Mikakati inayoweza kuwasaidia vijana kuepuka ukosefu wa ajira
Takwimu mpya kutoka Sekretarieti ya ajira ya utumishi wa umma zinabainisha kuwa ni mtu mmoja tu kati ya waombaji 100 alifanikiwa kupata ajira.
Wahitimu nao wanapaswa kubadilika kimtazamo na kuacha kusubiri ajira za Serikali badala yake wageukie shughuli zinazoweza kuwahakikishia upatikanaji wa kipato. Picha|JamiiForums.
- Kuna kila sababu ya kupitiwa upya kwa mfumo wa elimu unaowandaa wahitimu kuingia kazini ili kuepuka makosa yanayojitokeza wakati wa maombi ya kazi na kuwaandaa kisaikolojia kujiajiri wenyewe.
- Wachambuzi hao wamesema ushindani wa soko ajira inaweza kuwa sababu kwa baadhi yao kutumia vyeti vya kughushi kupata mpenyo wa ajira.
- Vijana washauriwa kujiajiri ili kuepuka usumbufu unaotokea wakati wa kufuatilia ajira za Serikali.
Dar es Salaam. Wachambuzi wa masuala ya ajira nchini wamesema kuna kila sababu ya kupitiwa upya kwa mfumo wa elimu unaowandaa wahitimu kuingia kazini ili kuepuka makosa yanayojitokeza wakati wa maombi ya kazi na kuwaandaa kisaikolojia kujiajiri wenyewe.
Maoni hayo yanakuja ikiwa imepita siku moja baada ya Sekretarieti ya Ajira ya Utumishi wa Umma (PSRS) kutangaza kuwa asilimia 98.9 ya watu walioomba ajira serikalini hawakufanikiwa kupata ajira hizo kwa miaka mitatu iliyopita kwa sababu mbalimbali huku waombaji 706 wakiwasilisha vyeti feki.
Katibu wa Sekretarieti hiyo, Xavier Daudi alieleza Desemba 17 kuwa Watanzania 594,300 walioomba ajira serikalini hadi Desemba 15 mwaka huu lakini ni waombaji 140,000 pekee waliitwa kwenye usaili kwa ajili ya kujaza nafasi 6,554 zilizotangazwa.
Kiwango hicho cha walioitwa kwenye usaili ni takriban robo tu au asilimia 23.5 ya waombaji wote huku nafasi za ajira zikiwa ni asilimia 1.1 tu ya maombi katika sekretarieti hiyo.
“Tangu Serikali iingie madarakani Sekretarieti ya Ajira imetangaza nafasi za kazi 6,554 kwa ajili ya wizara, idara, wakala, sekretarieti za mikoa, manispaa, halmashauri na taasisi mbalimbali za elimu.
“Hadi kufikia Desemba 15, 2018 nafasi wazi za kazi 6,099 zilishajazwa na nafasi 455 zilizotangazwa kati ya Novemba na Desemba 2018 mchakato wake unaendelea na unatarajiwa kukamilika hivi karibuni,” Daud aliwaambia wanahabari.
Takwimu hizo za sekritarieti ya ajira zinaibua maswali lukuki yakiwemo ufinyu wa fursa za ajira nchini na uwezo wa waombaji wa nafasi mbalimbali za kazi hizo katika kuwavutia waajiri.
Baadhi ya wataalamu wa masuala ya ajira na elimu nchini wameeleza kuwa hali hiyo ni matokeo ya mfumo dhaifu wa elimu kuanzia ngazi ya chini na vijana kushindwa kujiongeza katika kuboresha maarifa na ujuzi unaotakiwa katika soko la ajira.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Ekihya, Lilian Madeje amesema hashangazwi na idadi kubwa ya waombaji kukosa ajira serikalini na sekta binafsi kwa sababu ushindani umeongezeka na nafasi za kazi ni chache kukidhi mahitaji yote ya waombaji.
“Hali hii inamaanisha kuna watu wengi zaidi waliomaliza vyuo ambao wanatafuta kazi na kwa bahati mbaya nafasi za ajira serikalini na kwenye sekta binafsi hazitoshelezi mahitaji yao,” amesema Madeje.
Kutokana na ushindani uliopo, Madeje amesema inaweza kuwa ndiyo sababu inayowasukuma baadhi ya waombaji kutumia vyeti feki au visivyo vyao ili kutafuta mpenyo wa kuonekana kuwa wana sifa zinazohitajika katika kazi husika.
Sambamba na hilo ni kuwepo kwa mianya katika mifumo inayosimamia uhakiki wa vyeti na uelewa mdogo wa wahitimu kuhusu vigezo na sifa za kuomba kazi katika taasisi mbalimbali.
“Watu wengi wana uchu wa kuingia kazini kwa namna moja ama nyingine hawajaweza kutimiza zile requirement (mahitaji) zote,” amesema Madeje ambaye kampuni anayosimamia hujishughulisha na kuajiri wafanyakazi kwa niaba ya mashirika mbalimbali nchini.
Zinazohusiana:
- Fursa za mikopo, soko kuwanufaisha wakulima wa miwa Mbigiri
- Wahitimu vyuo vikuu wakumbushwa kuchangamkia fedha za halmashauri
- Vijana waanika fursa zilizojificha katika matumizi ya mitandao ya kijamii
Hata hivyo, vijana wametakiwa kuangalia fursa nyingine za kujiajiri na kuwa huru kufanya shughuli za ujasirimali ambazo zitawasaidia kuinuana kuliko kusubiri ajira za serikalini ambazo hazitoshelezi mahitaji yao ikizingatiwa kuwa idadi ya wahitimu wa vyuo vikuu inaongezeka kila mwaka.
“Wanatakiwa wajiongeze, wajiajiri wenyewe kwa aina moja au nyingine ikiwemo kuanzisha biashara yako mwenyewe ambayo inaweza kuajiri watu wengi ili kuongeza ajira zaidi,” amesema Madeje.
Chama cha Waajiri Afrika Mashariki (EAEO) kinaeleza kuwa kila mwaka zaidi ya vijana 60,000 wanahitimu vyuo vikuu katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) huku nusu ya wahitimu hao wakiwa hawana vigezo vya kuajiriwa.
Wahadhili wa vyuo vikuu wamesema kuna haja ya kupitia upya mitaala ya elimu tangu ngazi ya shule za msingi ili iendane na mabadiliko yanayotokea katika soko la ajira ambalo linahitaji vijana wenye ujuzi na maarifa ya kutosha kutimiza majukumu wanayokabidhiwa katika jamii.
Mhadhili kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam (TUDARCO), Richard Ngaiza amesema mitaala hiyo ni muhimu ikalenga kuwajengea uwezo wa kivitendo wanafunzi na kuwafunza kuzingatia maadili ya kazi ili kuongeza ushindani katika soko la ajira.
Amebainisha kuwa wahitimu nao wanapaswa kubadilika kimtazamo na kuacha kusubiri ajira za Serikali badala yake wageukie shughuli zinazoweza kuwahakikishia upatikanaji wa kipato.