November 24, 2024

Mohammed Dewji awapa vijana ujumbe wa kufungulia mwaka

Awashauri vijana kupanga bajeti vizuri ili kuepuka kutokujua pesa yao imetumikaje.

  • Awashauri vijana kupanga bajeti vizuri ili kuepuka kutokujua pesa yao imetumikaje.
  • Amesisitiza vijana waache tabia ya kutumia pesa ambayo hawana.
  • Baadhi ya wafuasi wake wameupokea ujumbe wake kwa hisia tofauti ambapo wengi wao wameonyesha kuukabali na kuutumia katika mipango na maisha yao.

Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu na mdhamini wa timu ya Simba, Mohammed Dewji amewashauri vijana kujenga utamaduni wa kupanga bajeti ili kuepuka matumizi ya fedha zisizokuwepo ikiwa ni njia ya kujiletea maendeleo. 

Dewji maarufu kama Mo Dewji ametoa ushauri huo leo (Januari 3, 2018) katika ukurasa wake wa Twitter ukiwa ni ujumbe wake wa pili kuweka katika mtandao huo tangu mwaka 2019 uanze.

Amebainisha kuwa vijana wanapaswa kuweka bajeti na kuifuata, licha ya kupata vishawishi vya kutumia pesa vibaya lakini wakiwa kwenye bajeti wanajifunza kuelekeza pesa pa kwenda na si kujiuliza pesa ilipokwenda.

“Usitumie usichokuwa nacho! Uwe makini na masuala ya pesa 2019,” ameandika Mo.

Changamoto inayowakumba vijana wengi ni kukosa elimu ya masuala ya fedha jambo linalowafanya waendelee kuona kila siku hawana pesa kutimiza malengo yao.

Mo Dewji na wafanyabiashara wengine maarufu duniani kama Warren Buffett wamekuwa mstari wa mbele kutoa ushauri kwa vijana jinsi ya kutumia fedha vizuri na kuwekeza katika mambo ya msingi ikiwemo ujasiriamali ambao unaweza kuwatoa kimaisha. 


Zinazohusiana: Mbinu zitakazokusaidia kutimiza malengo wakati ukiukabili mwaka mpya

                        Jinsi ya kufanya mitandao ya kijamii isikuharibie mahusiano yako


Bilionea huyo ambaye ni tajiri namba moja Afrika Mashariki, na tajiri mdogo zaidi Afrika ambaye ana utajiri unafikia Dola za Marekani 1.5 bilioni ana wafuasi 613,000 katika mtandao wa Twitter.

Baadhi ya wafuasi wake wameupokea ujumbe wake kwa hisia tofauti ambapo wengi wao wameonyesha kuukabali na kuutumia katika mipango na maisha yao.

Hata hivyo, siyo mara ya kwanza kwa Mo Dewji kutoa jumbe mbalimbali zinazohamasisha maendeleo hasa kwa vijana ili waweze kufika malengo waliojiwekea katika kufanikiwa kwa vile wanavyovifanya.