November 24, 2024

Mkimbizi wa zamani wa Afghan azunguka Dunia kwa ndege

Shaesta Waiz aendesha ndege ndogo mwenyewe kuzunguka Dunia

Sheista Waiz, 29, alianza safari hiyo ya aina yake kwenye ndege ndogo yenye injini moja akitokea Marekani ambako ndiko anakoishi mpaka Kabul, Afghanstan.

Bi Waiz amewaambia waandishi wa habari kwamba amefurahi sana kupata nafasi ya kurudi Afghanstan.

“Yapata miaka 29 sasa. Kurudi tena nchini kwangu kama rubani nikizunguka Dunia kuwatia moyo wengine – inanipa furaha sana”

Kama alivyoandika kwenye tovuti yake, Bi Waiz alizaliwa kwenye kambi ya wakimbizi na kuhamia Marekani mwaka 1987 walipokimbia vita ya Afghan na Sovieti.

Anasema alikulia katika mazingira magumu huko Richmond, California, mpaka alipogundua na kuanza kufuatilia mambo ya anga na kwenda chuo kuendeleza ndoto yake.

“Nilipokuwa binti mdogo, niliwaza pengine nitaenda chuo, lakini nitaolewa na umri mdogo na kuanza familia. Lakini nikakutana na kitu ambacho nilikipenda sana, nacho ni kuendesha ndege,” aliliambia jopo la waandishi wa habari huko Kabul.

“Ni faraja ya ajabu sana kuwa rubani wa ndege yako mwenyewe and kuruka kwenda kokoto moyo wako unakotamani. Ni kitu ninachokifurahia sana, kwamba najali na ni mwanamke toka Afghanistan.”

Alianzisha shirika lisilo la faida liitwalo Dreams Soar na anataka safari yake ya kuzunguka Dunia iwape changamoto mabinti na wanawake vijana kuwa wanasayansi, wahandisi na wanamahesabu.

Bi Waiz ni mtu wa kwanza kwenye familia yake kupata shahada ya kwanza na ya pili.

Pia amesema yeye ni mwanamke wa kwanza kuwa rubani ambaye si mwanajeshi kutokea Afghanistan na mwisho wa zoezi lake atakuwa mwanamke mdogo zaidi kuruka mwenyewe kuzunguka Dunia.

Bi Waiz anasema ujumbe wake ni kwamba “haijalishi umeanzia wapi, unaweza kuwa na vikwazo vya aina yoyote lakini cha msingi ni kuwa na ndoto, kuwa na ndoto kubwa, jitume sana uifikie ndoto yako”

Bi Waiz alianza safari yake Florida tarehe 13 Mei na anatembelea nchi 19 kwa ndege yake aina ya Beechcraft Bonanza A36. Akitoka Afghanistan atapita Asia na Australia kabla ya kurudi Florida huko Marekani.

Anasema tayari ana mipango ya kurudi kuishi Afghanistani.

“Miaka michache ijayo nina nia ya kurudi Afghanistan na labda kufungua shule ya urubani au nifanye kitu chochote ili wanawake wa Afghanistani wapate fursa ya kujua ujuzi wa mambo ya anga”

“Hapa wanawake wanapata shida sana” akaongeza “Nina bahati sana nilipata nafasi ya kupata elimu, kupata kitu ninachokipenda ambacho ni kurusha ndege na inaniumiza moyo sana kwakuwa najua kuna wasichana wengi wa umri wangu ambao hawajapata hii fursa”

“Nataka nifanye kitu kuwarudishia hawa wanawake hizi fursa walizopoteza”