October 7, 2024

Muungano wa kuthibitisha habari za Corona wazinduliwa Afrika

Unaunganisha mashirika 13 ya kimataifa na makundi ya uthibitishaji habari yanayojihusisha na takwimu, utafiti, afya ya kidijitali na mawasiliano.

  • Muungano huo unahusisha zaidi ya mashirika 10 ya kimataifa na uthibitishaji habari.
  • Muungano huo utakua na kazi kubwa ya kupambana na habari za uzushi kuhusu Corona Afrika.
  • Pia utawawezesha wanahabari kupata taarifa sahihi za kuhabarisha umma.

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limeanzisha muungano mpya wa kudhibiti na kupambana na habari za uongo zinazohusu sekta ya afya ukiwemo ugonjwa wa virusi vya Corona na dharura zingine za kiafya barani Afrika.

Muungano huo unaojulikana kama ‘Africa Infodemic Response Alliance’ (AIRA) ulizionduliwa mapema mwezi Desemba mwaka huu unaunganisha mashirika 13 ya kimataifa na makundi ya uthibitishaji habari yanayojihusisha na takwimu, utafiti, afya ya kidijitali na mawasiliano.

Baadhi ya mashirika hayo ni pamoja na  Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (CDC), Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (IFRC), Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Taasisi zingine ni Shirika la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Africa Check, Agence France-Presse Fact Check, PesaCheck, Dubawa na Meedan.

Mkurugenzi wa WHO kanda Ya Afrika, Dk Matshidiso Moeti, amesema katika kipindi cha dharura ikiwemo COVID-19, habari za uongo zinaweza kusababisha madhara mengi ikiwemo vifo na ongezeko la magonjwa.

Amesema muungano huo utasaidia kukabiliana na habari za uzushi barani Afrika na hivyo kuwawezesha watu kufanya maamuzi sahihi kutoka vyanzo sahihi vya habari.

“Watu wanahitaji ukweli uliothibitishwa kisayansi kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya na ustawi wao, uwepo wa mchanganyiko wa wimbi la habari za uongo unasababisha ugumu kufahamu kipi ni halisi  na sahihi,” amesema Dk Moeti wakati wa uzinduzi wa muungano huo Desemba 3, 2020. 

Kwa mujibu wa WHO, tangu Corona ilipotiwe mwaka 2019, zaidi ya taarifa bilioni 270 zinazohusiana na ugonjwa huo zimesambazwa na kutazamwa mtandaoni.


Soma zaidi:


Pia, habari za aina hiyo zimetajwa takribani mara milioni 40 katika mtandao wa Twitter na katika vyombo vya habari mbalimbali mtandaoni.

Shirika hilo limesema kwa sehemu kubwa habari hizo ni za kupotosha na zisizo na ukweli na bado zinaendelea kusambazwa na wadau wa mitandao ya kijamii bila kufahamu madhara yanayotokea kwenye jamii. 

“Kupima kwa kiasi gani habari zinazosambaa zinapotosha ni vigumu lakini mashirika mbalimbali ya uthibitishaji barani Afrika yanasema kuwa yamethibitisha zaidi ya habari na ripoti 1,000 kuwa za uongo tangu kuanza kwa ugonjwa waCorona,” inaeleza WHO.

Umoja huo utakua na kibarua kigumu cha kupambana na habari za uongo zinazoenea kuhusu chanjo ya ugonjwa wa COVID-19 na kukuza ufahamu wa kiafya huku ukiwawezesha wanahabari kupata taarifa sahihi kuhusu ugonjwa huo. 

Wakati WHO ikianzisha muungano huo, tovuti ya habari ya Nukta (www.nukta.co.tz) kupitia programu yake ya #NuktaFakti imekua ikifanya kazi ya kuthibitisha habari mbalimbali zikiwemo za Corona tangu Mei, 2020. 

Unaweza kutembelea ukurasa wa Facebook wa Nukta Fakti kujifunza zaidi.