October 6, 2024

Mtindo wa maisha anayotakiwa kuishi mjasiriamali

Mjasiriamali aliyefanikiwa anaishi maisha ya kawaida yanayoendana na jamii inayomzunguka huku akizingatia uadilifu, uaminifu na kuwekeza katika kuimarisha thamani ya huduma na bidhaa anazotoa.

  • Mjasiriamali aliyefanikiwa anaishi maisha ya kawaida yanayoendana na jamii inayomzunguka
  • Ni mwadilifu, mwaminifu na anawekeza katika kuimarisha thamani ya huduma na bidhaa anazotoa.

Dar es Salaam. Ujasariamali wa aina yoyote ni safari ya kukua kutoka chini hadi kufika katika kilele cha mafanikio ya huduma na bidhaa unazouza kwa wateja wako ili kuiwezesha biashara yako kukua na kuwafikia watu wengi zaidi.

Lakini mjasiriamali anapaswa kuishi maisha gani? Baadhi ya wajasiriamali waliofanikiwa duniani wanaeleza mtindo wa maisha ya mjasiriamali mwenye ndoto za kufika mbali. 

Mjasiriamali na Mwandishi wa vitabu wa nchini Afrika Kusini, Alan Knott-Craig katika mikutano ya motisha kwa wafanyabiashara amekuwa akisisitiza kuwa  mjasiriamali anapaswa kuishi maisha ya kawaida yanayoendana na jamii inayomzunguka.

Anasema hali hiyo inasaidia kujiona sehemu ya jamii yake na watu kuzipokea kirahisi huduma na bidhaa anazotoa. 

Craig ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao wa Mxit anabainisha kuwa maisha ya mjasiriamali ni pamoja na kupunguza gharama za maisha, na kuwekeza fedha katika miradi na fursa zinazojitokeza mbele yake ili kujiongezea faida na uhuru wa kifedha (Financial Freedom)

Wakati akizungumza katika warsha ya Startup Grind Cape Town, Aprili 3, 2019 nchini Africa Kusini, Craig aliweka wazi kuwa mjasiriamali pia anatakiwa kujenga mtandao mpana wa watu anaofanya nao kazi ili kufanikisha malengo yake.

“Hauna chaguo. Huwezi kuanza moja kwa moja, ni vigumu. Sio haiwezekani kabisa, lakini ni ngumu kuanzisha kitu peke yako, unahitaji watu wa kukusaidia,” anasema Craig.

Wadau wengine wanaeleza kuwa ujariamali ni zaidi ya kuishi maisha ya kawaida bali ni kuwa mwaminifu na kulifahamu soko lako vizuri.

Ujasiriamali ni dhana mtambuka lakini unajikita zaidi katika kuboresha thamani ya bidhaa na huduma. Picha|Mtandao.

Mwandishi katika mtandao wa Addicted2Success wa nchini Australia, Sarah Peterson anasema dhana ya ujasiriamali na mjasiriamali inajengwa katika misingi ya uadilifu na uaminifu.

Anasema uadilifu unasaidia kuaminiwa na watu unaofanya nao biashara kwasababu, “ watu wanafanya biashara na watu wanaowafahamu, wanaowapenda na kuwaamini.”


Zinazohusiana:


Katika hatua nyingine, Peterson anasema mjasiriamali aliyekomaa anaamini katika ushindani na jambo hilo ni afya katika ukuaji wa biashara yoyote. 

Ushindani unakupa kuwafahamu vizuri washindani wako na maeneo muhimu ya kuyafanyia kazi hasa katika uboreshaji wa huduma, bidhaa na soko. 

Unataka kuwa mjasiriamali basi ishi maisha ya kawaida huku ikizingatia uadilifu na uaminifu katika kila eneo la biashara yako.