Mwalimu Nyerere kujengewa sanamu ya kumuenzi Ethiopia
Ujenzi wa sanamu hiyo unaoratibiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, tayari upo kwenye hatua za awali na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba 2020.
- Sanamu hiyo inatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh600 milioni.
- Ikikamilika, itasafirishwa kutoka nchi ya Afrika Kusini inapotengenezewa hadi makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU), Ethiopia.
- Wazo la ujenzi wa sanamu hiyo, lilitolewa na Rais wa zamani wa Zimbabwe Hayati Robert Mugabe.
Dar es Salaam. Sanamu ya baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere inatarajiwa kujengwa katika viwanja vya jengo la amani na ulinzi la Julius Nyerere lililopo kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) Jijini Addis Ababa, Ethiopia ili kuenzi mchango wake katika mapambano ya kudai uhuru wa Afrika.
Ujenzi wa sanamu hiyo unaoratibiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, tayari upo kwenye hatua za awali na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba 2020.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe amesema ujenzi wa sanamu hiyo ni utekelezaji wa azimio la mkutano wa 35 wa wakuu wa nchi na serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Jijini Harare, Zimbabwe mwaka 2015.
“Ujenzi huo, lengo lake ni kutambua na kuenzi mchango wa waanzilishi wa SADC(akiwemo Mwalimu Nyerere) katika kulikomboa bara la Afrika,” amesema Dk Mwakyembe katika hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2020/2021 Bungeni Jijini Dodoma hivi karibuni.
Mwakyembe emesema sanamu hiyo itajengwa kwa kutumia malighafi ya shaba nyeusi (bronze statue) na kamati za ujenzi wake imeshaundwa tangu mwaka 2018.
Zinazohusiana
- Bashungwa: Sijapewa fedha za maendeleo wizara ya viwanda, biashara 2019-2020
- Serikali yasema ongezeko la bajeti ya kilimo litategemea mahitaji ya kibajeti ya sekta nyingine
- Kamwelwe aomba matrilioni kugharamia ujenzi, uchukuzi Tanzania
Naye Meneja Mradi wa mradi huo Dk Emmanuel Ishengoma ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya wizara hiyo amesema mradi unatekelezwa na kampuni ya SAMCRO ya nchini Afrika Kusini chini ya usimamizi wa SADC na Tanzania.
Sanamu hiyo inayotarajia kugharimu Sh615 milioni ambazo zitatolewa na SADC huku Serikali ya Tanzania ikichangia gharama za usimamizi wakati wa ujenzi wa sanamu hiyo ambayo kazi kubwa inafanyika nchini Afrika Kusini.
Dk Ishengoma ameongeza kuwa sannamu hiyo ikikamilika na kuridhiwa na Tanzania pamoja na SADC itasafirishwa na kusimikwa katika makao makuu ya AU.
Ujenzi wa Sanamu hiyo umetokana na wazo alilolitoa Rais wa zamani wa Zimbabwe Hayati Robert Mugabe katika mkutano wa 35 wa wakuu wa nchi na serikali wa SADC kuhusu mkakati wa kuwaenzi viongozi waanzilishi wa SADC ambao walishiriki katika kulikomboa bara la Afrika.