November 24, 2024

Mikakati itakayowasaidia wanafunzi waliofeli kidato cha nne 2019

Siku mbili baada ya Baraza la Mtihani la Taifa (Necta) kutangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ya mwaka 2019, wadau wa masuala ya elimu wameeleza mambo mambo yanayotakiwa kufanywa ili kuongeza ufaulu na kuwasaidia watahiniwa waliofeli kutumiza ndoto

  • Hali ya kushindwa kupenda katika mitihani hii ya kidato cha nne haimaanishi wamefeli kila kitu.
  • Ni jukumu la wanafunzi kuelewa na kujiandaa kisaikolojia na maisha mengine.

Dar es Salaam. Siku mbili baada ya Baraza la Mtihani la Taifa (Necta) kutangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ya mwaka 2019, wadau wa masuala ya elimu wameeleza mambo mambo yanayotakiwa kufanywa ili kuongeza ufaulu na kuwasaidia watahiniwa waliofeli kutumiza ndoto zao. 

Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa na Necta, ufaulu wa jumla umeongezeka kidogo kwa asilimia 1.4 kutoka ule wa mwaka 2018 huku watahiniwa 81,808 sawa na asilimia 19.4 wamepata daraja sifuri au wamefeli kabisa na hawatapa vyeti.

Kundi kubwa la watahiniwa limepata daraja la nne ambalo huwa ni vigumu kidogo kuchaguliwa moja kwa moja kwenda kidato cha tano. Wanafunzi 205,613 au sawa na asilimia 48.6 ya watahiniwa wote wa kidato cha nne mwaka jana wamepata daraja hilo la nne.

Kutokana na matokeo hayo ambayo idadi kubwa ya watahiniwa wameangukia daraja la IV na 0 ambayo kwa sasa ni gumzo nchini Tanzania, wachambuzi wa masuala ya elimu walioongea na  www.nukta.co.tz wamesema walioferi hawapaswi kukataa tamaa na kuona kama ndiyo mwisho wa safari yao kielimu.

Mwandishi mashuhuri wa vitabu na mdau wa elimu,  Richard Mabala ameiambia Nukta kuwa kufaulu na kwenda kidato cha tano kisha chuo siyo njia pekee ya kufanikiwa kimaisha.

Mabala ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi ya HakiElimu amesema wanafunzi hawatabahatika kwenda kidato cha tano wanaweza kusoma kozi zinazoweza kuwaongezea stadi za maisha ambazo ni muhimu katika kuajiriwa au kujiajiri.

Baadhi ya taasisi ambazo zinatoa kozi za muda mfupi na mrefu kwa watu kada tofauti hata wale ambao wamefeli kidato cha nne ni pamoja na Mamlaka ya Ufundi Stadi Veta (VETA) na ikamsaidia kufanikiwa kimaisha.

“Tusione kwamba kwenda kidato cha 5 na cha 6 ndio njia pekee ya kufanikiwa katika maisha. Kusoma kozi mbalimbali pia ni njia inayoweza kutumika na walioshindwa kufaulu,” amesema Mabala na kuongeza kuwa,

“Kuna umuhimu wa kuwa na vyuo vinavyotoa elimu mchanganiko (Polytechnic) ili kuwasaidia wanafunzi kutokutegemea elimu ya darasani pekee.”

 Mabala amesema ni vema Watanzania wakaondokana na fikra kuwa mafanikio ya elimu yamejikita katika njia moja tu ya kutoka sekondari kwenda chuo kwa sababu yapo mambo mbalimbali anayoweza kufanya mtu ambayo yataongeza thamani katika maisha yake. 

Hata wale ambao itakuwa ni vigumu kupata elimu katika mfumo mwingine wa elimu, wanaweza kuingia katika shughuli za ujasiriamali ambazo wanaweza kuanza kuzifanya baada ya kupata mafunzo yenye gharama ndogo kutoka kwa watu wenye uzoefu wa biashara.

Pia wazazi na walezi wanashauriwa kuwatia moyo watoto wao walioferi na kuangalia fursa nyingine za elimu ambazo wanaweza kuwapatia ikiwemo kugundua na kuviendeleza vipaji vyao ambavyo vinaweza kuwa tunu muhimu kwa wao kuinuka kiuchumi. 


Zinazohusiana


Utoaji elimu uboreshwe kuinua ufaulu wa wanafunzi

Hata wakati njia mbalimbali zikitumika kuwasaidia watahiniwa walioferi katika mtihani huo, wachambuzi wa elimu ambao wameongea na www.nukta.co.tz  wamesema kuna kila sababu kuitazama kwa jicho la tatu elimu ya sekondari hasa inayotolewa katika shule za Serikali.

Mdau mmoja kutoka Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema huenda hata wale wenye ufaulu mzuri wanaweza kuwa bado hawajapata maarifa na ujuzi wa kutosha kuwawezesha kukabiliana na changamoto za maisha. 

Amebainisha kuwa zipo shule ambazo zinashindana kufaulisha wanafunzi wengi kwa kuwakaririsha masomo pasipo kutathmini kama wamepata maarifa na ujuzi unaohitajika katika safari yao ya elimu.

“Tutapata wahitimu wengi wasio na taaluma ya kutosha. Hata waliofaulu sana si wote wana uwezo mzuri,” amesema mdau huyo.

Katika kuongeza ufaulu na kupunguza wanafunzi kupata daraja la IV na sifuri, kuna kila sababu ya kujenga msingi mzuri wa kuwaandaa wanafunzi tangu wakiwa shule ya msingi na wanapoingia sekondari. 

Mwalimu kutoka Shule ya Sekondari Nyabulogoya mkoani Mwanza, Godfrey Edward,ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) moja kati ya sababu kubwa za kufeli kwa wanafunzi wengi ni msingi wanoojengewa wakiwa kidato cha pili ambao unakuwa si rafiki kufaulu kidato cha nne.

Amesema sababu zingine pamoja na hiyo ni kubweteka kwa watoto kuona kufaulu ni jambo rahisi pasipo kujiandaa, kukosekana kwa ukaribu wa wazazi na mtoto anapokuwa shuleni na kubadilika kwa mfumo utungaji wa maswali kwa wanafunzi kuwa wa kujificha tofauti na ule wa mwaka jana.

Hata wale ambao itakuwa ni vigumu kupata elimu katika mfumo mwingine wa elimu, wanaweza kuingia katika shughuli za ujasiriamali ambazo wanaweza kuanza kuzifanya baada ya kupata mafunzo yenye gharama ndogo kutoka kwa watu wenye uzoefu wa biashara. Picha|Morocco Jewish Times.

Nini kifanyike?

Godfrey amesema ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi, alama za ufaulu wanapoingia sekondari zitiliwe mkazo ili kuboresha hali iliyotokea mwaka jana.

“Passmark  (Alama za ufaulu) hasa za kidato cha pili zitiliwe mkazo. Waje watu walioiva kwa ajili ya kuendelea na hatua nyingine.” amesema Godfrey.

Godfrey ameongeza kwamba panapotokea mabadiliko yoyote ya utungaji wa mitihani kwa wanafunzi, taarifa zitolewe mapema ili wanafunzi wapate muda wa kujiandaa na mabadiliko hayo.

Mabala naye anaungana na wadau wengi na kusema uboreshaji wa miundombinu na nyenzo za kufundishia na kujifunzia nao unatakiwa utiliwe mkazo hasa katika shule za Serikali.