Mkakati wa teknolojia kupambana na Corona wazinduliwa Uswisi
Mkakati huo wa C-TAP utasaidia upatikanaji wa chanjo, matibabu na teknolojia zingine dhidi ya ugonjwa.
- Mkakati huo wa C-TAP utasaidia upatikanaji wa chanjo, matibabu na teknolojia zingine dhidi ya ugonjwa.
- Nchi 30 duniani na taasisi za kimataifa likiwemo Shirika Afya Duniani (WHO) wamejiunga katika mkakati huo.
Nchi 30 duniani na taasisi za kimataifa likiwemo Shirika Afya Duniani (WHO) wamejiunga katika mkakati wa kiteknolojia (C-TAP) ili kuharakisha upatikanaji wa chanjo, matibabu na teknolojia zingine dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona.
C-TAP inalenga kuhakikisha chanjo na matibabu ya Corona yanamfikia kila mtu duniani pasipo kujali hali yake.
Mkakati huo ulipendekezwa kwa mara ya kwanza mwezi Machi na Rais wa Costa Rica Carlos Alvarado ambaye jana amejiunga na Mkurugenzi mkuu wa WHO Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus katika uzinduzi rasmi uliofanyika kwa njia ya video mjini Geneva Uswisi.
Dk Tedros ameyakaribisha makampuni na Serikali ambazo zinatengeneza vifaa tiba ili kuchangia muundo wao katika mkakati huu wa tiba.
“Huu ni wakati ambapo watu wanatakiwa kuweka vipaumbele. Nyenzo za kuzuia, kubaini na kutibu COVID-19 ni masuala muhimu kwa umma ambayo yanahitaji kupatikana kwa wote,” amesema.
C-TAP inatoa fursa ya sehemu moja ambapo patapatikana ujuzi wa kisayansi, takwimu na hati miliki ambavyo vitatumika sawia na jumuiya ya kimataifa katika mapambano ya Corona.
Soma zaidi:
Kamishina Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amesema endapo janga la COVID-19 halitodhibitiwa haraka litaendelea kusambaratisha maisha, biashara na chumi na kutuathiri watu wote kwa njia moja au nyingine.
“Hivyo hebu na tujiunge pamoja kubadilishana takwimu na taarifa, kusongesha mbele uhamishaji wa teknolojia na kupanua wigo wa upatikanaji wa madawa na teknolojia za afya,” amesema Bachelet.
C-TAP inakusudia kuchagiza uvumbuzi wa chanjo, madawa na teknolojia zingine kupitia utafiti ulio wazi wa kisayansi, na kuharakisha uzalishaji kwa kusanya uwezo wa ziada wa wazalishaji.
Hii itasaidia kuhakikisha kuwepo kwa fursa sawa za bidhaa ambazo tayari zipo na mpya za afya za kukabili COVID-19.