October 7, 2024

Mke wa Museveni hajaambukizwa corona

Msemaji wa wizara ya afya nchini Uganda, Emmanuel Ainebyoona ameiambia NuktaFakti kuwa habari hiyo ni uzushi na inapaswa kupuuzwa.

  • Licha ya ujumbe huo kusambaa kwa kasi tangu Juni 15, siyo ya kweli ni uzushi.
  • Msemaji wa wizara ya afya nchini Uganda, Emmanuel Ainebyoona ameiambia NuktaFakti kuwa habari hiyo ni uzushi na inapaswa kupuuzwa.
  • Amesema Uganda hakuna kiongozi wa juu ambaye amesharipotiwa kuwa na Corona mpaka sasa. 

Dar es Salaam. Kwa kadiri siku zinavyoenda, uzushi dhidi ya viongozi wa juu katika mataifa mbalimbali kuwa wameambukizwa Corona umeendelea kupenyezwa mtandaoni kwa kasi. 

Safari hii habari inayosambaa kwa kasi ni ile inayoeleza kuwa mke wa Rais wa Uganda Mama Janeth Museveni ameambukizwa ugonjwa wa virusi vya Corona.

Ujumbe huo uliopo kwenye picha inayodaiwa kutoka kwenye akaunti ya Twitter ya kituo cha televisheni cha NBS cha Uganda inaeleza kuwa mama huyo mke wa Rais Yoweri Museveni alipata corona baada ya kumaliza kikao cha baraza la mawaziri.

“BREAKING NEWS: The First Lady of Uganda, Janet Kataha Museveni has tested positive for #Covid-19 after Monday’s Cabinet Meeting and has been admitted to Nakasero Hospital. Statehouse Under Emergency Lockdown with the President feared to be isolated in the banker. Developing story,” inasomeka picha hiyo.

Kwa tafsiri isiyo rasmi picha hiyo inaeleza: “HABARI ILIYOTUFIKIA HIVI PUNDE: Mama Janet Kataha Museveni imekutwa na maambukizi ya virusi vya corona (Covid-19) baada ya kushiriki kikao cha baraza la mawaziri na amelazwa katika hospitali ya Nakasero. Kwa sasa Ikulu ipo katika zuio la dharura la watu kutoka nje huku Rais akihofiwa kutengwa katika eneo lenye usaidizi maalum. Habari inayoendelea.”

Licha ya ujumbe huo kusambaa, habari hiyo iliyoanza kusambaa tangu Juni 15, siyo ya kweli ni uzushi.

Kwanini ni uzushi?

Nukta Fakti imebaini kuwa picha hiyo ni matokeo ya twiti iliyotengenezwa na maneno hayo kubandikwa katika picha ya moja ya twiti za kituo cha televisheni ya NBS ili kuwahadaa watu waamini uzushi huo. Hakuna mahali ambapo NBS imetwiti kuhusu jambo hilo.

Televisheni ya NBS tayari imekanusha habari hiyo kuwa haikuichapisha. 

Ukiangalia kwa makini picha hiyo utagundua kuwa toka eneo la lilipo jina la akaunti ya yalipo maneno hayo kuna mwanya mkubwa ambao upo tofauti na mwanya unaoachwa katika twiti halisi.

Pia, Kiingereza kilichoandikwa kina makosa mengi ya kisarufi na kimuundo kiasi cha kuacha maswali lukuki kabla ya mtu kuamini kuwa taarifa hizo ni za kweli.

Mbali na uchunguzi huo, Msemaji wa wizara ya afya nchini Uganda, Emmanuel Ainebyoona ameiambia NuktaFakti kuwa habari hiyo ni uzushi na inapaswa kupuuzwa.

“Kuna mtu kafanya uhalifu kwa kughushi twiti ya kituo cha televisheni. Huu ni uongo kabisa. Hapa Uganda hakuna kiongozi wa juu ambaye amesharipotiwa kuwa na Corona mpaka sasa,” amesema Ainebyoona.


Zinazohusiana


Uamuzi wa mwisho

Habari hizo zapaswa kupuuza na watu hawana sababu ya kuendelea kuisambaza kwa kuwa ni uzushi wa kiwango cha lami. Usisambaze habari kama huna uhakika nayo.