October 6, 2024

Mipango endelevu inavyoweza kuipa uhai miradi ya umemejua Tanzania

Ni lazima kujua ufanisi na ubora wa vifaa vyote vitakavyofungwa kwenye mradi husika, uimara na kudumu kwake.

  • Kutokuwepo kwa mipango endelevu kunachangia kupunguza utendaji kazi wa mifumo ya umemejua.
  • Ni lazima kujua ufanisi na ubora wa vifaa vyote vitakavyofungwa kwenye mradi husika, uimara na kudumu kwake.
  • Kila mradi uteue watu watakaosimamia matumizi bora, endelevu na matengenezo ya mifumo ya umemejua katika halmashauri.

Pamoja na jitihada zote zinazofanyika ulimwenguni kuhakikisha watu wote wanafikiwa na huduma za umeme ifikapo mwaka 2030, zikichagizwa na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG’s), bado Waafrika 600 milioni wanakadiriwa watakosa huduma za umeme itakapofika mwaka 2030.

Pia inakadiriwa kwamba watu 1.6 bilioni duniani kote hawajafikiwa na huduma za umeme.

Hivyo basi, kuhakikisha tunafikia malengo ya nishati kwa wote hapo mwaka 2030, teknolojia mbalimbali za nishati jadidifu zinaendelea kupewa msukumo mahali pote ulimwenguni. 

Hapa kwetu Tanzania, Sera ya Nishati ya Mwaka 2015 imetamka bayana kwamba teknolojia za nishati jadidifu zinatambulika na zinapewa msukumo kuhakikisha kuwa zinachangia katika kuwafikishia wananchi hasa wa vijijini huduma za nishati na umeme.

Ni kwa sababu hiyo basi, kumekuwepo na miradi mbalimbali ya nishati jadidifu, hasa nishati ya jua katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwa ni hatua ya kuziba pengo la upatikanaji wa nishati nchini.  

Kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati ya mwaka 2019/20,  inakadiriwa kuwa, jumla ya megawati 26 za mifumo midogo ya umemejua (Stand Alone Solar Systems) zimefungwa nchini kote hadi Mei, 2019. 

Kumekuwepo pia miradi kadhaa ya kuweka umemejua kwenye vituo vya kijamii (public facilities) hususani vituo vya afya na zahanati, shule, vituo vya polisi pamoja na kuweka taa za mitaani na barabarani (Solar Street Lights) katika Halmashauri, Manispaa na Miji mbalimbali hapa nchini. 

Mfano mzuri ni mradi wa “Sustainable Solar PV Market Package” (SSMP I and II) ambao kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na kusimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambapo sekta binafsi ilishirikishwa katika kuweka mifumo ya umemejua katika vituo vya afya, zahanati, shule, vituo vya polisi katika maeneo ya vijijini yasiyofikiwa na umeme wa gridi katika wilaya za Sumbawanga, Tunduru, Namtumbo, Biharamulo, Kasulu, Kibondo, Chato, Sikonge na Bukombe, mwaka 2007 na 2013. 


Zinazohusiana: 


Pia, kwa sasa miradi ya taa za umemejua za mitaani na barabarani (solar street lights) inaendelea hapa nchini kupitia miradi ya kuboresha miundombinu katika manispaa na halmashauri mbalimbali.

Katika jiji la Dar es salaam kupitia mradi wa Dar es Salaam Metropolitan Development Project (DMDP), taa za umemejua za barabarani na mitaani zinaendelea kufungwa katika manispaa zote tatu za Kinondoni, Ilala na Temeke kwenye barabara muhimu za pembezoni zinazorekebishwa kuwa katika kiwango cha lami.

Hata hivyo, kukosekana kwa mipango thabiti ya huduma baada ya mifumo hii kufungwa (After sale support) pamoja na matengenezo endelevu (Progressive Maintenance) kunatishia uendelevu wa miradi hii muhimu. 

Mifumo ya Umemejua inaweza tu kuwa bora na endelevu endapo vifaa bora vyenye viwango sahihi vitafungwa ipasavyo na mafundi wenye ujuzi sahihi wa ufungaji pamoja na kuwepo kwa mipango endelevu ya matumizi na matengenezo ya mifumo husika (Operation and Maintenance).

Katika matokeo ya utafiti iliyofanywa na Watafiti Christopher Mgonja na Hassan Said ulioangazia ufanisi wa mifumo ya memejua iliyofungwa katika Mradi wa SSMP I wilayani Sumbawanga imethibitishwa kuwa ufanisi endelevu wa mifumo ya umemejua una uhusiano wa moja kwa moja na kuwepo kwa mipango endelevu ya matengenezo.

Kutokuwepo kwa mipango hiyo kunachangia kupunguza utendaji kazi wa mifumo ya umemejua na hivyo kufanya kazi kwa kipindi kifupi, tofauti na utendaji kazi wa miaka zaidi ya 25 unaotarajiwa.

Utafiti huo uliochapishwa katika Jarida la International Journal of Mechanical Engineering and Technology, unapendekeza kuwepo kwa mipango endelevu ya matumizi na matengenezo tangu awali kabisa wakati miradi hii inabuniwa. 

Kudumu kwa miradi ya umemejua kunategemea zaidi mipango endelevu ya matengenezo inayosimamiwa na wataalam waliobobea. Picha|Mtandao. 

Ni lazima kujua ufanisi na ubora wa vifaa vyote vitakavyofungwa kwenye mradi husika, uimara na kudumu kwake, ni wakati gani vitahitaji matengenezo ama kubadilishwa, kutenga utaratibu na fedha kwa ajili ya matengenezo na kuandaa mipango ya mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa watumiaji na wahudumiaji wa miradi hii, watakaotoa huduma baada ya ufungaji pamoja na matengenezo. 

Watafiti hao wanapendekeza kuhakikisha kila mradi unateua mtu au watu watakaosimamia matumizi bora na endelevu pamoja na matengenezo ya mifumo ya umemejua katika halmashauri zenye miradi.

Ni vizuri wahisani, wafadhili na watunga sera kwenye eneo la nishati kuzingatia suala zima la matumizi na matengenezo endelevu katika kila mradi wa nishati jadidifu wanaohusika kufadhili ama kusaidia ili kuifanya miradi hii kuwa endelevu na kuleta manufaa yanayokusudiwa.

Prosper Magali ni Mtaalamu wa Nishati Jadidifu mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 17, ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Nishati Jadidifu (Tanzania Renewable Energy Association) na mmoja wa wakurugenzi wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa ya Alliance for Rural Electrification yenye Makao yake Makuu Brussels, Ubelgiji na pia Mkurugenzi wa Miradi na Ubunifu wa Kampuni ya Ensol Tanzania Ltd, waendelezaji miradi ya nishati jadidifu wa hapa Tanzania. Makala hii ni maoni yake binafsi.