November 24, 2024

Muswada sheria ya bima ya afya kwa wote kutua bungeni Juni 2021

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima amesema wizara yake inakusudia kuwasilisha muswada wa Sheria ya Bima ya afya kwa Wote bungeni Juni mwaka huu.

  • Itasaidia wananchi wote kupata huduma za afya bila kikwazo cha fedha.
  • Sheria hiyo ikipita itaondoa changamoto za afya hasa kwa watu masikini. 

Dar es Salaam. Adha ya kukosa matibabu ya uhakika kwenye vituo vya afya inayokumba baadhi ya Watanzania kutokana na ukosefu wa fedha inaweza kutokomezwa siku chache zijazo baada ya Serikali kuongeza kasi ya mchakato wa uanzishwaji wa bima ya afya kwa wote. 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima amesema wizara yake inakusudia kuwasilisha muswada wa Sheria ya Bima ya afya kwa Wote bungeni Juni mwaka huu.

Gwajima, ambaye pia ni Mbunge wa kuteuliwa na Rais, amesema maudhui ya sheria hiyo ni kutoa fursa kwa wananchi wote kupata huduma za afya bila kikwazo cha fedha na hatimaye kulifikia lengo namba 3 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Lengo hilo linahimiza nchi zote duniani kuhakikisha ifikapo 2030, wananchi wake wanakuwa na afya bora kwa kuboresha huduma za afya katika ngazi zote kwenye jamii.

Wizara hiyo imetenga Sh231.7 milioni kwa ajili ya uratibu wa zoezi hilo muhimu ambalo litawahakikishia wananchi wa kipato cha chini matibabu ya uhakika wanapokwenda hospitali. 

Endapo Bunge litapitisha muswada huo na kutunga sheria ya bima, itawafanya watu wote kuwa katika mfuko wa bima ya afya na hivyo kujihakikishia matibabu katika vituo vya afya.

Kwa mujibu wa Dk Gwajima, hivi sasa, Watanzania milioni 8.3 sawa na asilimia 14.7 ya Watanzania wote (takriban milioni 59.4) ndiyo wanaonufaika na huduma za bima ya afya. Hii ni sawa na kusema Watanzania 15 tu kwa kila 100 nchini Tanzania ndiyo wanapata huduma ya bima ya afya. 

“Kati ya wananchi waliojiunga na mfumo wa bima ya afya, asilimia 8 wamesajiliwa na NHIF (Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya), asilimia 5.4 wanahudumiwa na iCHF (bima ya afya jamii iliyoboreshwa), asilimia 0.3 wanufaika na huduma kupita SHIB-NSSF na asilimia 1 wakiwa wamejiunga na bima ya afya inayotolewa na makampuni ya bima binafsi za afya,” amesema Gwajima katika hotuba yake.

Bima ya afya husaidia mnufaika kutovunja kibubu chake pale yeye au mtegemezi wake anapougua kwa ajili ya kugharamia matibabu katika vituo vya afya.


Soma zaidi:


Bajeti wizara ya afya yaongezeka

Wizara ya Afya imeliomba Bunge lijadili na kuidhinisha Sh1.1 trilioni kwa ajili ya bajeti ya mwaka 2021/22 ambapo kati ya fedha hizo Sh491.7 bilioni (asilimia 45.6)  ni fedha za miradi ya maendeleo.

Bajeti hiyo imeongezeka  kutoka Sh900.1 bilioni iliyotengwa mwaka 2020/21 ambapo hadi Aprili mwaka huu, wizara ilipokea Sh667.8 bilioni ya bajeti iliyoidhinishwa sawa na asilimia 74 au robo tatu ya bajeti nzima kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake. 

Tofauti na miaka ya nyuma pamoja na changamoto nyingine za afya, wizara hiyo ina kazi ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa corona ambao umeongeza gharama za afya katika mataifa mengi ulimwenguni zikiwemo ununuzi wa vifaa vya kupimia, vifaa vya kujikinga (PPEs).