November 24, 2024

Mtanzania atwaa tuzo ya ubunifu nchini Misri

Rahma Bajun amepokea tuzo ya utambuzi kutoka jukwaa la ‘Arab and African Youth Platform’.

  •  Rahma Bajun amepokea tuzo ya utambuzi kutoka “Arab and African Youth Platform” Jijini Aswan nchini Misri mapema jana (17 Machi 2019)

Dar es Salaam Mbunifu wa mavazi kutoka Tanzania Rahma Bajun amepokea tuzo ya utambuzi kutoka “Arab and African Youth Platform” Jijini Aswan nchini Misri mapema jana (17 Machi 2019) huku akipokea sifa lukuki kutoka kwa  Watanzania.

Mwanadada huyo, ambaye  hushiriki  kwenye  maonyesho mbalimbali, amefanikiwa kuliteka soko la mitindo ndani na nje ya nchi kwa muda mfupi huku akivalisha baadhi ya vigogo nchini wakiwamo Maria Tsehai Sarungi na Zitto Kabwe.

Saa chache baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo na Rais wa Misri Abdelfattah Elsisi pamoja na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki , mamia ya Watanzania walisifu kazi za mwanadada huyo kupitia kurasa za mitandao ya kijamii ikiwemo Twitter.

Baadaye kidogo, Bajun aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akisema  “Ni heshima kwangu na kwa nembo ya MnM na kwa Tanzania kupokea tuzo hii sambamba na vijana mahiri kutoka Uarabuni na Africa.”

Kinachovutia zaidi juu ya ubunifu wake ni kwamba Rahma hutumia malighafi zinazotengenezwa nchini kwa kuwa kwa asilimia kubwa hushona mavazi yatokanayo na vitenge ama khanga.

Wengi wanamfahamu Rahma kama mbunifu wa mavazi anayechipukia nchini Tanzania lakini huenda siku zijazo neno anachipukia likabadilishana na “mwenye mafanikio zaidi” kwa kuwa amekuwa akikua siku hadi siku kupiga hatua katika kazi za ubunifu.