 2024

Mifumo thabiti kuboresha maisha ya wafanyakazi Tanzania

Serikali imewataka waajiri kote nchini kuweka mifumo madhubuti ya usalama mahala pa kazi ili kuwakinga wafanyakazi na kuwalinda na hatari zinazoweza kutokea wanapotekeleza majukumu yao ya kazi.

  • Ni mifumo inayoweka mazingira salama ya kufanyia kazi.
  • Mishahara mizuri na mafao kuwalinda wafanyakazi Tanzania.

Mwanza. Serikali imewataka waajiri kote nchini kuweka mifumo madhubuti ya usalama mahala pa kazi ili kuwakinga wafanyakazi na kuwalinda na hatari zinazoweza kutokea wanapotekeleza majukumu yao ya kazi.

Kauli hiyo imetolewa leo Aprili 27, 2021 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu  Kazi, Sera, Bunge, Ajira na Vijana,  Patrobas Katambi wakati akizungumza jijini Mwanza kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya usalama mahala pa kazi ambayo huadhimishwa kila mwaka  ifikapo April 28.

Katika hotuba yake waziri huyo  amesema waajiri wanatakiwa kuweka mifumo madhubuti ya ufanyaji kazi kwa wafanyakazi wao maeneo wanayofanyia kazi yawe salama. 

“Haiwezekani mfanyakazi halipwi mshahara miezi 13, tisa hadi nane wakati huo mfanyakazi huyo ndiye analinda mitambo na shughuli zingine hali inayochangia wengi kuwaibia waajiri wao,” amesema Katambi.

Waziri huyo ameagiza waajiri hao kuhakikisha wanapeleka michango ya  wafanyakazi wao katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili wanapofikia umri wa kusataafu wapate mafao yao kwa wakati  na si vinginevyo.


Soma zaidi: 


Agizo hilo lilipokelewa na Kaimu Mtendaji Mkuu Wakala wa Usalama na Afya mahala pa kazi (OSHA), Khadija Mwenda amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wafanyakazi  ili kulinda haki zao.

Khadija pia ameeleza kuwa wameondoa tozo ya elimu kwa umma tofauti na ilivyokuwa awali ambapo walilazimika kuwatoza kiasi cha sh50,000.

Amesema serikali imebakisha tozo ya kufanya uchunguzi wa ajali kazini ambapo pia imeshusha kutoka Sh500,000 ya awali hadi kufikia Sh120,000.

Mwaka huu OSHA inatarajia kufanya utafiti kwa waajiri kuona namna wanavyotengeneza misingi inayowaepushia ajali wafanyakazi wao.

Amesema takwimu zinaonyesha kuwa sekta zinazoongoza kwa wafanayakazi kupata ajali ni uzalishaji na ujenzi huku rika linaloongoza kwa ajali hizo ni umri wa miaka 18 hadi 35.