October 8, 2024

Mke wa Reginald Mengi aibua mazito kuzuiwa kuliona kaburi la mume wake

Mke wa aliyewahi kuwa mfanyabiashara maarufu Tanzania, Dk Reginald mengi, Jacqueline Ntuyabaliwe (K-Lynn) amesema Asema amechoka kuzuiwa na ndugu wa marehemu mume wake kuingia kwenye kaburi la baba wa watoto wake.

  • Asema amechoka kuzuiwa na ndugu wa marehemu mume wake kuingia kwenye kaburi la baba wa watoto wake.
  • Asema amenyamaza kwa mengi lakini katika hilo hatanyamaza tena.
  • Wafuasi wake wamtaka atafute njia sahihi kumaliza tatizo hilo. 

Dar es Salaam. Mke wa aliyewahi kuwa mfanyabiashara maarufu Tanzania, Dk Reginald Mengi,  Jacqueline Ntuyabaliwe (K-Lynn) amesema amekuwa akizuiwa kuingia katika eneo alilozikwa mume wake na kuwa suala hilo limekuwa likimsononesha yeye na watoto wake na hatalinyamazia tena. 

Mengi ambaye alikuwa Mwenyekiti wa makampuni ya IPP na moja ya watu matajiri na mashuhuri nchini Tanzania alifariki dunia usiku wa kuamkia Mei 2, 2019 mjini Dubai, Falme za Kiarabu alikokuwa akipatiwa matibabu. 

K-Lynn ambaye ni mjane wa watoto wawili wavulana ameandika ujumbe huo leo (Februari 22, 2020) katika ukurasa wake wa Twitter akisema amechoka kuzuiwa na ndugu wa marehemu mume wake kuingia kwenye kaburi la baba wa watoto wake. 

 “Mmefikia hatua ya kunizuia mimi na wanangu kuingia kwenye kaburi la mume wangu, tunafukuzwa eti mpaka tuombe ruhusa ya kuingia kwenye kaburi la mume na baba wa watoto wangu,” inasomeka sehemu ya ujumbe aliyoweka Jacqueline katika ukurasa wake wa Twitter. 


Soma zaidi:


Amebainisha kuwa amekuwa akifukuzwa na kutakiwa kuomba ruhusa kabla ya kuingia kwenye eneo la kaburi alilozikwa mume wake.

Mengi alipumzishwa katika kijiji cha Kisereni Machame mkoani Kilimanjaro, eneo la makaburi ya familia ambapo pia wamezikwa wazazi wake na ndugu wengine. 

Kutokana na kadhi hiyo, mjane huyo ambaye aliwahi kuwa mlimbwende wa Tanzania mwaka 2000 amesema amechoka na hatakaa kimya tena kuhusiana na jambo hilo. 

 pic.twitter.com/6wBm12R5bH

Kutokana na ujumbe huo, wafuasi wa mwanadada huyo wamekuwa na maoni tofauti huku wengine wakimtaka avumilie na kutafuta maridhiano na ndugu wa mume wake.

Wengine wamesema haikuwa sahihi kuweka ujumbe huo Twitter kwa sababu hawezi kupata majibu sahihi lakini atufute watu wenye hekima kulimaliza tatizo hilo. 

“Pole sana dada, hili tatizo lako kwa hapa Twitter haliwezi pata suluhisho,tafuta watu sahihi ikibidi wanasheria, kwa heshima ya mzee wetu mpendwa silioni kuwa na afya kujadiliwa hapa,kaeni mumalize tofauti kama wanafamilia, haya maisha tu,” ameandika MKEKA WAKUDESA (@Mkekawakudesa).

Jacquiline ambaye ni mwanamuziki, mfanyabiashara na mwanzilishi wa kampuni ya samani iliyoshinda tuzo Amorette Ltd alifunga ndoa na Mengi mwaka 2015.

Tangu kufariki kwa mengi, kumekuwa na sintofahamu ya nani hasa anatakiwa kurithi mali zake, jambo ambalo limezua mivutano kati ya K-Lyn na ndugu wa mume wake.