September 29, 2024

Mradi wa kuchakata gesi LNG Tanzania sasa kuanza Julai 2023

Mradi huo wa kusindika gesi asilia na kuwa kimiminika (LNG) utakaojengwa mkoani Lindi unatarajiwa kuanza Julai, 2023 ukipigwa kalenda ya mwaka mmoja zaidi ya mipango ya awali.

  • Majadiliano baina ya wawekezaji yamekwama kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
  • Rais Samia amekuwa akihimiza Wizara ya Nishati kukamilisha mazungumzo na wawekezaji.
  • Unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitano.

Dar es Salaam. Waziri wa Nishati, Dk Madard Kalemani amesema mradi kusindika gesi asilia na kuwa kimiminika (LNG) utakaojengwa mkoani Lindi unatarajiwa kuanza Julai, 2023 ukipigwa kalenda ya mwaka mmoja zaidi ya mipango ya awali. 

Mradi huo unatarajia kutumia gesi kutoka katika vitalu namba 1, 2 na 4 mkoani humo na kuuzwa katika masoko ya nje ambapo gharama za mradi huu zinakadiriwa kuwa Dola za Marekani bilioni 30 sawa na takriban Sh70.5 trilioni. 

Hata hivyo, utekelezaji wa mradi huo umekuwa ukipigwa danadana kutokana na kutokamilika kwa majadiliano baina ya wawekezaji wa mradi huo uliopo kusini mwa Tanzania. 

Dk Kalemani ameliambia Bunge leo Juni 2, 2021 wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2021/22 kuwa baada ya kuanza kujengwa Julai mwaka 2023, unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni, 2028.

Mwaka 2019 Serikali ilisema mradi huo ungeanza ujenzi mwaka 2022 na kukamilika mwaka 2028. Hata hivyo, mabadiliko hayo mapya ya kuanza kwa ujenzi hakujabadilisha matazamio ya awali ya kukamilisha mradi huo mwaka 2028. 

Dk Kalemani amesema kazi zilizotekelezwa hadi kufikia mwezi Machi, 2021 katika mradi huo wa LNG ni pamoja na kukamilisha malipo ya Sh5.7 bilioni kwa ajili ya fidia na riba kwa wananchi 642 waliopisha mradi; na kuweka mpaka eneo la mradi (Likong’o, Mto Mkavu na Masasi ya Leo).

“Katika mwaka 2021/22 kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na: kukamilisha majadiliano ya kimkataba (Host Government Agreement negotiations) na wawekezaji wa mradi; kukamilisha mapitio ya mikataba ya ugawanaji mapato (Production Sharing Agreements – PSAs),” amesema Dk Kalemani.

Iwapo majadiliano ya kimkataba yataafikiwa baina ya Serikali na wawekezaji wa mradi huo, utamaliza mvutano wa uliodumu kwa muda mrefu katika kuanza kutekelezwa kwake. 


Zinazohusiana:


Mradi huo unatekelezwa kwa ushirika na kampuni za kimataifa za mafuta za Shell, Equinor, Pavillion, Exxon Mobil, Ophir Energy na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan aliiagiza wizara ya nishati ya Tanzania kukamilisha majadiliano na wawekezaji ili mradi huo uanze kutekelezwa. 

Tanzania inakadiriwa kuwa na futi za ujazo trilioni 57.54 za gesi asili ambazo uzalishaji wake utasaidia taifa hilo la Afrika Mashariki kupata faida lukuki za kiuchumi ikiwemo kuchangia ongezeko la kasi ya ukuaji wa uchumi hadi kuzidi asilimia 7 mwanzoni mwa mradi.  

Kuanza kwa ujenzi wa mradi huo wa LNG huenda ikiwa moja ya kete muhimu ya kisiasa na mafanikio kwa Rais Samia ambaye amerithi miradi mikubwa ya kimkakati ya kimaendeleo ikiwemo mradi wa umeme wa bwawa la Nyerere litakalo kuzalisha megawati 2,115 kutoka kwa mtangulizi wake hayati Dk John Magufuli.