July 8, 2024

Mwigizaji filamu wa Mexico atembelea hifadhi nne za Taifa kwa mpigo

Ni Leticia Calderon mwigizaji liyeigiza sinema maarufu ya ESMERALDA.

  • Hifadhi hizo ni za Ngorongoro, Serengeti, Manyara na Tarangire.
  • Mwigizaji huyo wa Mexico amekuja akiambatana na familia yake.
  • Anaungana na mastaa wengine wa filamu kama Juhi Chawla,Jodi Sta.Maria waliotembelea Tanzania hivi karibuni.

Dar es Salaam. Muingizaji  maarufu wa filamu kutoka Mexico, Leticia Calderon (51) ametembelea hifadhi nne za Taifa za Ngorongoro, Serengeti, Manyara na Tarangire kwa mpigo na kusifia kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na hifadhi hizo za wanyama. 

Muigizaji huyo ambaye amefanya kazi hiyo kwa miaka 36 akiigiza  sinema maarufu kama ESMERALDA, yuko Tanzania kwa mapumziko ya siku saba kwenye hifadhi za wanyama za ukanda wa Kaskazini.

Leticia anaungana na waigizaji wengi waliowahi kutembelea mbuga zetu ambao ni Juhi Chawla kutoka India ambaye ameigiza filamu nyingi na mastaa wengine wa Bollywood kama Shah Rhuk Khan, Aamir Khan na wengine wengi.

Mwingine eliyetembelea hivi karibuni ni Jodi Sta.Maria kutoka Ufilipino ambaye wengi wanamjua kwa jina la Maya kutokana na tamthilia maarufu ya ‘Be Careful with My Heart’ aliyoigiza kama msichana wa kazi na kumpa umaarufu duniani

Mbali ya Esmeralda, filamu nyingine maarufu ambazo Leticia ameigiza ni En Nombre del Amor (In the Name of Love); Amor Bravia (Valiat Love) na La Indomable (The Taming of the Shrew).Pamoja na  tamthilia ndefu (soap operas) 29 katika jiji la Mexico City ambalo ni mji mkuu wa Mexico

Akisalimiana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyekuwa mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi, Leticia amesema amevutiwa na uzuri wa hifadhi za Tanzania na idadi kubwa ya wanyama aliowaona kwenye hifadhi za Taifa za Tarangire, Manyara na Ngorongoro.

“Kwa miaka mingi nilikuwa natamani sana kuja Tanzania kuona wanyama. Tuliyoyaona yametufurahisha mimi pamoja na wanangu. Nchi yenu ina uzuri wa kustaajabisha. Watu wenu ni wema na wakarimu,” .amesema mama huyo katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu. 

“Ninafurahi kwamba ndoto yangu imetimia. Tulienda Tarangire, Manyara na Ngorongoro ma sasa tunajiandaa kwenda Serengeti. Tulipokuwa Ngorongoro, tuliona simba wanne, majike wawili na madume wawili. Tumefurahi sana na nikirudi nyumbani, nitawaonyesha picha marafiki zangu na kuwaalika waje kutembelea Tanzania,” ameongeza.

Leticia ambaye amefuatana na wanaye wawili Luciano Collado (15) na Carlo Collado (14) alisema wakimaliza mapumziko yao huko Serengeti watakwenda Masai-Mara kwa siku tatu na kisha wataelekea Paris, Ufaransa kumtembelea rafiki yake ambaye waliigiza filamu pamoja huko nyuma.

Majaliwa alimshukuru mwanamama huyo na wanaye kwa kuichagua Tanzania kwa mapumziko yao na akawatakia heri katika safari yao ya mbugani.


Zinazohusiana:Mastaa walivyoitangaza Tanzania kimataifa 2018


Akizungumza na wafanyakazi wa hoteli ya The Retreat at Ngorongoro iliyoko Karatu ambako muigizaji huyo alikuwa amefikia, Waziri Mkuu aliwataka wafanyakazi wa hoteli hiyo na wengine walioko kwenye hifadhi za Taifa, wafanye kazi kwa bidii ili huduma zao ziwavutie watalii wengi zaidi.

“Tunampongeza mwenye hoteli kwa uwekezaji huu mkubwa lakini niwasihi wafanyakazi mchape kazi ili wageni wengi zaidi waweze kuvutiwa na huduma zenu,” 

“Sasa hivi tunapata watalii wengi na watu maarufu kama hawa, wamechagua kuja kupumzika Tanzania. Mheshimiwa Rais Magufuli ameshanunua ndege sita, nyingine mbili zinakuja, moja itawasili Oktoba, na nyingine Januari, mwakani. Na tayari kuna ndege tatu nyingine zimeagizwa. Lengo lake ni kuimarisha usafiri wa ndani kwa kutumia ndege,” amesema Waziri Mkuu.

Majaliwa amesema zamani ilikuwa ni vigumu sana kuja Tanzania moja kwa moja. Ili mtalii afike, ilibidi apitie nchi nyingine na huko akidakwa anaondokea hukohuko. Sasa hivi, akitoka kwao ataweza kuja Tanzania moja kwa moja, akitua KIA anakuja Karatu au Serengeti moja kwa moja.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Muigizaji wa Tamthilia maarufu ya ESMERALDA kutoka nchini Mexico, aliyekuja nchini kwa mapumziko ya siku saba na watoto wake, wakati Waziri Mkuu akiwa mkoani Arusha kwenye ziara ya kikazi. Julai 23.2019. Tokea kushoto ni watoto wa muigizaji huyo, Carlo Collado (14) na Luciano Collado (15). Picha | Ofisi ya Waziri Mkuu.