November 24, 2024

Misingi ya kuvuta wateja katika biashara yako

Kwenye biashara hamna kutegemea bahati, lazima ujenge msingi wa kuwa na wateja ambao watanunua bidhaa zako.

  • Bainisha aina ya wateja unaotaka kuwahudumia.
  • Jenga mahusiano mazuri na wateja wako.
  • Tumia lugha yenye staha na inayoeleweka kwa wateja.

Siku zote tunaamini kwamba yeyote anayeanzisha biashara basi huwa na malengo ya kutengeneza faida lakini pia hata kutoa huduma kwa wateja wake. 

Lakini swali ambalo kila mfanyabiashara hulifikiria zaidi ni je nitapata wateja?.

Cha kuzingatia ni kuwa, katika suala la kupata wateja huwa halitokei popote tu kisha wateja wanaanza kufika kwenye biashara yako la hasha.

Lazima uzingatie misingi na kanuni za kibiashara. Biashara yako inatakiwa kuwa na wateja wa aina gani mfano wewe unauza vyakula mgahawani maana yake wateja wako ni watu wa rika zote isipokuwa watoto wachanga.

Aidha, wewe unafanya biashara ya kuuza sigara tu au pombe maana yake wateja wako wewe watakuwa ni watu wazima wenye umri kuanzia 18 na zaidi, chini ya hapo ni mtoto atakuwa ameagizwa kuja kununua.

Kupitia hiyo mifano ya biashara hapo juu ni dhahiri sasa unafahamu wateja wako na sasa unachotakiwa kujua ni kuwa wateja wako wanajielewa na wanafahamu nini wanakuja kukifanya/kufuata dukani au sehemu yako ya biashara.

Kwenye biashara hamna kutegemea bahati, tunasema mfanyabiashara yule anapata idadi kubwa ya wateja kwasababu ana bahati, hapana. 

Ukweli ni jinsi gani anaishi na wateja wake na jinsi gani hushirikiana nao muda wote. Mfano wafanyabiashara wengi hasa hapa Tanzania wakipata mteja wanamkaribisha vizuri lakini akishatoa pesa yake hawamthamini tena.

Wafanyabiashara wa soko la Masumbwe mkoani Geita wakisubiri wateja kuja kununua bidhaa. Picha| Gift Mijoe.

Upatapo mteja kwenye biashara yako yoyote lazima uweke akilini mwako vitu vifuatavyo, kwanini amekuja kwako?, kesho akitaka bidhaa ataipata wapi na je ameridhika na huduma yako?, kama hajaridhika basi jitahidi kumuhudumia ili atoke kwa furaha na kesho pia aje.

Pia shirikiana naye kuanzia anapoingia na anapotoka hata kama hajanunua kitu huyo bado ni mteja wako. Yafuatayo pia ni mambo ya kuzingatia katika kuvutia wateja wengi zaidi.

Zingatia Matumizi ya lugha

Hapa nazungumzia lugha ya kibiashara kwa sababu biashara yako ina wateja wa aina tofauti tofauti kwa hiyo ni lazima uzingatie lugha ya heshima ilimradi iwe ni lugha ya kukidhi mahitaji yake bila kumbagua au kumkera mtu. 

Mfano unaweza kuhudumia wateja wako kwa lugha ya kabila lako bila kujua ni kikwazo kwa mteja wako mwingine ambaye si wa kabila lako na akajiona kama anabaguliwa mwisho wake kumpoteza.


Imarisha usafi wa eneo la biashara

Wateja wengi hupenda sehemu safi na isiyo na mazingira hatarishi, hapo ndipo utamuona kila siku. Hakikisha eneo la biashara yako ni safi na lenye kuvutia wakati wowote. 

Mfanyabiashara ukizingatia haya yanaweza kuwa chachu ya mabadiliko katika biashara yako sababu idadi ya wateja wa kudumu itaongezeka na wateja wengi zaidi kuendelea kuvutiwa mwisho wa siku unakuwa na mtandao mkubwa wa wateja.