October 6, 2024

Mo Dewji awashauri vijana kuacha kutumia zaidi ya wanachopata

Amewashauri kuishi kulingana na uwezo wao na kuepuka kukimbilia wasivyoviweza huku ushauri wake ukipokelewa kwa hisia tofauti na vijana.

  • Amewashauri kuishi kulingana na uwezo wao na kuepuka kukimbilia wasivyoviweza.
  • Awapa kaulimbiu ya “uishi chini ya uwezo wako lakini ndani ya mahitaji yako.”
  • Ushauri wake wapokelewa kwa hisia tofauti na vijana.

Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu na mdhamini wa timu ya Simba, Mohammed Dewji maarufu kama Mo amewashauri vijana kuishi kulingana na uwezo wa vipato vyao wanavyopata huku wakijiepusha kukimbilia maisha wasiyoyaweza. 

Mo Dewji ametoa ushauri huo katika ukurasa wake Twitter ambapo amesema vijana wanapaswa kujitia nidhamu ya matumizi ya pesa ili kujihakikishia maisha kutokana na kipato wanachopata katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. 

Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la BBC, mfanyabiashara huyo ambaye ni tajiri namba moja Afrika Mashariki, na tajiri mdogo zaidi Afrika amebainisha kuwa kaulimbiu ya kijana lazima iwe, “uishi chini ya uwezo wako lakini ndani ya mahitaji yako.”

Mo Dewji na wafanyabiashara wengine maarufu duniani kama Warren Buffett na Bill Gates wa Marekani wamekuwa mstari wa mbele kutoa ushauri kwa vijana jinsi ya kutumia fedha vizuri na kuwekeza katika mambo ya msingi ikiwemo ujasiriamali ambao unaweza kuwatoa kimaisha. 


Zinazohusiana: 


Hata hivyo, ujumbe wa Mo Dewji umepokelewa kwa hisia tofauti na wafuasi wake ambapo baadhi yao wameonyesha kuukubali kwa sababu unawakumbusha mambo ya msingi ya kufanya ili wafikie ndoto zao katika safari ya mafanikio. 

“Vijana hatuna budi kuishinda tamaa hasi . Hakika ndio adui mkubwa wa mifuko yetu,” ameandika @Lord_Ibra2 Jun 18 wakati akitoa maoni yake katika ukurasa wa Twitter. 

Wachangiaji wengine wamesema changamoto wanayokutana nayo ni mahitaji kuwa makubwa kuzidi kipato wanachokipata, jambo linalowazuia kuweka akiba na wakati mwingine wanaingia katika madeni. 

“Tatizo huja pale mahitaj yanakuwa mengi kuliko kipato..Inabidi tubaki kusema ‘Tumia pesa ikuzoee’..we are grateful though (tunashukuru),” amesema @Neylan. 

Ujumbe unaofanana huo, aliutoa mwanzoni mwa mwaka huu ambapo aliwasisitiza vijana ambao ni nguvukazi muhimu ya Taifa kuzingatia bajeti wanazojiweka ili kuepuka matumizi ya pesa yasiyo na mpangilio. 

Mo, aliyezaliwa miaka 44 iliyopita katika kijiji cha Ipembe mkoani Singida, mbali na kuwa mfanyabiashara,amewahi kuwa Mbunge wa Singida Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi kati ya mwaka 2005 na 2015.