November 24, 2024

Mkataba ujenzi reli ya Mtwara-Mbambabay kusainiwa Juni 2019

Serikali imesema tayari imempata mshauri mwelekezi wa kifedha na mkataba wa uwekezaji wa ujenzi wa reli hiyo itakayofungua fursa nyingi za kiuchumi mikoa ya kusini.

  • Serikali imesema tayari imempata mshauri mwelekezi wa kifedha na mkataba  wa uwekezaji wa ujenzi wa reli hiyo itakayofungua fursa nyingi za kiuchumi mikoa ya kusini. 
  • Mshauri mwekezaji atakuwa na jukumu la kuunadi mradi huo kwa wawekezaji mbalimbali. 
  • Mradi huo utatekelezwa kwa ubia wa sekta ya umma na binafsi.

Dar es Salaam. Serikali imesema tayari imempata mshauri mwelekezi wa kifedha na mkataba  wa uwekezaji wa ujenzi wa reli kutoka Mtwara hadi Mbambabay mkoani Ruvuma unatarajiwa kusainiwa Juni mwaka huu. 

Kuanza kwa ujenzi wa reli hiyo itakuwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu Septemba mwaka 2015 akiwa mkoani Mtwara.

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye ametoa ufafanuzi huo leo (Mei 9, 2019) bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia aliyetaka kujua ni lini ujenzi wa reli kutoka Mtwara hadi Bambabay  utaanza kujengwa.

Mhandisi Nditiye amesema mpaka sasa Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa awali (Feasibility and preliminary design) wa ujenzi wa reli kutoka Mtwara mpaka Mbambabay yenye urefu wa kilomita 1,092. 

“Mshauri mwelekezi wa kifedha na uwekezaji (Transaction Adviser) tayari amepatikana, mkataba wa uwekezaji unatarajiwa kusainiwa ifikapo Juni 2019,” amesema Mhandisi Nditiye.

Amebainisha kuwa mshauri mwekezaji atakuwa na jukumu la kuunadi mradi huo kwa wawekezaji mbalimbali ikizingatiwa kuwa mradi huo unatekelezwa kwa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi yaani PPP (Public-Private Partnership). 

Tayari wameanza kupokea maombi ya wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika reli hiyo ambapo wanaelekezwa kufuata sheria na taratibu za ununuzi kwa miradi inayofuata mfumo wa PPP. 

“Taratibu hizo zinawaelekeza kuandaa na kuwasilisha wazo lao yaani proposal na kufanya uwekezaji katika shirika la reli Tanzania (TRC) ambalo nalo litawasilishwa katika wizara yetu (Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano) baada ya kuwa wamejiridhisha,” amesisitiza Nditiye. 


Soma zaidi:


Baada ya wizara kuchambua kwa kina, wazo litawasilishwa katika kitengo cha PPP Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya uchambuzi wao.

Mhandisi Nditiye amesema Wizara ya Fedha na Mipango kupitia kitengo hicho wakimaliza uchambuzi na kuridhia, mwekezaji naye atatakiwa kufanya upembezi yakinifu wa kwake ambao baadaye utalinganishwa na upembevu yakinifu uliofanywa na Serikali kabla ya kukamilisha taratibu za uwekezaji. 

Swali la Ghasia liliulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Nanyamba mkoani Mtwara, Abdallah Chikota.

Kuanza kwa ujenzi wa reli hiyo itakuwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu Septemba mwaka 2015 akiwa mkoani Mtwara. Picha|Mtandao.

Umuhimu wa reli ya Kusini

Ujenzi wa reli kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay unakuja ikiwa imepita miaka zaidi ya 45 baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Reli ya TAZARA  yenye urefu wa kilomita 1,860 ambayo inaunganisha miji ya Dar es Salaam nchini Tanzania na New Kapri Mposhi, Zambia.

Kukamilika kwa ujenzi wa reli ya Kusini kutafungua milango ya fursa mbalimbali zilizopo katika mikoa ya kusini mwa Tanzania ikiwemo utajiri wa mafuta, gesi na madini yaliyoko Mchuchuma na Liganga wilayani Ludewa.

Pia itafungua fursa za maendeleo katika Korido ya Maendeleo Mtwara (MDC) inayohusisha mikoa na kukuza mtandao wa biashara kati ya Tanzania na nchi za Malawi, Msumbiji na Zambia kwa kupunguza gharama za usafirishaji na kuboresha uchumi kwa bidhaa za ndani na nje.