Mkulazi kuwawezesha wakulima wadogo kuzalisha sukari Morogoro
Viwanda viwili vitakavyojengwa na kampuni hiyo vitasaidia kupunguza uhaba wa sukari unaolikabili Taifa.
- Benki zahamasishwa kuwapa mikopo wakulima kuinua kilimo cha miwa.
- Viwanda viwili vitakavyojengwa kupunguza tatizo la uhaba wa sukari nchini.
- Mabaki ya miwa kuzalisha umeme wa megawati 20 utakaouzwa kwa Tanesco.
Dar es Salaam. Kampuni Hodhi ya Mkulazi imetoa fursa kwa wakulima wa Kijiji cha Mbigiri wilayani Mvomero mkoa wa Morogoro kujiunga na mpango wa kulima miwa na kukiuzia kiwanda cha Mkulazi II kinachotarajiwa kujengwa katika eneo hilo ili kupunguza tatizo la upungufu wa sukari nchini.
Mkulazi imeandaa utaratibu chini ya Mpango wa Wakulima wa Nje wa Miwa (Mkulazi Sugarcane Out griwers Scheme) ambapo wakulima wanaomiliki mashamba hao wanatakiwa kujiunga katika kikundi ambacho kina mashamba ya miwa yenye ekari zisizopungua 50 kutokana na ukweli kuwa kilimo hicho kina tija kubwa.
Kikundi cha wakulima pia kinatakiwa kujiunga kwenye Chama Cha Msingi Cha Ushirika cha Kuuza Mazao (AMCOS) kitaratibu mauzo ya miwa kwa kampuni ya Mkulazi na kuhakikisha wakulima wanapata stahili zao kwa wakati.
“Kampuni haina haina eneo la kugawa kwa wakulima wa nje, wakulima waliojiunga na mpango huu kwa upande wa Mbigiri wanamiliki maeneo yao wenyewe. Maeneo hayo yatathaminiwa na kupimwa na Maafisa wa Ardhi wa Maafisa wa kilimo wa sehemu husika ili kuthibitisha ukubwa wa eneo na ubora wake kwa kilimo cha miwa kabla ya kukubaliwa katika mpango huu,” inaeleza sehemu ya taarifa ya Mkulazi iliyotolewa hivi karibuni.
Tofauti na wakulima wa Mbigiri, wenzao wa kijiji cha Mkulazi watatengewa eneo kwa ajili ya kukodisha kwa wakulima wa nje.
Katika hatua za awali za kuandaa mashamba na mitaji ya kuendesha kilimo hicho, Mkulazi imezihamasisha benki ikiwemo ya Azania ambayo imeanza kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa wakulima kupitia udhamini wa vyama vya ushirika.
Katika taarifa yake iliyotolewa Agosti 14 mwaka huu, Mkulazi ambayo ni kampuni hodhi iliyoanzishwa kwa ubia baina ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Taifa (NSSF) na Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) Septemba 2016, ina lengo la kuanzisha viwanda viwili katika maeneo ya Mkulazi wilayani Ngerengere na Mbigiri wilayani Mvomero katika mkoa wa Morogoro ili kuzalisha wastani wa tani 250,000 za sukari kwa mwaka.
“Tani 200,000 zitazalishwa kupitia kiwanda cha Mkulazi I (Ngerengere) na tani 50,000 kutoka kiwanda cha Mkulazi II (Mbigiri),” inasomeka sehemu ya taarifa ya Mkulazi.
Ikiwa mpango huo wa uzalishaji miwa na ujenzi wa viwanda vya sukari utatekelezwa kikamilifu, huenda ukasaidia kuondoa changamoto za uagizaji sukari nje ya nchi ili kufidia upungufu unaojitokeza kila mwaka.
Hadi sasa Nukta kupitia taarifa za Wizara ya Biashara,Viwanda na Uwekezaji inatambua kwamba, viwanda vya ndani vya ndani vinazalisha wastani wa tani 300,000 kwa mwaka wakati mahitaji halisi ni tani 420,000 kwa mwaka, hivyo kuwepo kwa pengo la tani 120,000.
Ikiwa miwa italima kwa wingi nchini itasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa sukari. Picha| IPPMedia.
Mpango huo pia utahusisha wakulima wakubwa na taasisi zenye mashamba yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 250 ambazo ziko tayari kuwekeza kwenye kilimo cha miwa ili kusaidiana na shamba la kampuni hiyo lenye ukubwa hekta wa 63,227 linalopatikana katika vijiji vitano vya Usungura, Chanyumbu, Mkulazi, Kidunda na Kwaba ambavyo wananchi wake wanajishughulisha na kilimo na ufugaji.
Shamba hilo ambalo liko katikati ya reli ya TAZARA na reli ya kati likiwa limepakana na Mto Ruvu linatarajia kuajiri wananchi 100,000 ambao watahudumu shambani na viwandani.
Licha Mkulazi kujitosa katika kuinua kilimo na viwanda vya miwa nchini, itaelekeza nguvu zake pia katika kilimo cha alizeti, mtama mweupe, dengu, ufuta na uzalishaji wa umeme wa mabaki ya miwa kiasi cha megawati 20 kwa ajili ya viwanda vya sukari na kuuza kwa Shirika la Umeme nchini (Tanesco).