November 24, 2024

Mwandishi wa Nukta Africa kinara tuzo za takwimu 2020

Ni Rodgers George ambaye ameibuka mshindi wa tatu katika tuzo za mwandishi bora wa kitakwimu zinatolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

  • Ni Rodgers George ambaye ameibuka mshindi wa tatu katika tuzo za mwandishi bora wa kitakwimu.
  • Tuzo hizo zinatolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
  • Wengine waliopata tuzo hiyo ni Veronica Mrema kutoka blogu ya Maisha na mwanahabari kutoka gazeti la Mwananchi, Halili Letea. 

Dar es Salaam. Mwandishi wa habari wa kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa, Rodgers George ametangazwa kuwa moja ya waandishi watatu bora wa habari za kitakwimu kwa mwaka 2020 nchini Tanzania, ikiwa ni mara ya pili kwa mwanahabari wa kampuni hiyo kupata tuzo hizo za heshima.  

Tuzo hizo ambazo hutolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinalenga kuhamasisha uandishi wa habari za takwimu kwenye vyombo vya habari zenye mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii.

Katika tuzo hizo, George alikuwa mshindi wa tatu baada ya mfululizo wa makala zake za kuhusu namna tumbaku zinavyoiathiri jamii zilizochapishwa kwenye tovoti ya Nukta Tanzania (www.nukta.co.tz) kupenya katika nafasi za juu. 

Hii ni mara ya pili mwandishi wa Nukta Africa anapata tuzo hizo za heshima katika tasnia ya habari nchini. Mwaka 2019 Mhariri wa habari, Daniel Samson aliibuka mshindi wa kwanza wa tuzo hizo wakati zinaanzishwa.

George amepata tuzo hiyo wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika (ASD 2020) zilizofanyika leo Novemba 18, 2020 mkoani Kigoma. 

Wengine waliopata tuzo hiyo ni Veronica Mrema kutoka blogu ya Maisha ambaye ameshika nafasi ya pili na habari yake iliyoshinda ilichapishwa katika gazeti la Jamvi la Habari huku mwanahabari kutoka gazeti la Mwananchi, Halili Letea akishika nafasi ya kwanza.

Akizungumza mara baada ya kupata tuzo hiyo, George ambaye huandika habari za teknolojia na jamii, amesema tuzo aliyoipata leo imemuongezea motisha ya kuandika zaidi habari za takwimu ili kuinufaisha jamii inayomzunguka. 

“Nina mwaka mmoja tu tangu nianze rasmi kazi ya uandishi wa habari za takwimu…tuzo hii inanipa motisha ya kuendelea kuandika habari hizo kwa manufaa ya jamii,” amesema George. 

Rodgers George (kushoto) akipokea tuzo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Hanga wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika (ASD 2020) zilizofanyika leo Novemba 18, 2020 mkoani Kigoma. Picha|NBS.  

Nukta Africa yazungumzia ushindi huo

Mkuu wa Utawala na Fedha wa Nukta Africa, Maphosa Banduka amesema ushindi wa Rodgers ni moja ya ishara njema kuwa habari za takwimu Tanzania na wanahabari wa kampuni hiyo wanatambulika na kuweza kupata tuzo kubwa za kitaifa.

“Tuzo hii ina tafsiri kubwa sana kwetu Nukta Africa na inatuongezea faraja na nguvu zaidi ya kuendelea kutumia takwimu katika kuhabarisha, kuelimisha na kuisaidia jamii yetu ya Kitanzania na dunia nzima kuhusu mambo mbalimbali ya maisha,” amesema Banduka. 

Banduka amesema ushindi alioupata Rodgers uwe chachu kwa wanahabari wa Tanzania kuchangamkia mafunzo ya uandishi wa habari za takwimu ambayo yanatolewa na kampuni hiyo ili kuongeza kasi ya kuwafikia wananchi kwa takwimu.

“Mwisho nampongeza ndugu Rodgers George kwa kuwa miongoni mwa waandishi watatu bora wa Takwimu kwa mwaka 2020, kwani ametuwakilisha vema,” amesema Banduka.


Soma zaidi: 


Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Hanga amesema tuzo hizo za NBS ni chachu ya matumizi sahihi ya takwimu kwenye jamii na shughuli za maendeleo.

“Vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuelimisha jamii juu ya masuala ya takwimu. Nawapongeza NBS kwa mashindano haya yanayochochea uandishi wa habari wa takwimu,” amesema Hanga ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo.

Hanga amesema takwimu ni muhimu katika maendeleo kwa sababu zinasaidia kufanya maamuzi na kupima mafanikio ya Serikali.

“Takwimu ni jicho la Serikali,” amesema Hanga mara baada ya kukabidhi tuzo hizo kwa washindi.  

Tuzo hizo zilizoanza kutolewa mwaka 2019 zinalenga kuwahamasisha na kuwashajiisha waandishi wa habari kutumia takwimu kuchambua, kuhoji na kuchunguza masuala yanayoisibu jamii.

Pia husaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa takwimu na matumizi yake ambayo yanatawala maisha ya kila siku. 

Mshindi wa kwanza wa tuzo hizo, Halili Letea kutoka gazeti la Mwananchi amesema tuzo hizo ziwe chachu kwa wanahabari wengine wa Tanzania kubobea katika uandishi wa takwimu ili kuisaidia jamii kufanya maamuzi sahihi kwa kutumia vyanzo vya uhakika. 

“Hili ni jambo kubwa sana kwangu kwani linahamashisha kuendelea kufanya kazi nyingi za takwimu na kuendea kuwahabarisha watu juu ya mambo yanayowahusu kwa kutumia takwimu,” amesema Letea ambaye amewahi kupata mafuta mafunzo kutoka Nukta Africa. 

Nukta Africa inamiliki tovuti ya habari ya www.nukta.co.tz na hufanya mafunzo kwa wanahabari na wadau wengine katika uandishi wa habari za takwimu na matumizi ya dijitali katika kuzalisha habari.