November 24, 2024

Mnada wa korosho kuanza Oktoba 9

Utazinduliwa katika Wilaya za Masasi na Tandahimba mkoani Mwanza.

  • Ulisogezwa mbele kwa siku saba kutoka Oktoba 2, 2020.
  • Utaanza katika Wilaya za Masasi na Tandahimba mkoani Mwanza.
  • Bodi ya Korosho yasambaza magunia ya kukusanyia korosho za wakulima. 

Dar es Salaam. Mnada wa ununuzi wa korosho katika msimu wa mwaka 2020/21 utaanza rasmi kesho Oktoba 9, 2020 katika Mkoa wa Mtwara ili kuwapata fursa wakulima kuuza zao hilo kwa wanunuzi. 

Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) katika ratiba yake mpya imeeleza kuwa mnada wa kwanza wa ununuzi wa zao hilo la biashara unaratajiwa kuanza Oktoba 9, 2020 siyo Oktoba 2 kama ilivyoripotiwa awali.

Mnada huo wa kwanza katika msimu wa 2020/21 ambao unahusisha ununuzi wa korosho ghafi kutoka kwa wakulima utafanyika katika maeneo mawili ya Chama cha Msingi cha Ushirika cha Luatala (Luatala Amcos) wilayani Masasi na katika mji wa Tandahimba mkoani Mtwara. 

Siku inayofuata yaani Oktoba 10, mnada utafanyika Mnazi Mmoja Amcos katika Mkoa wa Lindi na kuendelea maeneo mengine ambapo kwa mujibu wa ratiba ya CBT, minada hiyo itahitimishwa Januari 17, 2021 katika kituo cha malipo cha Liwale mkoani humo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CBT, Francis Alfred amesema wamejiandaa kuhakikisha rasilimali za ukusanyaji wa korosho ikiwemo magunia yanapatikana wakati wote wa ununuzi wa zao hilo.

Akizungumza Septemba 22, 2020 wakati Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya alipotembelea Bodi ya Korosho, Alfred alisema tayari vyama vya ushirika vina magunia 700,000 huku mengine milioni 2.3 yamewasili nchini tayari kuanza kusambazwa kabla ya kuanza msimu wa ununuzi mwaka huu.

“Sitaki ifike sehemu tatizo la upatikanaji magunia ya kukusanyia korosho za wakulima lijitokeze mwaka huu tena. Bodi ya korosho fuatilieni vyama vikuu vyenye dhamana ya kuagiza magunia vitekeleze wajibu wao haraka,” alisema Kusaya. 


Soma zaidi:


Hata hivyo, bodi hiyo haijaweka wazi bei elekezi ya zao hilo na idadi ya wanunuzi waliojitokeza kununua mpaka sasa, licha ya Serikali kusema itahakikisha wakulima wanapata bei nzuri zinazoendana na uzalishaji. 

Ununuzi wa korosho wa msimu mpya unahusisha teknolojia ya wanunuzi kujisajili kwenye Bodi ya Korosho kupitia mfumo wa Wizara ya Kilimo wa kusimamia Biashara za Kilimo (Agricultural Trade Management Informataion System – ATMIS)

Pia mfumo wa ununuzi wa korosho utakuwa kwa njia ya mnada wa wazi kwa kutumia jukwaa la Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).  

Korosho ina umuhimu wake katika maisha ya Watanzania hasa wakulima wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani, Ruvuma na Tanga kwa kuwa hutegemea zao hilo kujiingizia kipato ambacho hutumika kutunza familia na kusomesha watoto ili kuondokana na umaskini katika jamii.